Yule kocha wa Yanga mambo yamemchachia

LICHA ya rekodi tamu aliyoiandika akiwa na Yanga kwa kuipa mataji matatu kwa mpigo, ikiwamo kuifumua Simba kwa mabao 2-0 katika pambano la Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 25 na kuwafanya vijana wa Jangwani kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, hali si shwari kwa kocha Miloud Hamdi.

Hamdi aliyeipa Yanga Kombe la Muungano 2025, ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuifunga Singida Black Stars kwa mabao 2-0, kwa sasa amekalia kuti kavu huko Misri baada ya Ismaily kuburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ikifunga bao moja tu katika mechi saba.


Ismaily ambayo jioni ya leo Jumatano itashuka tena uwanjani ikiwa ugenini kuvaana na ENPPI katika mechi ya nane ya ligi hiyo, ndani ya mechi saba zilizopita imevuna pointi nne tu baada ya kushinda moja na kutoka sare moja pia, huku ikipoteza mechi tano zikiwamo tatu mfululizo zilizopita.

Ukuta wa timu hiyo, umeruhusu mabao manane, jambo ambalo limeifanya timu hiyo kuwa kati ya zilizofungwa mabao mengi na yenyewe ikifunga moja ikiwa ndio timu yenye safu mbovu ya ushambuliaji. Ismaily pia imezidiwa pointi 13 na vinara Zamalek wanaoongoza msimamo kwa alama 17 baada ya mechi nane ikiwamo sare ya jana dhidi ya El Gouna. Zamalek ndio iliyokuwa timu ya mwisho kuifunga Ismaily katika mechi tatu zilizopiota ilizopoteza mfululizo ilipolala 2-0 ugenini.


Hamdi alijiunga na Ismaily Julai 3, 2025 mara baada ya kumaliza kazi akiwa na Yanga akiiongoza katika mechi 13 za Ligi Kuu ikishinda 12 na kutoka sare moja na kubeba taji, huku kwa mechi za FA aliiongoza tano na kushinda zote ikiwamo fainali iliyowapa ubingwa dhidi ya Singida BS, ukiacha mechi tatu za Kombe la Muungano 2005 ikishinda zote na kubebea ubingwa kwa kuifunga JKU.

Hata hivyo, kocha huyo alinukuliwa hivi karibuni katika mahojiano maalumu, akieleza kufanya vibaya kwa timu hiyo anayoinoa kwa sasa kumetokana na kutumikia adhabu ya kutosajili kutoka FIFA, hali inayomlazimu kutumia wachezaji vijana na wale aliowakuta, ikisubiri dirisha lijalo kujinusuru.

Mapema mwezi uliopita Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo chini ya Nasr Abu Al-Hassan, ilinukuliwa na mtandao wa Kooora kuwa walikuwa wanapambana kumaliza mtataziko huo ikiwamo kukopa hata fedha za kulipa wachezaji walioenda kuwashitaki FIFA.


Lengo la kumalizana na tatizo hilo ni kuruhusiwa kusajili kupitia dirisha la Januari, ili kumrahisishia kazi kocha Hamdi aliyetua siku chache kabla ya adhabu hiyo kutolewa na kumkwamisha kushusha majembe mapya katika kikosi hicho kilichomaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 14 na kushindwa kuingia raundi ya ubingwa iliyoshirikisha timu tisa ambapo Al Ahly ilibeba taji.