Dar es Salaam. “Kama shida ilikuwa hela, angesema marehemu mume wangu hakumlipa mimi ningejua namlipaje, lakini si kudai nyumba ni yake.”
Ni kauli ya Alice Haule, mjane aliyefukuzwa kwenye nyumba anayodai ni yake iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam, huku vitu vikitolewa nje.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Alice amesema mtu anayedai nyumba ni yake alimkopesha fedha mume wake Justus Rugahibula (sasa ni marehemu).
“Sijui walikopeshana vipi, lakini ninavyosikia mume wangu na huyu mtu (anamtaja jina) walikuwa wakifahamia tangu mwaka 2010 na kukopeshana Sh150 milioni,” anasema.
Alice anasema mwaka 2012 mtu huyo alifanya jaribio la kumuondoa kwenye nyumba kama ilivyofanyika leo, wakati huo mume wake alikuwa hai ikashindikana.
“Mume wangu alisafiri kwenda Afrika Kusini, mimi nikiwa kwenye shughuli zangu Kariakoo, nikapigiwa simu nyumba yangu imevamiwa, bahati nzuri polisi waliwahi wakanisaidia kuzuia,” amesema.
Amedai baada ya tukio hilo alikwenda Wizara ya Ardhi kuweka zuio kwa kuwa mtu aliyemkopesha mumewe alikuwa na hati ambayo Alice anadai ni ya kughushi.
“Wizara ilitaka mume wangu akirudi kutoka Afrika Kusini wamalizane. Niliona document (nyaraka) mume wangu akieleza hakumuuzia nyumba, alimkopesha pesa. Nikasikia baadaye walilipana na mume wangu akataka arudishe hati ya nyumba,” anadai.
Amesema suala hilo lilikwenda likawa kimya, hivyo akajua tayari wamemalizana na limepita, kwani mtu aliyekuwa akimdai aliondoka nchini.
“Mwaka 2022 mume wangu alifariki dunia, ajabu miezi ya hivi karibuni nikaanza kupata vitisho kutoka kwa huyu mtu akiniita mvamizi kwenye nyumba yangu,” amesema.
Akizungumzia tukio la kutupiwa vitu nje lililotokea leo Septemba 23, 2025, amesema Ijumaa iliyopita, Septemba 19 alifungua kesi Mahakama ya Ardhi akidai hati ya nyumba yake.
Anadai pia aliwasilisha taarifa polisi kuhusu kosa la jinai la kughushi hati hiyo, lakini wakati wakiendelea na taratibu nyingine za kisheria ndipo watu wakavamia nyumba hiyo na kutoa vitu nje, wakishinikiza yeye ni mvamizi.
Tazama Mjane aliyevamiwa akidai kunyang’anywa nyumba Mikocheni aenda Polisi
“Nilipigiwa simu na serikali ya mtaa wakaniambia wamepata barua inatakiwa vitu vyangu vitolewe nje. Wakati watu hao wamefika nyumbani na kuanza kutoa vitu nilikuwa nimekwenda polisi kuomba msaada,” amesema na kuongeza:
“Nikatoka polisi na bodaboda nikakuta wamevunja geti, ndani kuna mabaunsa kama 18, nikaanza kupiga yowe, wakaanza kunipiga wakitoa vitu kwenye nyumba ya wapangaji wangu (Wachina) ipo mbele na kwangu ni nyuma, zote akidai ni zake.”
Akigumia kwa maumivu, amesema watu hao walimpiga na kumbeba juujuu kumtoa nje, kabla ya kuondoka baada ya waandishi wa habari kufika.
Alice amedai nyumba hiyo waliinunua pamoja na mume wake kwa gharama ya Sh470 milioni.
Amesema katika kukopa fedha, yeye hakuhusishwa, akieleza atapambania haki yake hadi mwisho.
Awali, kabla ya kwenye Hospitali ya Mwananyamala, Alice na binti yake alikwenda Kituo cha Polisi, Oysterbay.
Kutokana na tukio hilo, Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ameandika:
“Asante kwa ushirikiano, mama mjane amenitumia sms, nikampigia, nikamsikiliza. Kifupi amesema, mwanasheria anaye, kesi iko Polisi na pia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni anajua jambo hili.”
“Hata hivyo, changamoto zilizotokea ni huko kuvamiwa ghafla bila taarifa na kinyume na utaratibu stahiki wa kisheria ukizingatia kuwa, kesi iko Polisi. Hivyo, msaada wa haraka anaohitaji ni ulinzi wake na mali zake na dhidi ya hayo matishio anayopata,” ameandika Dk Gwajima.
Kuhusu hatua alizochukua amesema amewasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na RPC Kinondoni na kuomba, wafanye hatua stahiki ili mama mjane kwanza awe salama na utulivu kisha, hayo ya kisheria yaendelee kwa mujibu wa sheria ambapo, viongozi wote hao wamepokea kwa hatua stahiki.
“Aidha, saa 9:11 jioni nimeongea tena na mama mjane ambapo, ameniambia ni kweli Polisi walienda na wale waliokuwa wanamfanyia vurugu walitawanyika na sasa hali iko kwenye utulivu,” ameandika.
Dk Gwajima ametoa wito kwa wanaodai kununua nyumba ya mjane akisema:
“Ndugu, hata kama mnadaiana, tafadhali fuateni taratibu halali za kisheria kupitia kwa mwanasheria wa mjane huyu. Hata katika mapito ya kisheria, tafadhali kumbukeni kuwa na subira na utu uwe kwanza na hapo ndiyo kila mmoja atapata haki yake na Mwenyezi Mungu atapendezwa nanyi nyote na kuwabariki wote. Amina.”
Amesema: “Tuendelee kushirikiana kuzuia changamoto za kijamii na kuibua zinapotokea na kuzipatia mwongozo stahiki kwa wakati.”