Kampeni za uchaguzi zinahusisha njia nyingi zinazowafanya wananchi wahamasike kumchagua mgombea au chama fulani ambacho kitawafikia na kuwashawishi kwamba ndiyo kinastahili kuongoza Serikali.
Moja ya njia hizo ni mikutano ya hadhara ambayo vyama vya siasa vinakwenda moja kwa moja kwa wananchi na kuwaeleza kuhusu ilani za vyama vyao na kuahidi mambo ambayo wakipewa ridhaa watayafanya katika eneo husika.
Hata hivyo, njia nyingine ya kampeni ni kupitia mabango ambayo hubandikwa sehemu mbalimbali ambazo wananchi watayaona na kumjua mgombea na chama chake wanaotafuta kupigiwa kura kwenye uchaguzi.
Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 2025, Mwananchi limebaini kwamba mabango ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan yamejaa kila kona ya Jiji la Dar es Salaam na miji mingine.
Hata hivyo, Mwananchi limeshuhudia mabango machache ya wagombea wa vyama vingine vya upinzani yakiwa yamewekwa baadhi ya maeneo. Mabango hayo ni madogo na machache ukilinganisha na ya mgombea urais wa CCM.
Mwananchi limepita katika maeneo ya barabara za Mandela, Morogoro, Kilwa na maeneo ya mizunguko ya barabara (round about). Vilevile, kuna mabango madogo yanayobandikwa kwenye nguzo za taa za barabarani.
Vilevile, kuna mabango makubwa (billboards) katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama vile Gongo la Mboto, Tazara, Ubungo na Posta, hivyo kumpa fursa mgombea urais wa CCM kuonekana kwa umma kila kona.
Uchache wa mabango ya wagombea urais wa vyama vya upinzani, umeibua maswali huku viongozi na wagombea wenyewe wakitaja mambo matatu yanayowakwamisha ikiwa ni pamoja na hofu ya kung’olewa, ukata na wengine kudai kuzoeleka kwa utamaduni wa mabango.
Katika Jiji la Mwanza mabango ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yametalawa ikilinganishwa na vyama vingine.
Baadhi ya mabango yameonekana barabara ya Kenyatta mzunguko wa samaki ambapo display ya tangazo (TV) ikimuonesha mgombea udiwani wa Kata ya Butimba, Heri Emmanuel akiomba kura yake na ya Rais Samia ambapo picha zao za mjongeo zikicheza.
Pia, mabango mengine yapo katikati ya mji likiwamo eneo la mzunguko wa barabara ya Kenyatta, Makongoro na Nyerere jirani na ofisi za CCM Mwanza.
Mabango ya kawaida(A4) ya baadhi ya wagombea wa vyama vingine yanaonekana moja moja hasa kwenye nguzo za umeme, na kwenye kuta za watu.
Viongozi upinzani wafafanua
Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Abdallah anasema chama hicho kimekuwa kikijitahidi kuweka mabango lakini wanakwama kutokana na gharama kubwa za utengenezaji wake.
“Sio kama hatupendi na sisi tuwe na mabango ya kutosha mitaani, lakini changamoto kubwa inayotukabili ni ukata.
“Hatuna fedha, tunapambana kulingana na uwezo wetu, japo kubandika mabango ni bure lakini kutengeneza ni gharama, bei ya mita moja ya mraba ni Sh20,000,” anasema Husna ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho.
Anaongeza kuwa wanaruhusiwa kubandika bango la mgombea wao kokote, hata kwenye nyumba ya mtu kama mwenye nyumba atawapa ridhaa hiyo, lakini ukata unawakwamisha kutengeneza mabango mengi.
Mwenyekiti wa UMD, Mohamed Omari Shaame anasema suala la mabango ni wagombea wenyewe hawajataka, akidai kwao utamaduni huo umezoeleka, hivyo wameona hakuna haja ya kubandika mabango mitaani.
“Kuwa nayo mengi mtaani hiyo ni hamasa tu ya wagombea wenyewe, sisi hatujataka kuweka, kwani mabango ni utamaduni ambao tumeuzoea, hivyo wengine tumeona hakuna haja hiyo,” anasema.
Mwenyekiti wa United Peoples’ Democratic Party (UPDP), Twalib Kadege anasema hawana uwezo wa kubandika mabango nchi nzima japo yapo ambayo tayari wameyachapisha, wanachokisubiri ni Oktoba ndio waanze kuyabandika akidai kwa sasa wana hofu yatang’olewa.
“Tumetengeneza mabango mengi tu, makubwa na madogo. Tunahofia tukianza kubandika mapema yataondolewa yote, hata hivyo kuanzia Oktoba 15, tutaanza kuyabandika, kwani tayari tumeanza kusambaza mikoani kote,” anasema.
