NUSU fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), imeanza na moto huku timu zilizoshinda zikifanya hivyo kwa mbinde kutokana na ushindani uliopo ambao umeyanfanya mashindano hayo mwaka huu kuwa ya aina yake.
Tofauti na miaka michache ya karibuni iliyopita ambapo ligi hiyo haikuwa na ushindani mkali kutokana na kutokuwa na uwekezaji mkubwa katika masuala ya usajili, mwaka huu kuna mastaa wa maana tu wanaokipiga na hivyo ili timu ishinde inalazimika kufanya kazi ya ziada.
Majuzi, pointi 12 za zilizofungwa na Dar City dakika ya saba ya robo ya kwanza ndizo zilizochangia timu hiyo iishinde Stein Warriors kwa pointi 69-65 katika nusu fainali ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Donbosco uliopo Oysterbay.
Hata hivyo, ushindi wa timu hiyo haukupatikana kirahisi kutokana na ushindani mkubwa ulioonyeshwa na Stein Warriors, huku kukiwa na idadi kubwa ya mashabiki kana kwamba ilikuwa mechi ya fainali.
Wengi wa watazamaji waliofika uwanjani hapo waliamini Dar City haitapata upinzani mkubwa, lakini ilijikuta ikipambana kusaka ushindi kwa mbine ikiwatumia nyota wake mahiri kina Brian Mramba, Evance Davies, Jonas Mushi, Tryone Edward, Frank Luhamba na Mwinyipembe Jumbe.

Timu hizo zilitumia staili ya kushambulia kutokea pembeni ambapo wachezaji wa timu zote walikuwa wakipambana kusaka alama, ambapo mashambulizi hayo yalizaa matunda.
Kwa upande wake, Dar City iliyoongozwa na staa wa kimataifa wa Tanzania, Hasheem Thabeet katika nafasi ya ulinzi, aliisaidia kupora mipira mingi ya hatari inayofika upande wake na kuisukuma mbele.
Thabeet alisaidiana vizuri na wachezaji wengine kina Sharom Ikedigwe, Clinton Best, Jamel Marbuary, Amin Mkosa, Ally Faraji pamoja na Victor Mwoka kusukuma mashambulizi.
Nusu fainali ya pili itachezwa leo, Jumatano na endapo Dar City itashinda tena itatinga fainali kwa matokeo ya michezo 2-0. Nusu fainali hiyo inachezwa kwa mfumo wa kila timu kucheza michezo mitatu maarufu kama best of three off.

DB LIONESS VS JESHI STARS
Katika nusu fainali nyingine upande wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwa wanawake (WBDL), DB Lioness iliifunga Jeshi Stars kwa pointi 58-51 ukiwa ni ushindi uliotokana na tofauti ya alama saba.
Hata hivyo nusu fainali hiyo iliyochezwa Dobosco itaifanya Jeshi Stars ijute kupoteza mchezo baada ya wachezaji wake kushindwa kufunga pointi za wazi katika robo ya tatu na nne ya mchezo.
Wachezaji hao Witness Mapunda aliyeshindwa kufunga dakika ya pili, nne na sita pamoja na Anamary Cyprian ile ya saba, huku katika robo ya nne Bhoke Juma akishindwa kufunga katika dakika tano.
Katika mchezo huo, DB Lioness iliyoonyesha imejiandaa vizuri kutokana na kuimarisha kikosi kwa ingizo la wachezaji wawili wa kimataifa – Sokoudjou Mishelles aliyetokea Cameroon na Mkenya Christina Akinyi walishirikiana vizuri na mzawa anayecheza Malawi, Olyne Londo.
Katika mchezo huo Jeshi Stars iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 13-4 huku ile ya pili DB Lioness ikaongoza kwa pointi 18-11, 15-10, 21-17.
Timu hizo zitacheza nusu fainali ya pili leo na endapo Dar City itashinda itatinga fainali kwa matokeo ya michezo 2-0.

JKT STARS VS DB TRONCATTI
Wakati mechi za juu ushindi ukipatikana kwa mbinde, pointi 41 zilizofungwa na Jesca Ngisaise wa JKT Stars ziliiwezesha kuifumua DB Troncatti kwa pointi 75-48.
Huo ulikuwa ushindi wenye pointi nyingi katika mechi za nusu fainali zilizopigwa katika Uwanja wa Donbosco.
Kati ya pointi hizo Jesca alifunga katika eneo la mtupo mmoja wa ‘three pointi’ 15 na kuondoka na asisti nane akifuatiwa na Sara Budodi aliyefunga pointi 19. Kwa upande wa DB Troncatti alikuwa ni Nasra Bakari aliyefunga pointi 12 akifuatiwa na Irene Gerwin aliyetupia 11.
Katika mchezo huo kilichochangia DB Troncatti kuchezea kichapo kikubwa ni matumizi makubwa ya nguvu kubwa katika robo ya kwanza, ambapo kwa mujibu wa makocha na wachezaji wakongwe walidai baada ya robo ya kwanza wachezaji wa timu hiyo walionekana kuchoka.
DB Troncatti iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 13-10, ya pili JKT Stars ikaongoza kwa alama 27-13, ile ya tatu 21-8 na ya nne kwa 15-13. Katika mchezo huo Jesca na Sara ndio wachezaji pekee waliocheza robo nne bila ya kupumzika.