Gamondi ataka miezi sita tu Singida BS

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema ushindi dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara sio wa bahati mbaya, huku akiweka wazi ubora wa wachezaji alionao ndio siri ya mafanikio licha ya kukaa pamoja kwa muda mfupi, akisisitiza anataka apewe miezi sita tu.

Gamondi amefunguka hayo baada ya Singida kuifunga KMC kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya ligi tangu amejiunga na timu hiyo aliyoipa mapema Kombe la Kagame 2025, sambamba na kushinda pia 1-0 katika pambano la kwanza la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema timu hiyo inacheza vizuri na inapata matokeo licha ya kutoa nafasi kwa kila mchezaji ili kutengeneza usawa kwa timu kujijenga na kutoa nafasi kwa kila mchezaji.

“Wachezaji wangu wanacheza vizuri, licha ya kutokaa nao pamoja kwa muda mrefu kutokana na baadhi yao kuchelewa kujiunga na timu, nafurahishwa na uchezaji wao wana uwezo wa kutengeneza nafasi na kuzitumia pia wanatawala mchezo,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Ukiangalia timu ina mabadiliko makubwa tofauti na kikosi kilichocheza mchezo wa kimataifa hii inanipa picha nzuri ni namna gani natakiwa kuandaa timu ya ushindani kuanzia ndani ya timu hadi kwa wapinzani.”

Licha ya kuweka wazi timu hiyo inacheza vizuri, Gamondi alisema anahitaji miezi sita ili kujenga kikosi bora kitakachompa mataji ya ndani na kimataifa kwa kuwa na muendelezo wa ubora.

Nahodha wa timu hiyo, Khalid Aucho baada ya kuibuka mchezaji bora wa mchezo akikabidhiwa tuzo alisema anamshukuru Mungu kwa kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne aliyocheza Ligi Kuu Bara.

“Asanteni sana hatimaye nimepata tuzo yangu ya kwanza baada ya miaka minne,” alisema Aucho. ambaye misimu minne yote ameitumikia Yanga akiipa mataji hakuwahi kutwaa tuzo hata mmoja akicheza mechi moja tu ya ligi ametwaa tuzo hiyo.