Mgombea urais wa National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Almas amesema tatizo lao lipo kwenye fedha kwani bado wanategemea wanachama kupata fedha na hawajakidhi sifa kupata ruzuku ya Serikali.
“Kwa mazingira hayo, nguvu yetu ni ndogo ukilinganisha na wenzetu ambao wana nguvu kubwa, akitokea mtu wa kutusaidia mabango angekuwa mtu mwema sana,” anasema mgombea huyo.
Anasema chama hicho kilitamani kufanya harambee ili kuchangisha fedha kuwasaidia kwenye kampeni zao, lakini walikwaa kisiki kutokana na wananchi wengi kuwa na hamasa ya kuchangia chama kimoja pekee.
Katibu Mkuu wa African Democratic Alliance (Ada-Tadea), Saleh Msumari anasema suala la vyama vya upinzani kukosa mabango kila pahala kila mara wamekuwa wakilia kuhusu kupatiwa ruzuku.
Akitolea mfano wa ugumu wanaopitia katika kupata fedha za kampeni, anasema ni ngumu kuwa na fedha kwa ajili ya kutengeneza mabango ambayo wakati mwingine hata machache wanayobandika yanaondolewa na watu wasiojulikana.
Kwa upande wake, mgombea urais Demokrasia Makini (Makini) Coaster Kibonde amesema ili mabango hayo yawepo hitaji kubwa ni fedha.
“Changamoto kubwa kwetu ni fedha, uwezo wa kuchapisha mabango hatuna, tungekuwa na fedha hakuna mtu ambaye hapendi kuwa na mabango mengi kwasababu hiyo ni sehemu ya kempeni,”amesema.
Akizungumzia umuhimu wa kusambaza mabango mengi katika mitaa mbalimbali, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Richard Mbunda anasema hiyo ni moja ya mbinuya kuwafikia wapiga kura.
“Kuna mbinu nyingi za kuwafikia wapiga kura, mgombea lazima azitumie, wapo wanaotumia vyombo vya habari, wengine mitandao ya kijamii, kutumia watu maarufu wenye ushawishi na mbinu nyinine.
“Njia nyingine ya kuwafikia wapigakura ni ya mabango, ambayo ni ya kiutamaduni, mfano katika jimbo fulani, ili wananchi wakufahamu, mgombea atatumia bango, hiyo ni kwenye ubunge, vivyo hivyo kwa nafasi nyingine.
Amesema, kutumia bango ni njia rahisi ya kuwafikia wapiga kura wa eneo hilo, na kwa tafsiri ya wapiga kura wengi, kama mgombea haujaweka bango, basi wengi watakuona kama haupo ‘serious’.
“Watu ambao mabango yao kipindi cha kampeni yanasmabaa kweli kwli wana nafasi nzuri ya kushinda, mfano 2015 kule Kawe Halima Mdee (alikuwa mgombea ubunge wa Chadema) mabango yake yalitapakaa kweli kweli mitaani, kushinda hata yamgombea wa chama tawala, alishinda,” anasema.
Anasema kama mgombea haujabandika mabango kwa tafsiri ya wapiga kura wengi unaonekana kama haupo serios.
Akifafanua wale wanaobandua mabango ya wagombea fulani na kubandika ya wagombea wao, amesema hio ni kesi ya jinai, japo kuna maeneo bado tabia hiyo inaendelea, jambo ambalo si sawa.
“Hata hivyo inapaswa mgombea kuwa na mabango mengi, ili aliyobadika yaking’olewa aweze kuweka mengine, jambo ambalo ni gharama na changamoto inakuja endapo mgombea hauna pesa kutosha ambazo kimsingi ni pesa za kampeni utaathirika na hilo,”.
CCM kimeweza kuweka mabango hayo na kuendelea na mikutano ya kampeni nchi nzima kwa kuwa Agosti 12, 2025, ndani ya saa 24, kilikusanya zaidi ya Sh86 bilioni katika harambee iliyoanzishwa ya kuchangia shughuli za kampeni za urais na ujenzi wa chama hicho.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh56.3 bilioni zililipwa papohapo, huku zaidi ya Sh30.2 bilioni zikiwa ni ahadi zinazotarajiwa kulipwa na wadau, makada na washabiki wa chama hicho kwa siku zijazo.
Usiku wa Agosti 12, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City ilikokuwa inafanyika harambee hiyo, saa 5:30 usiku, Dk Nchimbi alitangaza tayari zaidi ya Sh56.3 bilioni ziliingizwa kwenye akaunti iliyotajwa, huku zaidi ya Sh30.2 bilioni zikiahidiwa.
Hata hivyo, alisema harambee hiyo inaendelea hadi Oktoba 27, 2025 siku ya mwisho wa kampeni za uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.