WAKATI kesho Septemba 25, 2025 Fountain Gate usiku ikitarajiwa kuwa mgeni wa Simba katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, timu hiyo ina takribani siku 90 za mateso.
Fountain Gate ambayo mechi ya kwanza ya ligi ilipasuka nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, ina wachezaji 14 pekee walioingizwa kwenye mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS) ambao ndio wanaruhusiwa kutumika.
Kwa mujibu wa Fountain Gate, licha ya taratibu zote za usajili kukamilika kwa wachezaji wake wapya, lakini mfumo huo ulipata tatizo na kusababisha hali hiyo.
Kwa sasa mabosi wa Fountain Gate, wanapambana kuona tatizo hilo linapata ufumbuzi katika mamlaka husika, lakini kama mambo yakiwa magumu, ni wazi timu hiyo italazimika kusubiri hadi Desemba 16, 2025 wakati usajili wa dirisha dogo utakapofunguliwa, hivyo itakuwa na kipindi cha siku 90 cha kucheza ligi na wachezaji 14 kuanzia Septemba 18, 2025 ilipocheza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Mbeya City.
Hali hiyo imejirudia tena kwa Fountain Gate kama ilivyokifanya msimu uliopita ilipoanza msimu bila ya kuwa na wachezaji muhimu iliyowasajili kutokana na kuchelewa kukamilisha taratibu.
Msimu uliopita ilishindwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Namungo ugenini, lakini ikajikuta ikikumbana na Simba katika raundi ya pili na kupasuka mabao 4-0 bila ya baadhi ya mastaa na kuchangia timu hiyo kunusurika kushuka daraja kupitia mechi za play-off. Hata hivyo, tatizo hilo lilishughulikiwa haraka kabla ya kucheza mechi zaidi ya tatu, wakaendelea kuwatumia nyota wake wapya.
Kinachoendelea sasa kilitokea msimu uliopita, hivyo ni marudio hii ni kutokana na changamoto ya kufungiwa kusajili na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kutokana na madai ya malimbikizo ya madeni kwa wachezaji ambao wameachana na timu hiyo.
Licha ya kuelezwa kuwa timu hiyo imekamilisha malipo waliyokuwa wanadaiwa, inaelezwa kuwa walichelewa mfumo wa usajili na kujikuta wakisajili nyota 14 pekee ambao waliipambania timu hiyo msimu uliopita huku lundo la nyota wengine wapya likiendelea kushuhudia mechi jukwaani.
Katika siku hizo 90 hadi kufikia usajili wa dirisha dogo, Fountain Gate itakuwa imecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara kwa mujibu wa ratiba dhidi ya Mbeya City (Septemba 17), Simba (Septemba 25), Mtibwa Sugar (Septemba 28), Dodoma Jiji (Oktoba 17), Coastal Union (Oktoba 22), KMC (Oktoba 25), Pamba Jiji (Novemba 23), Tanzania Prisons (Novemba 26), JKT Tanzania (Novemba 29) na Tabora United (Desemba 2).
Fountain Gate baada ya kukumbana na changamoto hiyo, imeiangukia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuomba mechi zake zijazo zisogezwe mbele ikiwemo ya Septemba 25, mwaka huu dhidi ya Simba hadi pale itakaposhughulikia ishu hiyo.
Kabla ya hilo halijatokea, Septemba 7, 2025, siku ambayo dirisha la usajili lilikuwa linafungwa, Mmiliki wa Fountain Gate FC, Japhet Makau alinukuliwa akisema: “Tumefanya usajili mkubwa na tunaamini wachezaji wetu walioko kwenye timu na sehemu ya wachezaji hao tumewachukua City FC Abuja ambao walikuwa wachezaji muhimu kwao. Sasa kama unachukua wachezaji muhimu wa timu na kuwaweka kwetu maana yake ni kwamba naamini tunakwenda kupata matokeo mazuri.
“Usajili unafungwa leo (Septemba 7, 2025) si ndio, tusubiri kesho (Septemba 8, 2025) tuone kama hatujasajili, mpaka sasa mfumo upo wazi mpaka saa sita usiku leo.
“Tulikuwa na changamoto kidogo hapo mwanzo lakini tumeshakamilisha, naamini kabla ya dirisha kufungwa tutakuwa tumekamilisha kila kitu. Baada ya hapo tutafanya utaratibu wa kutangaza wachezaji wetu ili watu waweze kuwajua.”
Wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likitangaza Julai Mosi, 2025 limefungua dirisha la usajili kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu Wanawake, lilibainisha tamati yake itakuwa Septemba 7, 2025, hivyo hakutakuwa na muda wa ziada.
Zoezi hilo likiwa linaendelea, Fountain Gate ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikipambana kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu huu wa 2025-2026. Katika hilo, ikashusha nyota takribani kumi kutoka Nigeria kwenye timu ya City FC Abuja kwa ajili ya kuwajaribu kabla ya kuwasajili.
Katika majaribio hayo, taarifa kutoka ndani ya Fountain Gate zilibainisha kwamba wachezaji saba walikidhi vigezo na kuwekwa kwenye mikakati ya kusajiliwa, lakini hadi dirisha linafungwa, haikuwa hivyo.
