Moto ghorofa Kariakoo, hakuna majeruhi wala vifo, Zimamoto wafunguka

Dar es Salaam. Ajali ya moto iliyotokea katika mtaa wa Narung’ombe, Kariakoo baada ya jengo lenye ghorofa saba kuungua, imeelezwa hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kufariki dunia.

Jengo hilo ambalo ni maarufu kwa uuzaji wa viatu vya jumla na rejareja pia hutumika kuhifadhia mizigo ya wafanyabiashara mbalimbali waliopanga eneo la Kariakoo, liliungua jana Septemba 22, 2025.

Katika ajali hiyo ghorofa ya tano na ya sita ndizo zilizoathiriwa na moto huo, ilizua taharuki miongoni mwa wafanyabiashara na wakazi wa Kariakoo, ukizingatia imepita siku chache tangu jengo jingine liungue katika maeneo hayo.

Mwananchi ilifika eneo hilo leo Jumanne, Septemba 23, 2026 na kukuta baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wanahamisha bidhaa zao, huku maduka machache yakiwa yamefunguliwa hususan upande wa nyuma wa jengo hilo.


Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kuhusu tukio hilo, amesema wanashukuru katika ajali hiyo licha ya kuteketea kwa baadhi ya mali, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kufariki dunia.

Sambamba na hilo, Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi na hakuna mfanyabiashara aliyeibiwa mali baada ya askari kufika mapema katika eneo hilo, kufuatilia hali ya usalama na kuhakikisha utulivu katika kipindi chote cha shughuli za uokozi.

“Tunashukuru tuliweza kulinda mali za wafanyabiashara zilizokuwepo ndani na nje ya jengo hilo na hakuna aliyeibiwa hata jozi moja ya kiatu.

“Lakini kubwa ni kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza uhai hadi moto ulipomaliza kudhibitiwa na Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji. Hakika walifanya kazi nzuri na wanastahili kupongezwa,” amesema Kamanda huyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi, akizungumzia hali ya uokoaji ilivyokuwa, amesema walipata changamoto hususani kwa wafanyabiashara kuziba njia.

Kamanda Mabusi amesema ni kutokana na hali hiyo, iliwachukua muda kulifikia jengo hilo na kuanza kuudhibiti moto huo, kwa kuwa magari yao yanahitaji nafasi kubwa ili kukata kona.

“Kwa kweli, wafanyabiashara kupanga bidhaa zao kwenye barabara za kuingia na kutoka eneo la Kariakoo imekuwa tatizo. Tumeingia kwa shida sana hadi tumeumiza magari yetu kwa kugonga meza za wafanyabiashara, kwa kuwa ukimwambia mtu asogee, anasogeza meza yake kidogo tu,” amesema Kamanda huyo.

Kutokana na hali hiyo, amesema bado kunahitajika hatua zaidi pamoja na elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuacha njia wazi, kwani kuzizuia hakuathiri tu wapita njia au wafanyabiashara wa maduka makubwa, bali pia huchangia kuchelewesha msaada wa haraka pindi ajali kama moto zinapotokea, kutokana na magari ya uokoaji kushindwa kufika eneo husika kwa urahisi.

Pia, amewashauri wafanyabiashara kutafuta maghala au stoo nje ya maeneo ya Kariakoo, akieleza kuwa eneo hilo kwa sasa limejaa kupita kiasi.

Baadhi ya wafanyabiashara wakihamisha bidhaa zao kwenye maduka



Alisema kuwa kuhifadhi bidhaa zao nje ya Kariakoo kutawapa nafasi ya kutumia maeneo yenye nafasi kubwa na yaliyo wazi, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi na usalama wa biashara zao.

Catherine Kimaro, amesema anaona mabadiliko chanya katika utendaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hasa kwa kuzingatia aina ya magari ya kisasa waliyotumia katika tukio hilo, yakiwemo yale yenye uwezo wa kufika hadi katika ghorofa za juu, jambo ambalo awali halikuwepo.

“Jamani, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Zimamoto wa leo si wale wa zamani waliokuwa wakifika eneo la tukio bila hata maji. Jana tumeona teknolojia ya kisasa, magari yao yameweza kufika hadi ghorofa za juu na kudhibiti moto kwa ufanisi,” amesema Catherine.