Unguja. Mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema atakapochaguliwa kuiongoza Zanzibar, Serikali yake haitatoa huduma kwa kuangalia itikadi za kisiasa.
Sambamba na hilo, amesisitiza kusimamia ardhi kuwa rasilimali inayomilikiwa na mwananchi badala ya Serikali na wananchi ndio watakaokuwa na mamlaka ya kuikodisha, huku Serikali ikipokea kodi na kutoa mwongozo unaosimamia.
Othman ameyasema hayo leo, Jumatano Septemba 24, 2025 katika mkutano wake wa kampeni za urais wa Zanzibar uliofanyika katika Uwanja wa Nyota Nyekundu Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Serikali yake haitatoa fursa na huduma kwa kuangalia itikadi za kisiasa za mwananchi husika, badala yake kila mtu atapata kila haki anayostahili kwa usawa.
“Serikali yangu haitatoa fursa na huduma kwa kuangalia itikadi za kisiasa za wananchi. Kila mwananchi ana haki ya kupenda chama chake, kwa hiyo hatutaangalia hilo,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema Serikali yake itaisimamia sheria ya ardhi kwa uadilifu kuhakikisha rasilimali hiyo inakuwa mali ya wananchi badala ya Serikali.
“Akitokea mtu anataka kuwekeza, Serikali tunakuja kukaa na wewe kukwambia ametokea mwekezaji anataka ardhi yenu, kama mpo watu sita au watano.
“Mnapewa mwongozo wa kukodisha Serikali inawasimamia mnakodisha baada ya kuitambua na kuisajili kwa kuwa ndilo jambo la kwanza tutakalofanya,” amesema Othman.
Amesema utaratibu huo, utamwezesha mwananchi mwenye ardhi kupanga bei ya ukodishaji chini ya mwongozo wa Serikali na yenyewe itapokea kodi.
“Tukifika hapo mtaufurahia uwekezaji, sisi tunapotaka kuwafikisha, mkisikia anakuja mwekezaji mseme Alhamdulillah, neema imekuja,” amesema.
Othman amesema watafanya hivyo kwa kuwa wanatambua ardhi ndiyo muhimili wa maisha ya binadamu, akiondolewa anabaki kuwa mtumwa kwa nchi yake.
Jambo lingine aliloahidi kuhusu ardhi, ni kuchunguza madai yote ya dhuluma za rasilimali hizo, ukweli ukibainika, waliodhulumiwa watarudishiwa maeneo yao.
Amesema atafanya hivyo ili kuifanya Zanzibar kuwa eneo ambalo wananchi wanaishi kwa amani na furaha kwa kuwa huo ndio msingi wa mapinduzi.
“Mapinduzi ni wananchi kufaidi matunda ya mapinduzi, hatutakubali tuyale tuyamalize. Sisi tutakwenda kukomesha hayo,” amesema.
Othman amesema Serikali yake itahakikisha ardhi yote ya kilimo inasimamiwa ili itumike na kuzalisha.
“Kwenye suala la kilimo mwekezaji wa kwanza ni mwananchi na kwamba masoko yatatumika kwa wananchi husika kuuza mazao yao,” amesema.
Kwa kufanya hivyo, amesema Mzanzibari atanufaika hata na soko la mazao la visiwani humo, badala ya watu kutoka nje kuuza ndani.
Ameahidi kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kwa pembejeo na ardhi ili kuwaepusha na njaa na umaskini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema vijana wanapaswa kujiuliza kuhusu thamani zao ili wafanye machaguo ya viongozi sahihi wa kuiongoza Zanzibar.
“Wewe kijana, huwezi ukaishi kwa kutegemea kugaiwagaiwa, leo utakuwa naye wa kukugaia, kesho na keshokutwa hayupo, msingi wa utu wa kujituma ukajisimamia,” amesema.
Ameeleza vijana wanapaswa kuchagua kiongozi anayeonyesha upendo kwao kwa kuhakikisha anawasomesha elimu ya kawaida au ya ufundi na kuwatafutia ajira.
“Mlimsikia mgombea wetu wa urais jana, alisema atasomesha vijana kuanzia awali hadi vyuo vikuu, ukishamaliza kusoma kaahidi atatengeneza mazingira ya vijana kupata ajira,” amesema.