AZAM FC imeutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge.
Ibenge ambaye hii ni mara ya kwanza kufundisha timu ya Tanzania, ameshuhudia vijana wake wakimkaribisha vizuri kupitia mabao ya Nassro Saadun na Feisal Salum.

New Content Item (1)
Saadun alikuwa wa kwanza kucheka na nyavu alipofunga dakika ya 32 akimalizia shambulizi la kona lililoanzishwa na Feisal Salum na kumfikia Abdul Suleiman Sopu aliyetoa asisti ya bao hilo.
Kabla ya bao hilo, timu zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, lakini safu zao za ulinzi zilikaa imara kuzuia nyavu zisitikiswe.
Sekunde kadhaa baada ya ipindi cha pili kuanza, Fei Toto aliifungia Azam bao la pili akimalizia pasi ya Baraket Hmidi.

Mbeya City ambayo huu ulikuwa mchezo wa pili wa ligi baada ya kuanza na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Fountain Gate, ilionyesha mapambano lakini eneo la mwisho lilikosa utulivu.
Licha ya mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na Kocha aa Mbeya City, Malale Hamsini, kwa kuwatoa Habib Kyombo na Eliud Ambokile huku wakiingia Peter Mwalyanzi na Hamad Majimengi, lakini hakuna kilichobadilika kwenye ubao wa matangazo.
Azam nayo licha ya kuwa mbele kwa mabao 2-0, Ibenge alijaribu kufanya mabadiliko kwa kuongeza nguvu kikosi akiwatoa Saadun, Sadio Kanoute, Sopu na Baraket huku nafasi zao wakichukua Jephte Kitambala, James Akaminko, Muhsin Malima na Pape Doudou Diallo.
Nyota wa mchezo huo amechaguliwa kuwa Baraket Hmidi wa Azam aliyetengeneza bao la pili kwa timu hiyo.

Azam sasa inarudi uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali dhidi ya Al Merreikh FC Bentiu utakaochezwa Septemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Mchezo wa kwanza ugenini, Azam ilishinda mabao 2-0, hivyo inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote kufuzu hatua inayofuata.