Samia aomba kura Ruangwa akimtaja Majaliwa bado yupo

Ruangwa. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kumtumia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kama msaidizi muhimu kwenye Serikali yake pindi atakapochaguliwa kuwa madarakani.

Majaliwa ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 na kushika nafasi ya Waziri Mkuu kwa miaka 10, Julai 2, 2025 alitangaza kutogombea jimbo hilo kwa kile alichoeleza kutoa fursa kwa wana- Ruangwa wengine.

“Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa wana-Ruangwa wengine,  wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili kaulimbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo iweze kusonga mbele zaidi,” alisema Majaliwa alipotangaza kutogembea ubunge.

Uamuzi huo uliibua mijadala kutoka kwa wadau mbalimbali wa siasa kwa kile kilichotafsiriwa kwamba, mwanasiasa huyo nguli ameamua kujiweka kando na siasa.


Hata hivyo leo Septemba 25,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ruangwa Mjini, Samia amewaahidi wananchi kuwa ataendelea kumtumia Majaliwa kama msaidizi wake.

“Haikutakiwa nianzie ila nilisema nije Lindi na nianzie kwa mdogo wangu Majaliwa, nimefurahi kufika hapa nyumbani kwa mdogo wangu na kupata mapokezi makubwa namna hii,” amesema.

Samia ameeleza kuwa, kazi nzuri inayosifiwa kufanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 10 ni matokeo ya usimamizi mahiri wa Majaliwa serikalini.

“Ninamshukuru kwa ushirikiano wake, kujituma na uzalendo wake wa hali ya juu wakati tunafanya kazi pamoja. Ahadi yangu kwenu Katika kuutambua na kuuthamini mchango wake, ataendelea kuwa msaidizi muhimu na makini katika Serikali licha ya kuanza nafasi ya ubunge na uwaziri mkuu,” amesema Samia.

Mgombea huyo amewaeleza wana Ruangwa kuwa, endapo atapa ridhaa ya kuongoza nchi, Serikali yake itaendelea kuzifanyia kazi  sekta zote za maendeleo kwa kile alichoeleza kwenye wilaya hiyo bado kuna maeneo ya kipaumbele yanayohitaji kufanyiwa kazi.

“Bado tunakuja kujenga vituo vya afya, zahanati, shule za msingi na sekondari na kukamilisha miradi ya maji ili kila mwana Ruangwa apate majisafi na salama,”amesema Samia.


Kuhusu tatizo la uvamizi wa wanyama pori  linalovikabili baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo, amesema linakwenda kufanyiwa kazi kuhakikisha hawaharibu mashamba na kuhatarisha maisha ya binadamu.

“Nafahamu kuna tatizo la wanyama waharibifu kuingia kwenye mashamba, hilo tunalielewa vyema. Na kama mnaweza kuwaambia hao wanyama basi waambieni dawa yao inakuja. Tunawapenda wanyama, lakini lazima tuhakikishe hawaharibu mashamba na kuhatarisha maisha ya binadamu,” amesema.

Katika kilimo, mgombea huyo ameahidi Serikali yake kuendelea kuwashika mkono wakulima kwa kutoa pembejeo na mbolea ya ruzuku sambamba na kutafuta masoko na bei kubwa za mazao.

Majaliwa aibua shangwe Ruangwa

Mbunge mstaafu wa jimbo hilo, Majaliwa ni miongoni mwa viongozi walioibua shangwe kwenye mkutano huo.


Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amesema mara kadhaa amekuwa akitumwa na wana Ruangwa kwamba, hakuna sababu ya mgombea urais kwenda kuomba kura kwenye jimbo hilo.

“Licha ya kwamba nilikufikishia ujumbe huo lakini leo umeamua kurudi tena Ruangwa, haya ni mapenzi makubwa. Tunayo sababu ya kukuhakikishia Oktoba 29 tunapiga kura zote kwa wagombea wa CCM.

“Wilaya hii ilikuwa changa sana, maboresho makubwa yamefanyika katika kipindi ulichoingia madarakani. Ruangwa hii iliyokuwa na changamoto mbalimbali lakini sasa zimepungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Majaliwa.

“Tunaamini kati ya wagombea wote waliojitokeza kugombea urais ni wewe pekee ndiye unaweza kuifanya Ruangwa iendelee, tuna kila sababu ya kukupa ridhaa ili ukamilishe kazi ambayo umeianza.”

Hoja ya kutokuwa na haja kwa Samia kwenda mkoani  humo kuomba kura imesisitizwa pia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi,  Hassan Jarufu ambaye ameeleza mgombea huyo hakuwa na sababu kwenda kutafuta kura Lindi kutokana na maendeleo aliyoyafanya kwenye mkoa huo.

“Wananchi wa Lindi wako pamoja na wewe Samia, ifikapo Oktoba 29 kura zote zitaelekezwa kwa wagombea wa CCM,” amesema Jarufu.

Hata hivyo, alipopanda jukwaani, Samia alijibu kuhusu hoja hiyo akieleza kwa mtu anayetaka jambo, uungwana ni kuomba.

“Mwaka 2023 nilipokuja kufanya ziara ya kikazi nikapita hapa Ruangwa, Waziri Mkuu aliniambia nisije huku kuomba kura mambo yote safi, lakini ndugu zangu uungwana unapotaka jambo ni lazima uende mbele yao wakuone, upige goti uombe kwa heshima na taadhima na ndiyo maana nimekuja,”amesema Samia.

Wabunge wasifu yaliyofanyika

Akizungumza kwenye mkutano huo mgombea ubunge wa  Ruangwa, Casper Mmuya amesema mahitaji ya wananchi wa jimbo hilo yameangaliwa kwa maono makubwa.

“Hatukuwa na lami,  lakini sasa tumepata lami ukiamua kutembea kwenye vumbi ni wewe, tuna taa zinazotuwezesha kutembea usiku bila wasiwasi wowote. Tumeunganishwa na wilaya nyingine kwa lami, tunaweza kufanya shughuli za ujasiriamali,” amesema Mmuya.

Mgombea ubunge wa viti maalumu, Zainab Kawawa amesema wanawake wa Mkoa wa Lindi bila kujali tofauti zao za kiitikadi, ajenda yao ni kuuheshimisha uongozi wa mwanamke, hivyo Oktoba 29 hawatafanya makosa.

Naye mgombea ubunge wa Nachingwea, Fadhili Liwaka amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Samia ameweza kuendesha nchi na kuhakikisha kila eneo linafikiwa na huduma zote muhimu.