Dar es Salaam. Kila mwaka, baada ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, maelfu ya watoto nchini hupata likizo ndefu ya takribani miezi mitatu wakisubiri matokeo na nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza.
Kwa mtazamo wa kawaida, kipindi hiki huonekana kama muda wa kupumzika na kujifurahisha baada ya safari ndefu ya kujiandaa kwa mtihani wa darasa la saba.
Lakini ukweli ni kwamba huu ni muda muhimu sana katika maisha ya mtoto, na unahitaji kutazamwa kwa umakini na wazazi, walezi pamoja na jamii kwa ujumla.
Kwa hakika, ni kipindi cha faraja na pumziko, lakini pia ni muda wa maandalizi mapya. Miezi hii mitatu inaweza kuwa daraja la mafanikio au sababu ya kurudi nyuma kwa mtoto, kulingana na namna inavyotumika.
Watoto wa darasa la saba hukabiliana na shinikizo kubwa la masomo kwa muda mrefu kabla ya kufanya mtihani wa kitaifa.
Wamekuwa wakiamka mapema, kusoma zaidi ya kawaida, na mara nyingi hukosa muda wa burudani. Kwa hiyo, mapumziko ya miezi mitatu yanaweza kuwa nafasi ya kurejesha afya ya mwili na akili.
Watoto wanahitaji muda wa kucheza, kuonana na ndugu wa familia, kujihusisha na michezo na hata kushiriki shughuli ndogo ndogo za kijamii. Pumziko hili huwasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuingia kwenye hatua mpya ya maisha yao wakiwa na ari na nguvu mpya.
Lakini pamoja na umuhimu huo, ni kosa kubwa kuwatelekeza watoto bila mwongozo wakati wa likizo hii ndefu. Kukaa bila mpangilio kunaweza kuwafanya waingie kwenye makundi yasiyofaa, kupoteza muda kwa michezo ya ovyo, au hata kuanza kujifunza tabia zisizo na faida.
Miezi mitatu ya kusubiri matokeo na shule mpya, inapaswa kutazamwa kama ngazi ya maandalizi ya maisha ya sekondari. Wazazi na walezi wanapaswa kuwasaidia watoto kuingia ngazi ya kidato cha kwanza kwa njia mbalimbali.
Lugha, hasa Kiingereza, ni moja ya changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi wanapoingia sekondari. Ni muhimu likizo hii ikatumiwe kuwapa watoto mafunzo ya lugha kupitia vitabu, mafunzo ya darasani au hata mazoezi ya kila siku nyumbani.
Lugha ikijengwa mapema, mtoto ataingia sekondari akiwa na ujasiri zaidi wa kuelewa masomo.
Mbili, kompyuta na teknolojia
Dunia ya leo inatawaliwa na teknolojia. Shule nyingi, hasa za sekondari, zinahitaji mwanafunzi kuwa na uelewa wa msingi wa kompyuta. Ni vyema wazazi wakawatafutia watoto kozi fupi za kompyuta, hata kama ni za wiki chache. Ujuzi huu utawasaidia sio tu shuleni, bali pia katika maisha ya kila siku.
Tatu, mafundisho ya dini na maadili
Pamoja na masomo ya kitaaluma, mtoto anahitaji misingi imara ya kimaadili na kiroho.
Likizo ndefu inatoa nafasi nzuri ya kushiriki mafundisho ya dini katika makanisa, misikiti au vikundi vya kijamii. Mafundisho haya husaidia kumjenga mtoto kimaadili, kumfundisha heshima, uadilifu na kumuepusha na vishawishi vya uovu mitaani.
Nne, shughuli za kimaisha
Mbali na masomo ya darasani, watoto wanapaswa kujifunza ujuzi wa maisha kama vile kufanya kazi za nyumbani, kushiriki shughuli ndogo za kilimo au biashara, na kujifunza stadi za kijamii. Hii huwajenga kiakili na kuwaandaa kukabiliana na maisha ya baadaye.
