Maswa. Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza, wameweka kambi ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Wananchi waliofika kupata huduma wamesema uwepo wa madaktari hao utawapunguzia gharama za kusafiri kwenda hospitali za mbali kufuata matibabu.
Seif Lyale, mkazi wa Mtaa wa Biafra A mjini Maswa, amesema amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kifua na uwepo wa madaktari hao umemrahisishia kupata matibabu kwa karibu.
“Badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda kuonana na madaktari bingwa, sasa nimepata huduma hapa Maswa. Imenipunguzia gharama za usafiri na matibabu,” amesema Lyale.
Esther Malale, mkazi wa Kijiji cha Budekwa, amesema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya macho na hakupata nafuu katika hospitali nyingine, lakini sasa ana matumaini baada ya kukutana na daktari bingwa wa macho.
Kwa upande wake, James Haraka kutoka Kijiji cha Lalago, amesema amempeleka mtoto wake mwenye matatizo ya kuota nyama puani, hali iliyomsababishia shida ya kupumua.
“Niliposikia kuna daktari wa masikio, koo na pua, niliona nimlete mwanangu. Nina imani kubwa kuwa atapona,” amesema Haraka.
Naye, Sarah Amir, mkazi wa Kijiji cha Senani amesema mtoto wake wa miaka miwili aliyekuwa akisumbuliwa na matatizo ya usikivu amepata matibabu na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa kuondoa nyama zilizoota masikioni.
Dk Masumbuko Madebele, bingwa wa magonjwa ya masikio, koo na pua, amesema wamebaini wagonjwa wengi wa eneo hilo wamepoteza usikivu kutokana na matatizo ya masikio kupiga kelele au kutoa usaha.

Sehemu ya wagonjwa waliojitokeza kupata matibabu kwa madaktari bingwa katika hospitali ya wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga
“Tumegundua baadhi ya wagonjwa wanategemea dawa za miti shamba. Tunawaomba waendelee kufika kwenye kambi hii wapate matibabu bora ya kibingwa,” amesema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki amesema kambi hiyo imesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Hospitali ya Bugando, jambo linaloonyesha mahitaji makubwa ya huduma hizo katika wilaya hiyo.
“Awali tulikuwa tunawalazimisha wagonjwa kusafiri hadi Bugando, lakini sasa wanapata huduma hapa. Tuna mpango wa kuendeleza utaratibu huu kwa sababu tumeona unasaidia wananchi wengi,” amesema Dk Mtaki.