Siha. Mgombea Urais kupitia Chama cha UDP, Saumu Rashidi ametangaza mambo matano ambayo anakwenda kushughulika nayo pindi atakapopata ridhaa ya wananchi ya kuwa kiongozi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Miongoni mwa mambo anayopigania mgombea huyo kipaumbele cha kwanza ni kilimo cha umwagiliaji, viwanda, afya, elimu pamoja na maji.
Saumu amesema leo Jumatano Septemba 24, 2025 katika viwanja vya Sanya Juu Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro katika mkutano wa hadhara wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo.
Amesema pamoja na vipaumbele vyao wameangalia maeneo mengine katika maisha ya kila siku ikiwamo ya kilimo ili kupata chakula.
Saumu amesema kama unavyofahamu kilimo ni uti wa mgongo wa wa Watanzania wote, mikoa yote waliyopita na wanayokwenda kupita kabla yakuitimisha kampeni hakuna mkoa ambao haujihusishi na kilimo, hiyo ni kuonyesha kwamba kilimo ni uti wa mgongo.
Kutokana na hilo ndiyo sababu tukasema tunataka kuwekeza kwenye kilimo ili kupata mazao kwa ajili ya chakula na biashara.
Amesema kwa sababu sasa hivi kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, mvua zimekuwa ni chache, wamepanga kuhakikisha maji yanakuwepo kwa kuchimba visima na mabwawa ili kuwa na maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo hicho.
“Sisi tupo pamoja na wakulima kwa kuweka mazingira rafiki na lengo kubwa ni kufungua kurasa za ajira kwa vijana wengi wakatakaokwenda kushughulika na kilimo, kwani kutokana na mvua kunyesha chini ya kiwango wanaona kilimo kama ni changamoto kwa sababu hawajawekwe mazingira wakione kilimo kama frusa,” amesema Saumu.
Mbali na kilimo pia amesema ataboresha elimu atahakikisha barabara zinapitika na huduma zinakuwa bora katika hospitaliwa, sambamba na kuhakikisha majiko ya gesi yanakuwa na nafuu ili kila mtu awaeze kuyatumia ili kulinda misitu.
Kwa upande wake mgombea mwenza, Juma Faki amewataka wananchi kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo na kuwataka kutunza kadi za mpiga kura ili wabaki kuwa na sifa.