Bosi Yanga ajitoa muhanga! Ajibu malalamiko

YANGA inaendelea kutoa vipigo lakini kuna baadhi ya watu kama hawaridhiki hivi, sasa uongozi umeibuka na kutoa msimamo mzito juu ya kocha wao Romain Folz.

Aliyetoa kauli hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, akisema wala wao kama uongozi hawana presha na kikosi chao kwa sasa na wamemuachia nafasi Folz kuwatengenezea kikosi imara.

Gumbo alisema kwa sasa ni mapema kutoa tathimini yao kubwa kwa kuwa timu yao ipo chini ya benchi jipya la ufundi linaloendelea kuwasoma wachezaji wao wapya na wale waliokuwepo kabla.

Bosi huyo aliongeza kuwa, mpaka sasa timu yao ipo njia salama kwa kuwa wameonyesha ukomavu mkubwa kwenye mechi zote walizocheza wakishinda vizuri.

“Tumesikia hizo taarifa lakini nadhani ni mitazamo tu tunatofautiana na namna tunavyopima mambo, unajua Yanga ina uongozi makini sana na mpira ni mchezo wa hadharani, hakuna asiyejua hii timu ipo chini ya kocha mpya na amekutana na wachezaji wapya na wale ambao tulikuwa nao kabla,” alisema Gumbo.

“Ukishapata kocha mpya, unatakiwa kumpa nafasi afanye kazi yake na ukaingalia kuanzia wiki ya Mwananchi ambao ulikuwa mchezo wa kirafiki, tukaja kucheza na Simba na juzi kule Angola kuna mwanga unaonekana.

“Timu imeshinda kwanza mechi zote lakini kama haitoshi, timu inatengeneza nafasi za kutosha tu, kitu muhimu hapa tunatakiwa kuongeza kiu ya kupata mabao mengi, hili tunamwachia kocha na wachezaji.

“Hatujaruhusu bao lolote lakini jambo zuri zaidi kuna ubora wa kiufundi unaonekana wakati wa kubadilisha wachezaji, nadhani bado kocha anaendelea kuwasoma taratibu wachezaji wake.”

Aidha Gumbo ambaye ameongoza kamati hiyo kwenye safari ya Yanga kubeba mataji misimu minne, aliongeza kuwa mashabiki wa timu yao kwa sasa wanatakiwa kuendelea kuwa nyuma ya timu yao kwani msimu bado uko hatua ya mwanzo wakiwa bado hawajaanza ligi.

“Mimi nadhani pia mashabiki wetu na wanachama hawatakiwi kuingia kwenye mkumbo, inawezekana wanaosema hivi ni wale ambao hawatupendi, tujikite kujaa uwanjani kuwapa nguvu wachezaji na makocha wetu wakati huu wanaendelea kuimarika,” alisema.

Yanga ambayo leo inaanza kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa nyumbani dhidi ya Pamba Jiji, tayari imeshinda mechi zake mbili za kimashindano ile ya Simba (1-0) na kuchukua Ngao ya Jamii, kisha ikaifunga Wiliete ya Angola (3-0) kwenye mchezo wa awali wa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini.