KONA YA MALOTO: Uchaguzi Mkuu 2025, harakati na ukumbusho muhimu

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anawania kurejea madarakani kwa muhula wa pili, hivi karibuni alitoa kauli, na kwa msisitizo alikumbusha kwamba yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Alisema, Oktoba 29, 2025, siku ya uchaguzi, amani, utulivu na usalama vitatawala, watu wajiandae kupiga kura bila wasiwasi.

Alisema: “Hakutakuwa na nywinywi wala nywinywinywi.” Kauli hiyo ya Rais Samia, inafuatia hamasa ya mitandaoni, kwamba Oktoba 29, watu wajitokeze kuzuia uchaguzi. Yupo mtu anasema Rais Samia alipaswa kunyamaza na kupuuza yenye kusemwa. Mwingine anakumbusha kwamba mzahamzaha guu huota tende.

Nchi ikielekea kwenye uchaguzi na uwepo wa hoja za mapambano ya “tutazuia uchaguzi” dhidi ya “hamna ubavu”, vema kukumbushana. Tanzania ndiyo ngome kuu ya wakimbizi eneo la Maziwa Makuu. Hadi sasa, kambi ya Nyarugusu ina wakimbizi 176,000, Nduta ina watu 78,000, na idadi kama hiyo inapatikana Mtendele. Kambi zote hizo zipo Kigoma.

Mwaka 2022, kiongozi mmoja wa kimataifa wa masuala ya wakimbizi, alilazimika kutema nyongo, alipozungumza na raia wa Burundi wanaoishi ukimbizini nchini Tanzania. Sitamtaja kiongozi huyo kwa sababu mkutano wake huo hakualika vyombo vya habari. Hata hivyo, hotuba yake niliiona. Ina ujumbe ambao unaifaa Tanzania nyakati za mashindano ya “tutakinukisha” dhidi ya “thubutu mkione cha mtema kuni.”

Sasa, Kiongozi huyo wa masuala ya wakimbizi, alifanya mkutano na raia wa Burundi wanaoishi kwenye Kambi ya Wakimbizi, Ndutu. Mkutano ambao Balozi wa Burundi nchini Tanzania alishiriki, vilevile mashirika yote yanayotoa huduma kwa wakimbizi, yalialikwa.

Kiongozi huyo alisema, anawasikitikia watoto wakimbizi kwa sababu wamejikuta katika maisha yasiyo na heshima wala utu ukimbizini kutokana na wazazi wao kuchagua maisha ya ukimbizi. Alisema, wazazi walichagua ukimbizi kwa kushawishiwa na mashirika yenye kuhudumia wakimbizi, ambayo kwao uwepo wa wakimbizi ni heshima na masilahi makubwa upande wao.

Aligusia vipengele 15, kimoja ambacho siwezi kukiacha ni kile ambacho aliwataka wazazi wajitafakari kwa namna wanavyoishi kwa kupanga mistari wa kuomba chakula pamoja na watoto. Alihoji watoto wanajifunza nini kwa wazazi wao ikiwa wote wanaishi kwa kuomba?

Naomba msingi wa hoja yote ujikite kwenye kauli kuwa wakimbizi wamechagua maisha ya ukimbizi kwa sababu ya kushawishiwa na mashirika ambayo kwao uwepo wa wakimbizi ndio kutathibitisha kwamba wapo kazini.

Sasa, tujadili ile kauli kwamba wazazi na watoto hupanga foleni kusubiri kupewa chakula. Wakati huohuo, tukumbuke kwamba makutano ya “tutakinukisha” na “jaribuni”, ni mgusano wa hasi na chanya, kwa hiyo moto lazima uwake. Nchi ikishapata moto, Tanzania itatengeneza wateja wa mashirika ya wakimbizi. Ni ukumbusho, wakati mivutano inaendelea na ushawishi wa mitandao, isisahaulike maisha yatakayofuata. Ukimbizi na taadhira zake.

Eneo la kupanga foleni ya chakula ni dogo. Kuna kukosekana faragha. Maradhi ya mlipuko na kuishi chini ya uangalizi muda wote. Ukimbizi ni zaidi ya jela. Busara ni silaha muhimu nyakati za mivutano ya kisiasa. Vinginevyo, majuto yatafuata kipindi ambacho nchi haikaliki. Hakuna atakayetamkwa shujaa katikati ya mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, damu ikimwagika, vifo vikitokea, maelfu wakiishi kwa manyanyaso, taadhira na dhiki ukimbizini.

Halafu twende Sudani Kusini. Ni vita ya ukabila baina ya jamii za Dinka na Nuer. Rais Salva Kiir ni kabila la Dinka. Makamu wa Rais, Riek Machar ni kutoka jamii ya Nuer. Zimepita nyakati, Machar haikuwezekana kuguswa, maana kabila zima la Nuer lingeingia vitani na nchi haikuweza kukalika. Sasa hivi, Machar yupo mahabusu na amepewa kesi ya uhaini. Hakuna maandamano.

Kama siku za nyuma Kiir hakuweza kuongoza nchi peke yake, ikabidi iundwe Serikali ya Umoja, nguvu za Nuer zimepotelea wapi? Hawampendi tena Machar? Wamekubali kutawaliwa kwa asilimia 100 na mahasimu wao jamii ya Dinka? Jeuri ya Kiir sasa hivi inatokea wapi, kiasi ambacho hawaogopi tena Nuer?

Ukweli ni kwamba maisha ya mapigano ya kila mara yanachosha. Inawezekana jamii ya Nuer ina maswali mengi hivi sasa. Wanapigania nini? Tangu nchi hiyo ilipojitenga na Sudan (Khartoum), wanasiasa ndiyo tabaka linalofurahia rasilimali za nchi. Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwa. Timu za Kiir na Nuer ndiyo zinanufaika. Mwananchi wa kawaida haoni nafuu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kuonya kuhusu Tanganyika na Zanzibar. Alisema, baada ya kuvunja Muungano, itagundulika bado kuna uhitaji wa kugawana. Alisema, Zanzibar ikijitenga, baadaye watabaini kwamba kuna Pemba na Ugunja. Visiwa vikigawanyika, Unguja wataelekeana Wazanzibari dhidi ya Wazanzibara.

Sudani Kusini baada ya kujitenga na Waarabu, wakabaini kumbe ndani yao kuna Dinka na Nuer. Mwalimu Nyerere alisema, ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu, ukishaila huachi. Uchaguzi Mkuu unavyobisha hodi, na hamasa za kuukamia uchaguzi dhidi ya kuulinda, inakumbushwa kuwa chochoko za machafuko ni sawa na kula nyama ya mtu. Zitaendelea na kuendelea ikiwa tu zitafanikiwa na matokeo kuonekana.

Nuer hawaandamani tena kwa sababu ya Machar. Hawaoni faida tena. Wameshazika ndugu zao wengi. Baada ya machafuko, hasa pale amani inapopatikana japo kidogo, wananchi wanageuka mashuhuda wa maisha ya wanasiasa yanavyobadilika kwa kasi, tena wakivimba kwa ufahari mkubwa kwa kodi wavuja jasho waliotoka kuuana.

Haya si maonyo ya mtoto akililia wembe mwache umkate, au tahadhari ya chondechonde amani ilindwe. Huu ni ukumbusho kwamba kila jambo lina matokeo yake. Kukinukisha dhidi ya Nywinywinywi, Tanzania haitakuwa ilivyo tena. Damu inapomwagika, akili hubadilika, chuki huwa kubwa. Roho ya ibilisi hustawi. Je, nani yupo tayari?