Sababu ya kushindwa kusajiliwa wachezaji hao mapema ni kutokana na Fountain Gate kufungiwa na FIFA mpaka pale itakapokamilisha malipo ya madai ya waliokuwa wachezaji wao, jambo ambalo lilikuwa kupatiwa ufumbuzi siku mbili kabla ya dirisha kufungwa.
“Tumefunguliwa usajili Septemba 5, kwa hiyo siku mbili zikawa bize sana kwetu kukamilisha majina kuweka kwenye mfumo, baadaye kukatokea tatizo ingawa taratibu zote zilikuwa tumezikamilisha.
“Muda wa kufungwa usajili ulipofika tulikuwa bado tunahangaikia suala hilo, tukawajulisha wahusika kuhusiana na tatizo tulilokutana nalo, tunasubiri majibu kutoka kwao,” alisema mmoja wa viongozi kutoka ndani ya Fountain Gate.
Hii si mara kwanza, msimu uliopita Agosti 17, 2024, Fountain Gate ilitarajiwa kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara ugenini dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi, lakini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikatangaza kuuahirisha huku sababu zikiwa hazijawekwa wazi.
Licha ya kutowekwa wazi, Mwanaspoti linafahamu kwamba kuahirishwa kwa mchezo huo kulitokana na kundi kubwa la wachezaji wa Fountain Gate kutosajiliwa katika mfumo wa usajili wa TFF na FIFA.
Kutosajiliwa huko kumetokana na FIFA kutopata uthibitisho wa Fountain Gate kulipa malipo ya mmoja wa wachezaji wake wa zamani ambaye aliishtaki timu hiyo akidai fidia ya kuvunjiwa mkataba kiholela hapo nyuma.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Bara, huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Fountain Gate, kisha Agosti 25, 2024 ikaenda kucheza dhidi ya Simba na kufungwa mabao 4-0.
Msimu huu, mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Mbeya City uliochezwa Septemba 18, 2025, Fountain Gate ilipoteza kwa bao 1-0, huku ikiwa na wachezaji 14 pekee waliosajiliwa kwenye mfumo.
Baada ya mchezo huo, taarifa zikatoka kwamba wachezaji wanne kati ya hao wamepata majeraha, hivyo wamebaki kumi wakiwemo makipa wawili.
Kutokana na changamoto hiyo, uongozi wa Fountain Gate ukaiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuomba michezo yao inayofuata ikiwemo dhidi ya Simba kusogezwa mbele hadi watakapoweka sawa mambo yao.
Taarifa ya Fountain Gate iliyotolewa Septemba 20, 2025 na uongozi wa klabu hiyo, ilieleza: “Uongozi wa Fountain Gate FC unapenda kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto zilizojitokeza katika mchezo wetu wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, Septemba 18, 2025.
“Kikosi chetu kililazimika kushuka dimbani kikiwa na wachezaji wachache kutokana na tatizo la kiufundi katika mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS), licha ya taratibu zote za usajili kukamilika kwa wachezaji wetu wapya.
“Changamoto hii ilitokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa klabu na tayari juhudi za pamoja kati ya Fountain Gate FC na TFF zinaendelea kutafuta suluhisho la kudumu.
“Hali hii imeathiri maandalizi ya timu, kwani kwa sasa tuna idadi ndogo ya wachezaji waliothibitishwa kucheza, huku baadhi wakikabiliwa na changamoto za kiafya na majeraha. Kutokana na hali hiyo, tumeiandikia Bodi ya Ligi (TPLB) kuomba michezo yetu isogezwe mbele mpaka pale suluhisho na mwafaka wa changamoto hii utakapopatikana.
“Fountain Gate FC inatambua umuhimu wa ushindani wenye uwiano katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Tunaamini Kwa kushirikiana na TFF na TPLB tutaweza kupata mwafaka wa haraka, na kuruhusu timu yetu kushiriki ligi kwa kikosi kamili na chenye ushindani.Tunawaomba wadau wetu wote kuendelea kuwa na subira na kuipa timu yetu sapoti wakati huu wa mpito.”
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, alipotafutwa kuzungumzia suala la ombi la Fountain Gate kuhairishiwa mechi yao na Simba alisema hakuna mabadiliko yoyote.
“Hakuna mabadiliko yoyote mchezo kati ya Simba ambayo ndio timu mwenyeji dhidi ya Fountain Gate utachezwa leo (jana) kama ulivyopangwa.” alisema Boimanda.
Msimu uliopita Fountain ilipangwa kucheza na Namungo ugenini Agosti 17, lakini mechi iliahirishwa kwa sababu za wagenui kutokamilisha wachezaji kisha ikakutana na Simba Agosti 25, 2024 ikiwa na baadhi ya wachezaji na kupasuka kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Edwin Balua dk 13′, Steven Mukwala dk 44′, Jean Ahou dk 58′ na Valentino Mashaka 80′. Leo itakuwaje? Tusbiri dakika 90.