Hai. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devota Minja ameahidi chama chake kitatua changamoto ya upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vya afya nchini, ikiwamo katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, kama kitapatiwa ridhaa ya kuongoza nchi.
Akizungumza leo Jumanne Septemba 23, 2025 na wakazi wa Bomang’ombe katika mkutano wa kampeni, Minja amesema sekta ya afya ni kipaumbele cha kwanza endapo chama hicho kikiingia madarakani.
Amesema wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kufika hospitalini kwa ajili ya vipimo na tiba, lakini huambiwa hakuna dawa na kulazimika kununua katika maduka ya binafsi, jambo alilosema si sahihi.
“Ni kweli, Chaumma tukipewa ridhaa ya kuongoza nchi, mambo haya yatabaki historia. Hospitali, zahanati na vituo vya afya lazima viwe na dawa. Hakuna haja ya kumwambia mwananchi akanunue dawa kwa sababu wao ni walipakodi,” amesema Minja.
Akiendelea na ziara yake ya siku tatu ya kampeni mkoani Kilimanjaro, Minja pia amefanya kampeni katika maeneo ya Sadala na Masama Mula, ambako amewanadi madiwani na wabunge wa chama hicho.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Hai kupitia Chaumma, Jemsi Mbowe amesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni ajira kwa vijana.
Hivyo, ameahidi kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira kwa kupandisha wageni Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Machema, likisaidiwa na kampuni iliyopo wilayani humo.
Mbowe pia ameahidi kuboresha masoko ya Sadala na Masama Mula ili wananchi wafanye biashara katika mazingira bora hasa wakati wa mvua, akieleza kuwa masoko hayo yamekuwa yakikosa miundombinu licha ya kuingiza mapato kwa halmashauri.
Aidha, amesema atashughulikia changamoto za barabara alizozitembelea wakati wa kampeni na kuhakikisha maeneo yenye uhaba wa maji, hususan Bomang’ombe, yanapatiwa huduma hiyo.
Pia, ameahidi kuwasaidia wanawake kupata mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri ili kuwaepusha na mikopo ya masharti magumu.