MSHAMBULIAJI wa Mashujaa, Ismail Mgunda, amesema matarajio yake makubwa msimu huu ni kuhakikisha anaingia katika orodha ya wachezaji watakaokuwa wanatajwa kwa mabao mengi ndani ya Ligi Kuu Bara.
Msimu uliyopita kabla ya kwenda kujiunga na AS Viya ya DR Congo, mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili, kitu ambacho anakitamani katika Ligi Kuu inayoendelea kufanya vitu vikubwa.
“Japokuwa sijaanza kucheka na nyavu katika mechi mbili tulizocheza tukiifunga Mtibwa Sugar (1-0) na tukitoka sare (1-1) dhidi ya JKT Tanzania, nina imani kubwa ya kufanya vizuri msimu huu.
“Kitu kikubwa ninachokifanya baada ya mazoezi ya timu na binafsi napumzika inavyotakiwa, nakula vizuri na kunywa maji ya kutosha ili kuupa mwili nguvu ya kupambana nikiwa ndani ya uwanja,” alisema Mgunda.
Mgunda alisema anatambua Ligi Kuu ya msimu huu itakuwa ngumu, lakini kitu cha msingi kwa mchezaji ni kujitunza ili kiwango chake kuwa juu kuja kuisaidia timu.
“Ni ligi inayohitaji kutumia akili kubwa, nguvu na mchezaji kuwa na mwendelezo wa kiwango ili kuisaidia timu kushinda mechi zake,” alisema.