Eneo korofi la ‘Kwa Kichwa’ Zingiziwa lakumbukwa

Dar es Salaam. Eneo korofi maarufu ‘Kwa Kichwa’ lililopo Kata ya Zingiziwa, Mtaa wa Ngobedi, Wilaya ya Ilala, limeanza kutengenezwa baada ya muda mrefu kuwa kero kwa wakazi, hasa msimu wa mvua.

Kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa likijaa maji na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii, huku wakazi wakishindwa kuvuka na kulazimika kulipa kati ya Sh1,000 na Sh2,000 ili kubebwa mgongoni kuvushwa na vijana waliogeuza changamoto hiyo kuwa ajira, au kulipa hadi Sh5,000 kwa usafiri wa bodaboda kwa safari inayopaswa kulipa Sh1,000 nyakati za kiangazi.

Kwa sasa, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) umeongeza karavati la tatu ili kupunguza mkusanyiko wa maji baada ya yale mawili ya awali kuzidiwa na kusababisha maji kupita juu yake.


Akizungumzia hatua hiyo leo Jumatano Septemba 24, 2025 alipozungumza na Mwananchi, mkazi wa Zingiziwa, Ester Lymuya amesema ukarabati huo unatoa matumaini mapya kwa wakazi hao kwa kuwa awali hali ilikuwa ngumu sana. “Wanavyoboresha hivi inaleta matumaini kwamba hata sisi tunafikiriwa,” amesema mkazi huyo.

Tecla Peter naye amesema changamoto kubwa ilikuwa kwa wajawazito na akina mama wenye watoto wachanga waliokuwa wakihitaji huduma katika Kituo cha Afya Zingiziwa. “Kukarabatiwa kwa eneo hili si faida za kiuchumi pekee bali pia za kijamii,” amesema.

Kwa upande wake, Renatus Milanzi amesisitiza kuwa ukarabati pekee hautoshi bila barabara kuwekwa lami.

“Zingiziwa inakua kwa kasi, ina huduma zote muhimu za jamii na hata ofisi za Serikali. Ni lazima barabara iwe ya lami,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngobedi, Seif Chamwande akizungmzia hilo, amesema hatua ya kuanza kwa ujenzi huo imewapunguzia lawama kutoka kwa wananchi.

“Tulionekana kama hatufikishi changamoto hizi kwenye mamlaka, lakini sasa wananchi wanaelewa jitihada zetu,” amesema.

Meneja wa Tarura Ilala, John Magori amesema  barabara hiyo ipo kwenye mpango wa kuwekwa lami na eneo la Kwa Kichwa litatanuliwa na kuboreshwa zaidi.

“Changamoto imekuwa bajeti ndogo, lakini wananchi wawe na subira kwa kuwa mradi huu upo kwenye mipango yetu,” amesema.

Mbali na Kwa Kichwa, Tarura pia imeweka karavati eneo maarufu la Fatuma Gesi lenye chemchemi, ili kuruhusu maji kupita na kupunguza athari za mafuriko.