RC CHALAMILA "MARUFUKU MABAUNSA KUTUMIKA KUTOA WATU MAENEO YENYE MIGOGORO DSM"

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameyasema hayo Kufuatia ukiukwaji wa sheria na vitendo vya ukatili vilivyofanywa na Mabaunsa dhidi ya wapangaji wa Bi Alice Paskali Haule kwenye nyumba yenye mgogoro iliyopo Msasani Beach jijini Dar es Salaam ambapo ameagiza kuanzia sasa mabaunsa wasitumike kutoa watu kwenye maeneo yenye migogoro badala yake madalali wa mahakama watumie jeshi la polisi ambao wanaweledi wa kufanya kazi hiyo

Mgogoro wa nyumba hiyo ambayo ni kiwanja namba 891 unahusisha mke wa marehemu Justis Lugaibula Bi.Alice Paskali Haule na bwana Muhamed Mustafa Yusufali ambae anaonekana alinunua nyumba hiyo kutoka kwa marehemu Justis Lugaibula enzi za uhai wake bila kumshirikisha mkewe

Akizungumza jijini Dar es salaam RC Chalamila ametoa agizo hilo leo septemba 24 alipofika katika nyumba hiyo msasani beach jijini humo baada ya jana septemba 23 kuona video zikionesha mabaunsa wakitumia nguvu kubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kuwaondosha watu waishio kwenye nyumba hiyo yenye mgogoro

Aidha Chalamila ameagiza nyumba hiyo kutotumika na upande wowote wa mgogoro hadi hapo mgogoro utakapomalizika ambapo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya kinondoni kuuunda kamati ya wataalamu ikiwemo jeshi la polisi, ofisi ya kamishina wa ardhi na wataalamu wengine ambapo ameitaka kamati hiyo na pande zote mbili za mgogoro kufika ofisini kwake ijumaa Septemba 26

Hata hivyo akizungumzia mgogoro huo bi Alice Pascal Haule ambaye ni mke wa marehemu Justis Lugaibula amesema yeye na mumewe walinunua nyumba hiyo mwaka 2008 lakini amekuwa akipata usumbufu kutoka mabaunsa wakidai kuwa Muhamed Mustafa Yusufali aliuziwa nyumba hiyo na mumewe wakati yeye anafahamu walikopeshana pesa na sio kuuziwa nyumba

Naye mwakilishi wa Muhamed Mustafa Yusufali ambae yupo safarini Bi Hajja Mungula amesema yeye anafahamu kuwa Muhamed alinunua nyumba hiyo mwaka 2011 kutoka kwa Marehemu Justis Lugaibula ambaye ni mume wa Alice kwa shilingi milioni 262 na kwamba Alice aliweka alama yake ya dole gumba kwenye nyaraka ya mauziano

Kwa upande wa Kamishina msaidizi wa ardhi Mkoa wa Dar es salaam Bw Shukrani Kyando ameeleza namna ambavyo nyaraka za nyumba hiyo zilivyokuwa zikibadilishwa kila inapouzwa na kusema kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo sasa nyumba hiyo aliuziwa Muhamed Mutafa Yusufali na hivyo hati inasoma jina lake huku mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Saad Mtambule akisisitiza changamoto ya uwepo wa mabaunsa wasio na weledi wa kazi katika wilaya hiyo.