Waislam wa Ahmadiyya kuliombea Taifa amani

Dar es Salaam. Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania imesema itafanya mkutano mkuu wenye lengo la kuchochea upendo miongoni mwa waumini na kuongeza huruma, unyenyekevu baina yao.

Mkutano huo wa 54 wa mwaka (Jalsa Salana) utafanyika Septemba 26 hadi 28, 2025 katika viwanja vyao vilivyopo Kitonga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Septemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam, kuhusu mkutano huo Amiri na Mbashiri Mkuu, Khawaja Ahmad amesema madhumuni yake ni kumuwezesha kila mfuasi wa kweli kunufaika kiroho, kupanua elimu yake na kuongeza maarifa juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kupitia fursa na neema alizopewa.

Amesema  kuwa mkutano huo pia utahusisha wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini, pamoja na viongozi wa kijamii, ambao watapata nafasi ya kutoa nasaha zao.

Kwa upande wake, Naibu Amiri na Mbashiri Mkuu wa jumuiya hiyo, Abdulrahman Ame, amesema mkutano huo pia unalenga kuwakumbusha waumini juu ya wajibu wa kuheshimu na kutekeleza haki za binadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’an tukufu, sunna na hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W).

“Waumini na washiriki wote watapata fursa ya kusikiliza hotuba na nasaha kutoka kwa wataalamu. Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na haki za binadamu, malezi ya yatima, wajane na wazee, pamoja na haki za watoto na wagonjwa,” amesema Ame.

Ameongeza kuwa mada nyingine zitahusu athari za ulevi, kamari, mmomonyoko wa maadili katika jamii, haki na wajibu wa wanandoa katika ndoa na talaka, pamoja na uhuru wa kujieleza kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.

Naye Katibu wa mambo ya ndani wa jumuiya hiyo, Yahya Kambaulaya, amesema mkutano wa mwaka huu pia utatoa nafasi kwa waumini na washiriki kuliombea amani ya Taifa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

“Mwaka huu, maombi ya unyenyekevu na machozi kwa Mwenyezi Mungu yataelekezwa hasa kwa ajili ya kipindi hiki cha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa Tanzania Bara na Visiwani,” amesema Kambaulaya.

Aidha, mkutano huo pia utahusisha huduma ya uchangiaji damu salama kwa watu watakaokidhi vigezo vya kiafya, kama sehemu ya mchango wa jumuiya hiyo kwa jamii.

Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 6,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani.