Arusha/Katavi. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amesema anasikitishwa na ugumu wa maisha unaowakabili Watanzania ilhali Taifa limebarikiwa rasilimali nyingi.
Akihutubia wananchi wa USA River kwenye mkutano wa kampeni sambamba na kukiombea kura chama chake leo Jumatatu Septemba 22, 2025 Jimbo la Arumeru Mashariki, Minja amesema haiwezekani wananchi wakakosa hata Sh1,000 mfukoni huku kilo moja ya mchele ikiuzwa kwa Sh3,000, jambo linalowafanya wengine washindwe hata kunywa chai ya asubuhi kutokana na ukosefu wa fedha.
“Serikali ya Chaumma itahakikisha mazingira ya upatikanaji wa chakula yanaboreshwa na ajira za kutosha zinapatikana. Mchele utashuka bei hadi Sh500 kwa sababu tutapunguza gharama za uzalishaji. Ajira zitatokana na utalii na kilimo, ardhi tutawagawia wananchi walime,” amesema mgombea mwenza huyo.

Amesema Taifa lina utajiri mkubwa wa bahari, maziwa, mito, ardhi yenye rutuba, madini na vivutio vya utalii, lakini changamoto zilizopo zinatokana na mikakati mibovu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoiongoza Serikali.
“Tupeni sisi Chaumma nchi ili tuje na mikakati mizuri na inayotekelezeka, hamtajuta,” amesisitiza.
Katika sera za kilimo, Minja amesema Chaumma itawekeza katika viwanda vya mbolea, viuatilifu na dawa ili kuongeza tija, sambamba na kutoa matrekta na zana bora za kilimo kwa bei nafuu. Amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na akiba ya chakula na wananchi hawapati njaa.
“Mchele ukiuzwa Sh500 watu watapata nafuu. Wakiwa na uhakika wa chakula wataweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Hatutaki mtu akienda hospitali akose chakula, kila kaya iwe na uhakika wa chakula,” amesema Minja.

Aidha, amesema uchaguzi wa mwaka huu ni fursa ya kuiondoa CCM madarakani.
“Tutaenda nao bampa tu bampa hadi kieleweke. Watu tujitokeze kwa wingi Oktoba 29 tukapige kura na ninawaomba tuipigie kura Chaumma,” amesema.
Katika hatua nyingine, mgombea ubunge wa Kavuu kwa tiketi ya Chaumma, Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, Iddi Mabembenya amesema wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa katika miundombinu ya barabara, upungufu wa maeneo ya malisho kwa mifugo pamoja na ukosefu wa soko la uhakika kwa mazao yao, hususan mpunga na mahindi.
Mabembenya amesema hali hiyo inarudisha nyuma juhudi za wakulima na wafugaji katika kukuza uchumi wa jimbo hilo.