Lilongwe. Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, amekubali kushindwa katika uchaguzi mkuu wa rais dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Peter Mutharika, na ameahidi kukabidhi madaraka kwa amani.
Katika hotuba yake kwa taifa mapema leo, Septemba 24, 2025, Chakwera amesema kulikuwa na ‘dosari’ na ‘hitilafu’ katika kuhesabu kura, lakini si kwa kiwango cha kuathiri ushindi wa Mutharika.
“Hitilafu hizo hazimaanishi kwamba matokeo ya uchaguzi yanayomwelekeza Profesa Mutharika kuwa mshindi si halali au hayawakilishi matakwa ya wananchi,” amesema.
Chakwera amesema kuwa bado anaitaka Tume ya Uchaguzi kutoa ‘taarifa kamili na ya uwazi’ kuhusu dosari hizo.
Chakwera amefikia uamuzi huo baada ya mpinzani wake wa karibu, Peter Mutharika, kuongoza kwa asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa, huku mshindi akitakiwa kupata kura zaidi ya asilimia 50.
Matokeo hayo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) yameonesha Rais aliyeko madarakani, Lazarus Chakwera, amepata asilimia 24 pekee ya kura katika uchaguzi huo uliokuwa na wagombea urais 17.
Ushindi wa Mutharika (85) unakuja kufuatia uchaguzi mkuu wa Malawi uliofanyika Septemba 16, 2025. Chakwera anamaliza kipindi chake cha kwanza na cha pekee madarakani, sawa na Mutharika ambaye naye aliwahi kuongoza kwa muhula mmoja kabla ya kushindwa na Chakwera mwaka 2020.
Chakwera, ambaye ni mchungaji wa zamani, alichukua madaraka katika uchaguzi wa mwaka 2020 alipoibuka mshindi dhidi ya Rais wa wakati huo, Mutharika, mtaalamu wa sheria za kikatiba kutoka chama cha Democratic Progressive Party (DPP).
“Dakika chache zilizopita, nilimpigia simu Profesa Mutharika na kumtakia kila la heri,” amesema Chakwera, saa chache kabla ya kutangaza kukubali matokeo.
Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo, “ilikuwa wazi kuwa mpinzani wangu, Peter Mutharika, ana uongozi mkubwa usioweza kufikiwa dhidi yangu,” amesema Chakwera (70) kutoka chama cha Malawi Congress Party (MCP).
Ushindi wa Mutharika unakuja ambapo pia zaidi ya nusu ya wabunge, wakiwamo mawaziri 14, wameshindwa katika uchaguzi huo.
Zaidi ya wabunge 110 kati ya 193 wa muhula wa mwaka 2019–2025 wamepoteza viti vyao, wakiwemo mawaziri 14 wa zamani.
Mutharika alifanya kampeni zenye hotuba fupi huku akizungumza kwa kurudia maneno.
Akizungumza na wapigakura kwa lugha ya Kichewa, mara kwa mara alirudia maneno mawili: “Mlinikosa, si ndiyo?” na “Mmeumia, si ndiyo?”
Ujumbe huo uliwagusa wapigakura wengi ambao, chini ya uongozi wa Chakwera, walishuhudia hali ya uchumi ikidorora, huku gharama ya maisha ikizidi kupanda na bei za vyakula zikiongezeka kwa kasi.
Hoja za hali mbaya ya uchumi ndizo zilizotawala kampeni na uchaguzi katika nchi hiyo, huku wakosoaji wakimlaumu Chakwera kwa kushindwa kusimamia vyema uchumi, kutokuwa na maamuzi ya haraka, na pia kushindwa kupambana na rushwa na kutekeleza ahadi zake za kuunda ajira.
Katika kipindi chake cha uongozi, gharama za maisha ziliongezeka katika taifa linalotegemea kilimo na lenye wakazi wengi vijijini, huku mfumuko wa bei ukifikia asilimia 33 na bei ya chakula kikuu, mahindi, pamoja na mbolea ikipanda kwa kiwango kikubwa, jambo lililokuwa ajenda kuu wakati wa kampeni za uchaguzi.
Pia, kulikuwapo na upungufu wa mafuta, kukatika kwa umeme mara kwa mara, na kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.