Kero ya maji kwa siku saba yamuibua RC Mtanda

Mwanza. Kwa zaidi ya wiki moja sasa wakazi wa baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza wamekosa huduma ya maji baada ya pampu na vifaa vya kusambazia maji katika chanzo cha Butimba kuungua kutokana na hitilafu ya umeme.

Changamoto hiyo imeathiri upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ikiwamo Mkuyuni, Buhongwa na Mkolani. Wakazi wa maeneo ya jirani na Ziwa Victoria wanaendelea kupata nafuu kwa kuchota maji ziwani, lakini walio mbali na ziwa wanalazimika kununua dumu la maji la lita 20 kwa Sh1,000 au kutumia kwenye madimbwi.

Happyness Charles, mkazi wa Nyamazobe A, amesema kero hiyo imewalazimisha wakazi kutafuta vyanzo vingine visivyo salama kwa afya.
“Maji haya si salama, yanaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, lakini ndiyo tunayoyatumia kwa kupikia, kunywa, kufulia na kuoga kwa kuwa maji ya bomba hayajapatikana kwa zaidi ya wiki,” amesema.

Mwananchiilipotembelea eneo la Luchelele, lilikuta bodaboda wakibeba madumu ya maji wakiuza dumu moja kwa Sh1,000, huku wakisema uhaba huo wa maji kwao ni fursa ya kujipatia kipato.

“Hii ni fursa kwetu kama bodaboda. Ukibeba madumu 10 unapata Sh10,000. Lakini tatizo ni kwamba hata mama ntilie sasa wanapika kwa maji haya yasiyo salama, jambo linalotishia afya zetu,” amesema mmoja wa waendesha pikipiki hao aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Akizungumzia changamoto hiyo leo Jumanne  Septemba 23, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema limesababishwa na kuungua kwa pampu na vifaa vingine kulikosababishwa na hitilafu ya umeme katika chanzo cha maji cha Butimba.

“Kwa wiki moja tumekuwa na upungufu wa maji kutokana na pampu kuungua. Chanzo cha Butimba pekee huzalisha zaidi ya lita milioni 48 kwa siku. Kwa sasa ukarabati umefikia asilimia 80 na kuanzia leo jioni baadhi ya maeneo yatapata huduma kama kawaida,” amesema Mtanda.

Amesema wataalamu wamebadilisha mfumo wa kuendesha mitambo ili kuepusha madhara endapo kutatokea kuyumba kwa umeme tena. Pia, amebainisha kuwa mahitaji halisi ya maji jijini Mwanza ni lita milioni 180 kwa siku, lakini uzalishaji wa miradi ya Capripoint na Butimba kwa pamoja ni lita milioni 138 pekee, hivyo kuna upungufu wa lita milioni 40.

Mtanda ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mradi wa upanuzi wa chanzo cha Capripoint, ambacho sasa huzalisha lita milioni 90 kwa siku, na baada ya kukamilika kitazalisha lita milioni 44 zaidi. Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Suma JKT.

Jabiri Suleyman, mkazi wa Mkolani ameshauri mamlaka husika kuweka utaratibu wa kuwa na vifaa vya akiba ili wananchi wasipate usumbufu endapo changamoto kama hiyo itajirudia.
“Wiki nzima bila maji ni muda mrefu sana. Ingekuwa vizuri wangeweka mbinu mbadala au vifaa vya akiba,” amesema.