Mtwara. Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameendelea na mikutano ya kampeni ya kunadi ilani ya chama hicho na leo amewomba ridhaa wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Samia ambaye ameanza kampeni mkoani humo leo Jumanne, Septemba 23, 2025 amepokelewa na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika wilaya za Nanyumbu na Masasi.
Katika mkutano huo, aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Nanyumbu kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Hamad Kadoma ametangaza kuhamia CCM kwa kile alichoeleza kuridhishwa na kazi zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Samia.
Kadoma amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi akiwa na Chama cha Wananchi (CUF) na sasa ACT-Wazalendo katika Kurugenzi ya Mipango na Uchaguzi wa Jimbo la Nanyumbu kabla ya leo kuhamia CCM.
“Nimevutiwa na mienendo na muonekano wa CCM, nimeangalia kwa umakini mikutano ya Samia, amenipa matumaini kuwa mama anaweza. Ameweza kuendeleza miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake basi nina imani atatufikisha mbali.
“Nimekuja hapa bila kulazimishwa na mtu yeyote, nimefanya hivi kwa mapenzi yangu ya dhati. Nawaomba wana CCM mnipokee,” amesema Kadoma.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na msemaji wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo, kuhusiana na kuhama chama kwa mgombea wao wa ubunge, Kadoma, akisema hawakuwa na taarifa lakini chama kinaheshimu uamuzi wake.
“Siasa inachukua watu, kama yeye (Kadoma) ameondoka, wengine watakuja, lakini yeye kama mgombea anafahamu utaratibu, alipaswa kuandika barua ila hajafanya hivyo. Hatuwezi kumuingilia kwenye uamuzi wake, tunauheshimu,” amesema Shangwe.
Kuhusu hasara ambayo imepata chama kufuatia uamuzi uliofikiwa na mgombea huyo, Shangwe amesema: “Hata asingekuwa mgombea ubunge, kuondoka kwake kama mwanachama ni hasara, lakini hatuna cha kufanya. Kama alivyoamua kuondoka CUF na kuja ACT-Wazalendo basi ndivyo ameamua kwenda chama kingine.”
Shangwe amesema taarifa walizonazo kumhusu Kadoma, alishaanza kufanya mikutano ya kampeni na hawafahamu kipi kimemsibu kiasi cha kumfanya apande kwenye jukwaa la CCM na kutangaza kuhamia chama hicho.
Akiomba ridhaa ya miaka mitano mingine ya kushika uongozi wa nchi, mgombea urais wa CCM, Samia ametoa ahadi tano kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara akiahidi kuzifanyia kazi atakapochaguliwa kuiongoza nchi Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Samia amesema kuwa, endapo atapata ridhaa na kushika hatamu ya uongozi, Serikali yake itahakikisha bei za mazao ya wakulima wa mkoa huo zinapanda, hasa kwa mazao wanayoyategemea zaidi kama korosho, mbaazi, ufuta na karanga.
Amesema mbolea na pembejeo za ruzuku zilizotolewa zimeongeza mazao yanayozalishwa mkoani humo.
Akitolea mfano zao la korosho lililokuwa likizalishwa kwa tani 15,000, sasa uzalishaji umefikia tani 24,000 ambazo zimeingiza Sh73 bilioni, na mbaazi kutoka tani 1,130 hadi tani 5,950 zilizoingiza Sh10.8 bilioni kwa wananchi.
Mazao mengine ni karanga, zao ambalo uzalishaji wake umepanda kutoka tani 26,100 hadi tani 33,170 zenye thamani ya Sh82.9 bilioni, na ufuta kutoka tani 1,580 hadi tani 11,800 zilizoingiza kwa wakulima Sh78.8 bilioni.
“Tukisikia kazi na utu tunasonga mbele, ndiyo hii. Tumeleta pembejeo na mbolea ya ruzuku kwa lengo la kukuza kilimo ili wakulima wapate fedha. Hapo tunakuwa tumejenga utu wao, tukijua kwamba fedha hizo watazitumia kupata maendeleo na watasomesha watoto wao,” amesema mgombea huyo.
Amesema mbali na mbolea na pembejeo, endapo atapata ridhaa ya kuongoza, Serikali yake itakamilisha mradi wa visima vya umwagiliaji vya Likokona na Masuguru ili kuruhusu wakulima kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji na waweze kulima mara mbili kwa mwaka.
Katika kilimo pia ameahidi kuendelea kutafuta masoko zaidi ili kulinda bei za mazao ambayo hutegemea soko la kimataifa.
“Tuko kwenye mazungumzo, imani yetu bei hazitashuka kama vile ambavyo wengi walifikiria. Pia hapa tutakwenda kuweka kongani za viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yetu badala ya kuuza malighafi, tuuze zao lililoongezwa thamani,” amesema.
Kwenye eneo la nishati, mgombea huyo amesema Mtwara utanufaika na mradi wa Gridi Imara unaogharimu Sh307 bilioni ambao unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Songea hadi Masasi.
Mradi huo utahusisha vituo viwili vya kupozea umeme, kimoja kikiwa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma na kingine kitakuwa Masasi mkoani Mtwara.
“Lengo la vituo hivi ni kuhakikisha Mtwara inapata umeme wakati wote bila kukatika au kupungua nguvu,” amesema Samia.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu, amesema endapo atapata ridhaa, Serikali yake itajenga madaraja na barabara zote zenye changamoto kwa kuzitengeneza kwa viwango mbalimbali vitakavyoruhusu kupitika mwaka mzima.
Mgombea huyo amegusia pia changamoto ya wanyamapori kuvamia makazi ya watu ambayo hutokea zaidi katika vijiji vilivyozungukwa na pori la akiba la Lukwila na Lumisule, akieleza kuwa jitihada za makusudi zitachukuliwa kuhakikisha wanyama hao wanabaki kwenye maeneo yao.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mtwara, Said Nyengedi amesema: “Nikuhakikishie wananchi hawa wataenda kukupa kura nyingi zitakazokuwezesha kupata ushindi wa kishindo. Mtwara tumeshikama kuhakikisha Oktoba 29 CCM inapata ushindi wa asilimia 100,” amesema Nyengedi.