NIKWAMBIE MAMA: Wala rushwa katika sura ya hisani

Mtu wa Pwani anaweza kuuliza swali linalofanana na jibu: “Hapo pajani pajani?” Kama anayeulizwa ni wa kutoka bara anaweza kujibu: “Sasa kumbe ulifikiria pajani ni gotini?” Lakini kumbe anakuwa hajaelewa kabisa mwenzake anaulizia nini. Swali ni: “Hapo kwenye paja panakuja nini? Ni kama mtu aliyeona dalili ya kitu kisicho cha kawaida (labda kipele hivi) kwenye paja la mwenzake.

Kule Bara, nyanya ni tunda linalotumika kuungia mboga. Lakini Pwani neno hilo linamaanisha “bibi”. Huku ukisema bibi unamaanisha mke au mwanamke anayeishi na mume. Kwa kuwa sisi Waswahili tupo kati, tunayapokea yote ya Bara na Pwani katika wakati mmoja. Tena basi tulivyo na bahati, tumetohoa maneno mengi kwa wakoloni waliotutawala na wafanyabiashara waliowahi kupita hapa.

Neno moja linaweza kuwa na maana nyingi, na maneno mengi yanaweza kumaanisha kitu kimoja. Hapa nchini neno rushwa linaweza kutajwa kama hongo au mlungula. Lakini watoa na wala rushwa kwa kuyaogopa maneno hayo, wanayapendezesha kwa neno “zawadi”. Kiuhalisia zawadi ni kitu anachotunukiwa mtu baada ya kufanikiwa jambo. Kwa mfano apohitimu, anapooa au kuolewa, anapojaliwa kupata mtoto na kadhalika.

Hivyo rushwa na zawadi havitangamani. Mtu hapewi rushwa kama tunu, bali anapewa kwa nia ya kushawishiwa. Mtoaji huhitaji hisani ya mtu kwenye jambo lake, hivyo atatoa chochote kama ushawishi kwa yule anaowahonga. Kuna tahadhari ya Kiswahili isomekayo “akupaye kitu bila sababu, basi ana sababu”. Kama anahitaji kazi, madaraka, kura basi hiyo ndiyo sababu ya yeye kutoa zawadi hiyo.

Wanasiasa wametohoa neno “rushwa” kuwa “takrima” ili kuziba tofauti kubwa iliyopo baina ya rushwa na zawadi.

Takrima inaingia kama tafsida inayopunguza makali ya neno rushwa. Katika vipindi mbalimbali, neno hili limekuwa likitumika badala ya “rushwa”. Washiriki wa mlungula wamekuwa wakilitamka moja kwa moja na bila woga kwa vile limepunguzwa makali. Sawasawa na kusema msalani badala ya chooni.

Katika msimu huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025, baadhi ya wagombea au wapambe wao wameshuhudiwa wakiranda majimboni, vitongojini na mitaani kuonana na wananchi moja kwa moja. Hiyo si habari maana “Mtarazaki Hachoki”, lakini la zaidi ni kwamba kuonana huko kumeambatana na takrima. Wananchi hawakushangaa kwani wanalinganisha wakati walio nao, na namna wahisani wanavyojitambulisha kwa nembo zao wakapata majibu.

Ili kuepuka ibilisi, waliamua kutoa taarifa kupitia namba walizopewa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Lakini wamedai kuwa kila walipopiga namba hizo hazikupokelewa. Wananchi hao wakapata bahati ya kulalamika kwenye vyombo vya habari kuhusu jambo hilo. Kituo kimoja cha Televisheni kilienda mbali zaidi kwa kuwahoji maofisa wa Takukuru kuhusu kadhia hiyo.

Katika ufafanuzi wao, Takukuru walidai kuwa hawapaswi kutangaza kila hatua wanayopita.

Wanasema wakati mwingine wanalazimika kufanya uchunguzi wa taarifa wanazopokea kutoka kwa wananchi kimyakimya. Mimi nakubaliana nao kwa hili, lakini najiuliza mbona wanatangaza baadhi ya mambo yanayofanana na hili? Kwa mfano la Wajumbe wa UWT Geita, walionaswa wakigawana rushwa mara baada ya zoezi la kuwanadi wagombea Ubunge ndani ya CCM kukamilika.

Kwa kuwa hatua zilichukuliwa baada ya tukio hilo kusambaa kwa picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii, watu wanahisi kuna mchezo unaoendelea. Wanadhani kuwa baadhi ya taarifa hazitangazwi kwa maslahi binafsi.

Upande mmoja nakubaliana na Takukuru kuwa kelele nyingi huweza kumtorosha tetere mtini. Lakini sioni kama kelele hizo zinaweza kumrusha ndege aliye mkononi mwa mwindaji.

Kuna nyakati ambazo watu wamejitokeza hadharani na kutoa ushuhuda bila woga. Kati yao wamo waliofuatwa moja kwa moja, na wengine walionasa matukio yakifanyika.

Kwa mfano yule kiongozi aliyemtangaza wazi mtia nia aliyetaka kumhonga. Wananchi wote walisikia, na Takukuru pia waliusikia. Mategemeo ya wote ni Takukuru kuchukua maelezo kutoka kwa shuhuda, kushughulikia jambo hilo na kisha kutoa taarifa kwa umma.

Vita dhidi ya rushwa inapaswa iwe wazi kwa sababu kuu mbili: Kwanza mla rushwa akome, lakini pili ni kuwatisha wanyemelezi wa rushwa. Mwalimu Nyerere aliwahi kuutamkia umma jinsi rushwa ilivyowakera enzi zao wakiwa madarakani.

Alisema mtuhumiwa alipothibitika kuwa na hatia, alichapwa bakora siku ya kuingia gerezani. Na alipomaliza adhabu yake, alitunukiwa bakora zingine ili arudi nazo nyumbani.

Kwa mantiki hiyo sioni ulazima wa Takukuru kuficha taarifa za uchunguzi kwa kiasi hiki. Rushwa haitolewi na kupokelewa hadharani, hutafutiwa vibebeo vya kuificha. Utaona bodaboda na baiskeli zikipelekwa kusaidia wajumbe wa nyumba kumi, kumbe ndani yake zipo za kuhonga wananchi.

Ni vigumu kupata ushahidi wa moja kwa moja bila kuwashirikisha wananchi. Wao ndio wanaziona hatua zinazokanyaga jimboni mwao

Mara zote kama wewe si mfanyakazi wa hospitalini, ukikutwa pale na mtu anayekufahamu atakuuliza: “Kwa nini uko hapa?” Takukuru nao wazizingatie zawadi zinazotolewa wakati wa maandalizi ya uchaguzi.

Waende na swali la “Kwa nini zitolewe wakati huu?” Hivi unamchukuliaje mtu anayekuuliza njia wakati unahesabu vibunda vya pesa kutoka kwa Wakala? Hakika unaweza kumtia bonge la ngumi.