Uhakiki anuani za makazi kufanyika Mbeya, wananchi 481,000 kufikiwa

Mbeya. Zaidi ya wananchi 481,000 jijini Mbeya wanatarajiwa kufikiwa na shughuli ya uhakiki na uhuishaji wa taarifa za anuani za makazi litakalodumu kwa takribani siku 14 kuanzia Septemba 25, 2025.

Uhakiki huo unatarajiwa kumaliza kero na changamoto ya wananchi wanaokosa huduma mbalimbali kutokana na kutosomeka katika mfumo ‘data base’ na badala yake kusaidia upatikanaji wa huduma kwa karibu na kufikiwa kwa haraka.

Akizungumza leo Septemba 23, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa shughuli hiyo jijini hapa, lililoshirikisha wenyeviti na watendaji wa mitaa na kata, Ofisa Tehama kutoka Wizara ya Mawasiliano, Tekonolojia ya Habari, Rehema Chillo amesema suala hilo ni la kawaida na mwendelezo kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara.

Amesema taarifa zinazochukuliwa ni za kijiografia, majengo, huduma, wamiliki na wategemezi wa anuani, akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi wakati watendaji wanapofika nyumbani kwa ajili ya majukumu hayo kuisaidia Serikali kupata takwimu.

“Taarifa za anuani za makazi zinabadilika, kwa maana hiyo shughuli hii itakuwa ni pamoja na kuhuisha, kuboresha na kutoa anuani kwa ambao hawakupata hapo awali kwa ajili ya kuingizwa katika mfumo wetu wa kidigitali,” amesema.

Baadhi ya wenyeviti watendaji wa mitaa na Watendaji wa Kata walioshiriki hafla hiyo iliyoambatana na mafunzo kwao.



Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema tangu mwaka 2022 hadi sasa yamekuwapo mabadiliko ikiwamo nyumba mpya, viwanja vipya na watu kuhama, hivyo hakuna budi kuendelea kuhakiki na kukusanya taarifa za anuani ili kuwa na kanzi data na serikali itoe huduma.

Amesema yapo mambo kadhaa yanayoisukuma nchi kuwa na mifumo imara wa anuani za makazi, ikiwa ni manufaa ya mfumo wenyewe kuimarisha utambuzi, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ajenda 2030 na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

“Ili kujenga jamii yenye maisha bora na maendeleo endelevu na uchumi kamili wa kidigitali, lazima tuwe na mfumo imara wa anuani za makazi, wasaidie wananchi kumaliza changamoto zao za majina ya barabara na kupewa nafasi ya kupendekeza majina wenyewe,” amesema Itunda.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Abdullah, Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimali watu, Josephine Mwaijande amesema hadi sasa halmashauri zaidi ya 40 nchini zimefikiwa kwa uhakiki huo na juhudi zinaendelea kuzifikia nyingine zilizobaki.

Amesema katika halmashauri zilizohakikiwa, wamesajili na kutoa anuani mpya 535,856 ikiwa ni uthibitisho wa ongezeko la makazi mapya ambayo yanahitaji kupatiwa anuani.

“Tunarajia kuboresha taarifa za wananchi na kutatua changamoto ya majina ya barabara na mtiririko wa anuani utaboreshwa, Wizara imejipanga kuwajengea uwezo watalaamu na tayari 9,072 wamenufaika,” amesema Josephine.

Ameongeza kuwa matarajio yao baada ya kukamilisha hilo, kero ya utambulisho wa mitaa itakwisha huku akibainisha kuwa hadi kufikia Septemba 21, mwaka huu, jumla ya barua 668,558 za utambulisho wa makazi kidigitali za mfumo wa namba zilitolewa nchini.

“Katika halmashauri ya Jiji la Mbeya, barua 14,325 zimeombwa, ambapo zote zimefanyiwa kazi, niwapongeze waratibu wote kwa kufanikisha huduma hii na shughuli hii ni endelevu,” amesema Josephine.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Jiji la Mbeya, Daud Dule amesema kumekuwa na vilio kwa baadhi ya wananchi ambao walipitwa awamu ya kwanza kutopata anuani za makazi.

“Mbali na mafunzo ya leo, tunaenda kuhamasisha wananchi kutoa ushirikiano lakini kuwaelekeza umuhimu wa anuani hizi kwa kuwa faida yake ni kubwa kwao, kila barua yoyote lazima iainishe anuani,” amesema Dule.

Naye Kotrida Sanga ambaye ni Mtendaji wa Mtaa wa Ndeje, Kata ya Iwambi, amesema kumekuwapo na changamoto ya baadhi ya watu wasio na nia njema kuondoa nguzo na vibao vya anuani katika maeneo ya mtaa huo.

“Kutokana na kero hiyo, tumekuwa na vikao kadhaa vya wananchi ambapo tumeunda askari wa jadi (Sungusungu) ili kuimarisha ulinzi na usalama, hatua hii ya uhakiki wa anuani za makazi italeta tija,” amesema Kotrida.