Macho na masikio ni Lindi leo, vijana wataja kero zao wasikimbilie Dar

Lindi. Leo macho na masikio ya wakazi wa Mkoa wa Lindi yameelekezwa Ruangwa na Mtama ambako mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara  akiinadi ilani ya chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Ziara hiyo ya mgombea urais inakuja ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni zake ambapo tayari amezunguka mikoa kadhaa akiahidi kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kusimamia uchumi jumuishi na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Kwa wakazi wa Lindi, ujio huu umeibua matarajio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwani mkoa huo kwa muda mrefu umekuwa ukikabiliwa na changamoto za miundombinu, ajira kwa vijana na uwekezaji mdogo katika sekta muhimu kama kilimo na uvuvi.

Wananchi wengi wa Lindi, hususan wakulima wa korosho, wametaja kilimo hicho kama eneo linalohitaji msukumo mpya kutoka kwa serikali.

Akizungumza na Mwananchi mkulima wa korosho wilayani Ruangwa, Rashid Ngalawa amesema bei za korosho na changamoto za masoko bado ni kikwazo, licha ya jitihada za serikali zilizopita za kuimarisha zao hilo linalotoa pato kubwa la fedha za kigeni.

“Tunatarajia kusikia ahadi mahususi kuhusu korosho. Wakulima tumekuwa tukihangaika na bei ndogo na wakati mwingine kuchelewa kulipwa. Tunataka mgombea urais atoe mwelekeo mpya wa kuhakikisha mkulima analipwa haki yake kwa wakati,” amesema Ngalawa.

Kwenye suala la ajira  wenyeji wa mkoa huo wanasema una idadi kubwa ya vijana waliomaliza shule na vyuo lakini wanakabiliwa na tatizo la ajira.

Kwa mujibu wa vijana waliozungumza na Mwananchi, matarajio yao ni kuona mikakati thabiti ya uwekezaji na miradi ya kiuchumi ambayo itawawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

“Hapa Lindi tuna vijana wengi wenye nguvu na elimu, lakini nafasi za ajira ni chache. Tunatarajia kusikia namna Serikali ya CCM itakavyotuletea viwanda vidogo na vikubwa ili tuweze kupata kazi na kutumia fursa zilizopo,” amesema Asha Salum, mkazi wa Ruangwa.

Kwa upande wake Jonathan Ungani amesema ukosefu wa ajira ni tatizo linalowafanya vijana wengi wa mkoa huo kukimbilia Dar es Salaam hivyo kushindwa kuundeleza mkoa wao.

“Kila siku mikoa yetu ya kusini inaonekana kuwa nyuma kimaendeleo, hatuwezi kupiga hatua kama wanaobaki ni wazee  peke yao. Vijana huku hawakai wanakimbilia Dar kutafuta maisha, hao ndiyo wangetarajiwa kuleta mabadiliko lakini wanakaaje hamna cha kufanya huku,” amesema Ungani.

Sekta ya uvuvi pia ni uti wa mgongo wa maisha  kwa  wananchi  wa mkoa huo hata  hivyo, wanasema bado wanakabiliwa na changamoto za vifaa duni, miundombinu ya bandari ndogo na soko la uhakika la mazao ya samaki.

“Tukiwezeshwa vizuri, uvuvi unaweza kuinua uchumi wa Lindi. Tunatarajia ahadi kuhusu mikopo ya zana bora na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia samaki ili tusipoteze kipato chetu,” amesema Hassan Mbwana.

Mbali na sekta za kiuchumi, wananchi wanatarajia mgombea huyo atazungumzia mikakati ya kuboresha huduma za jamii ikiwemo tatizo la maji safi, umeme, afya na elimu.

“Wengi wetu tunapata shida kubwa ya maji. Tunataka ahadi inayotekelezeka kuhusu visima na miradi ya maji vijijini. Bila maji, maendeleo hayawezi kufikiwa,” amesema Zainabu Mnali mkazi wa  Liwale.

Aidha, wananchi wameeleza matarajio ya kuona uwekezaji katika barabara za vijijini, ambazo mara nyingi hazipitiki hasa wakati wa mvua. Wanaamini barabara bora zitafungua fursa za kibiashara na kuongeza kipato.

Ujio wa mgombea urais wa CCM mkoani humo unatazamwa pia kama fursa ya kuimarisha mshikamano wa kisiasa na kuonesha kwamba chama kinatambua mchango wa mkoa wa Lindi katika historia ya Tanzania.

Mkoa huo umekuwa ukitajwa miongoni mwa ngome ya CCM kwa muda mrefu na mara nyingi umekuwa ukitoa kura za kutosha kuunga mkono wagombea wake.

Mchambuzi wa siasa Jumanne Ngwale amesema  safari ya mgombea huyo inatarajiwa kuongeza ari ya kampeni za chama hicho, huku wapinzani wake wakifuatilia kwa makini ahadi atakazozitoa.

“Lindi ni mkoa wenye historia kubwa ya ukombozi na uaminifu kwa CCM. Lakini hali ya maisha ya wananchi inahitaji majibu ya moja kwa moja. Mgombea anapaswa kusikika akizungumzia miradi ya maji, barabara na huduma bora za afya ili kuendelea kushikilia imani ya wapiga kura,” amesema Ngwale.