Wajibu wa wazazi na walezi
Kipindi hiki cha miezi mitatu pia ni mtihani kwa wazazi. Wajibu wao ni mkubwa zaidi kuliko ilivyo wakati wa masomo. Ni kipindi kinachohitaji nidhamu na uangalizi makini.
Kwanza, wazazi wasikubali likizo hii iwe ya mtoto kukaa tu nyumbani bila mpangilio. Ni lazima kuwe na ratiba ndogo ya shughuli zinazomjenga mtoto. Ratiba hiyo isiwe nzito kupita kiasi, bali iwe ya uwiano kati ya burudani, mapumziko na mafunzo.
Pili, wazazi wanapaswa kufuatilia mwenendo wa watoto wao. Miezi mitatu ni muda mrefu ambao unaweza kumgeuza mtoto ama kuwa na maadili mazuri au kujiingiza kwenye makundi mabaya ya mitaani. Ukaribu wa wazazi na watoto wakati huu ni jambo lisiloepukika.
Tatu, wazazi wanapaswa kutumia kipindi hiki kufikiria mustakabali wa kielimu wa watoto wao. Hii ni pamoja na utafutaji wa shule bora za sekondari.
Mara nyingi wazazi hukimbilia shule binafsi wakiamini ndizo bora zaidi. Ni kweli kwamba shule nyingi binafsi zimekuwa zikitoa matokeo mazuri, lakini wazazi wanapaswa kuwa makini zaidi.
Si kila shule binafsi inaendeshwa kwa kiwango bora. Baadhi ni za kibiashara zaidi kuliko za kielimu. Wazazi wanapaswa kuchunguza walimu waliopo, mazingira ya kujifunzia, na sera za shule kabla ya kufanya uamuzi.
Pili, wazazi wasikubali kuingizwa katika gharama zisizo na tija. Kuna shule zinazotoza ada kubwa bila kuonyesha thamani halisi ya fedha hizo. Ni muhimu kuangalia uwezo wa kifedha wa familia na kuhakikisha mtoto anapata elimu bora bila familia kuingia kwenye mzigo mkubwa na hatimaye kusumbua watoto kwa kuwahamisha.
Tatu, shule za Serikali nazo zimeendelea kuboresha miundombinu na walimu. Kwa hiyo, wazazi hawapaswi kuzidharau moja kwa moja. Ni busara kulinganisha kwa umakini kabla ya uamuzi.
Kwa upande wa jamii, nayo ina wajibu mkubwa katika kipindi hiki. Miezi mitatu ya watoto kukaa nyumbani inahitaji ushirikiano wa viongozi wa mitaa, taasisi za dini na asasi za kiraia.
Mashirika haya yanaweza kuandaa kambi za mafunzo, michezo na warsha za kuwajengea watoto stadi mbalimbali.
Aidha, shule za msingi zinaweza kuendelea kutoa mwongozo wa kile watoto wanaweza kufanya wakiwa likizo. Kwa mfano, kutoa vitabu vya ziada au mapendekezo ya mafunzo ya nyumbani.
Miezi mitatu baada ya darasa la saba si kipindi cha kupoteza. Ni safari muhimu katika maisha ya mtoto.
Huu ni muda wa kupumzika baada ya mashindano marefu ya elimu ya msingi, lakini pia ni ngazi ya maandalizi ya safari mpya ya sekondari.
Wazazi na walezi hawapaswi kuacha watoto wao waishi ovyo bila mwelekeo.
Ikiwa kila mzazi, mlezi na taasisi za kijamii zitashirikiana ipasavyo, basi kipindi hiki cha miezi mitatu kitapoteza jina la kuwa likizo ndefu isiyo na maana na badala yake kitakuwa daraja la kujenga kizazi cha vijana wenye maarifa, maadili na nidhamu ya kuongoza Taifa kuelekea mustakabali bora.