Ngorongoro. Mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yannick Ndoinyo, ameahidi kuanzisha benki ya wafugaji endapo atachaguliwa, ili kuwawezesha wakazi wa eneo hilo hasa wafugaji kupata huduma za kifedha kwa urahisi, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu.
Mbali na hilo pia ameahidi kuanzisha kiwanda cha kusindika nyama ili wafugaji hao waweze kunufaika zaidi ya shughuli zao za ufugaji.
Ndoinyo ameyasema hayo leo Septemba 23, 2025 kwenye ziara ya kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza kwenye mikutano tofauti ya kampeni iliyofanyika katika kata za Olorieni, Magaiduru na Maaloni, Ndoinyo amesema kuwa anaona shida wanayopata wafugaji kwenye taasisi za kifedha hasa wanapohitaji mikopo au huduma za kifedha, hivyo suluhu ni kuanzisha benki ya wafugaji itakayojibu changamoto zote za kifedha watakazokumbana nazo.
“Mimi mwenyewe ni mfugaji, najua kila kitu kuanzia kupata mkopo au hata huduma zingine, hivyo nitaanzisha benki yetu wenyewe ambayo itatupa elimu ya kifedha mara kwa mara, lakini huduma zote muhimu tutakazohitaji za kutatua changamoto zetu wafugaji,” amesema.
Mbali na hilo ameahidi kuanzishwa kwa kiwanda cha kuchakata na kuuza nyama katika Wilaya ya Ngorongoro ili kusaidia kupandisha thamani ya mifugo yao.
“Kiwanda hiki kitasaidia kuchakata bidhaa zote za mifugo na kila kiungo kimoja kuuzwa kivyake na faida ya ufugaji wetu tutauona mara tatu hadi nne, kuliko sasa hivi tunauza mifugo wazima bila kupata faida ya ziada kutoka kwenye mifupa, ngozi wala nyama yake” amesema na kuongeza;
“Kikubwa naombeni kura zenu ifikapo Oktoba 29 na naomba mumpe kura zote Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) ili haya yote yakatekelezwe haraka iwezekanavyo kwani viko ndani ya ilani ya CCM.”
Katika mikutano yake, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali ikiwemo kuchelewa miradi mingi ya maendeleo na kukatisha wananchi tamaa.
Mkazi wa Kata ya Maaloni, Lucas Kaisemi, amesema kuwa moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa miundombinu ya daraja muhimu linalounganisha kata hiyo na barabara kuu, ambalo huathiriwa sana wakati wa mvua za masika, hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi.
“Kukamilika kwa daraja hili kungesaidia sana wananchi hasa kipindi cha mvua ambapo mawasiliano hukatika na kusitishwa kwa shughuli nyingi za kiuchumi kwani halipitiki, tunaomba utusaidie mara baada ya kuapishwa,” amesema.
Kwa upande wake Sakara Murkuk ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Lukumai amesema kero kubwa ni ujenzi wa ofisi ya mtendaji iliyochukua muda mrefu sambamba na mradi wa maji unaopita katika maeneo yao.
Akijibu hoja hizo, Ndoinyo amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya Sh88 bilioni kwa kipindi cha miaka minne iliyopita kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
“Kwa kushirikiana na Serikali na ninyi wenyewe nitahakikisha miradi yote iliyosalia katika ilani inatekelezwa kikamilifu na mingine tutakayoanzisha itakamilika ndani ya kipindi changu cha uongozi,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Lucas Olemasiaya amesema kuwa ziara hiyo ya kuwaombea kura Rais Samia pamoja na wagombea ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu watahakikisha inafanyika katika kata zote na kusikiliza kero za wananchi.
“Kiburi hiki tunapata kwa sababu Serikali imetekeleza kwa mafanikio makubwa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro ikiwamo kutupatia zaidi ya Sh88 bilioni,” amesema.