Mbeya. Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amewataka wananchi kutokubali kurubuniwa kuingia kwenye vurugu za uvunjifu wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Fyandomo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 23, 2025 kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za kumnadi mgombea urais, wabunge na madiwani uliofanyika katika Mtaa wa Isoso, kata ya Mwasanga jijini Mbeya.
“Ndugu zangu msikubali kuingia kwenye vurugu na machafuko, wapo watu wanawashawishi wananchi kwa madai ya kutoona kazi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita jambo ambalo siyo kweli,” amesema.
Katika hatua nyingine, Fyandomo amesema kutokana na upofu walionao sasa, kama CCM watawaonyesha kwa vitendo miradi iliyo tekelezwa na ilani ya uchaguzi 2020/25 na ambayo inatekelezwa katika ilani ya 2025/30.
“Nimesimama kuomba kura za heshima za mgombea urais na mgombea ubunge wa Uyole, Dk Tulia ambaye ni dhahabu ya wana Uyole, kimsingi mmepata mtu mpiganaji na mpenda maendeleo,” amesema.
Amesema kama wanaCCM hawako tayari kumpoteza na kuona watu wachache wanaingia kuleta vurugu na machafuko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Mgombea udiwani wa Kata ya Mwasanga, Brandy Nelson ameomba wananchi kumpa ridhaa sambamba na kushawishi kura za wagombea nafasi ya Rais na wabunge.
Katika hatua nyingine, amejigamba kuleta maendeleo katika nyanja za elimu, barabara na ujenzi wa shule ya msingi Isoso kama sehemu ya kutekeleza ilani ya uchaguzi.
“Wananchi wa Isoso leo tumekutana hapa kwenye kampeni mmesikia haya niliyosema, pia niombe dada yangu Dk Tulia tusaidie kufikisha ombi, Mtaa wa Isoso hakuna shule ya msingi na uchakavu wa barabara,” amesema.
Akizingumza na wananchi wa Isoso, Dk Tulia amesema wamekuja kuomba kura za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mgombea udiwani, Brandy Nelson.
“Diwani wenu ameeleza kazi nzuri iliyofanyika katika kutekeleza ilani ya 2020/25 kwenye sekta ya elimu, lakini pia uwepo wa walimu wa kutosha ili watoto waweze kufanya vizuri,” amesema Dk Tulia.
Dk Tulia amesema ujio wa CCM katika kata hiyo kuomba kura kufuatia Rais Samia kutenda hisani ya kuleta maendeleo katika Mkoa wa Mbeya sambamba na kutekeleza ilani ya uchaguzi 2025/30.
“CCM ndiyo wenye ilani inayotekelezeka na maendeleo na ndio maana tunasema Samia mitano tena mchagueni kwa kura za kishindo ili mfikiwe na huduma muhimu,” amesema.
Kuhusu ombi la shule ya msingi Isoso, Dk Tulia amewataka wananchi waondoe hofu, ujenzi wa miundombinu mipya ya shule itajengwa endapo wanachi watamchagua Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Dk Tulia amewataka wananchi kuwa watulivu kwani mambo mazuri yanakuja sambamba na kugusa nyanja mbalimbali.
Amesema wapo wanaojisahaulisha kwa madai ya mgawo wa umeme, Serikali ya CCM imefikisha huduma maeneo mbalimbali na suala la mgao wa umeme halipo.
“Serikali imetekeleza mradi mkubwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere, hivyo ijulikane tuna nishati ya kutosha na kuuza nje ya nchi,” amesema.