Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu umeweka rekodi mpya kwa namna wanawake walivyojitokeza kuwania nafasi za juu za uongozi.
Historia hii mpya imeandikwa kutokana na ongezeko la wagombea wanawake wanaowania nafasi mbalimbali zikiwamo za urais sambamba na wagombea wenza.
Hatua hii inaonesha mafanikio ya mapambano ya usawa wa kijinsia, demokrasia na mustakabali wa Taifa.
Kwa upande wa urais, wapo wanawake watatu wanaosaka kura za kuomba ridha ya wananchi. Wa kwanza ni Samia Suluhu Hassan ambaye anaiomba nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Samia anaingia tena kwenye kinyang’anyiro akibeba rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke kuiongoza Tanzania kabla na baada ya kipata uhuru na sasa anatetea nafasi yake ya uongozi wa juu zaidi.
Mwingine ni Mwajuma Mirambo wa Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), ambaye kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kwenye jukwaa la siasa za urais, akiwakilisha sauti mpya za wanawake kutoka nje ya vyama vikubwa.
Wa tatu ni Saum Rashid wa Chama cha The United Democratic Party (UDP) akijaribu kuonesha kuwa, hata vyama vidogo vinaweza kutoa fursa kwa wanawake kusimama kuwania nafasi ya juu kabisa serikalini.
Hii ni hatua muhimu, kwa sababu mara nyingi historia ya siasa nchini imekuwa ikitawaliwa na majina ya wanaume pekee katika kinyang’anyiro cha kiti cha urais.
Lakini historia imeandikwa zaidi pale wagombea tisa wanawake waliposimamishwa kuwania nafasi ya mgombea mwenza wa kiti hicho cha urais kutoka vyama vinavyoshiriki uchaguzi mkuu huo.
Miongoni mwao ni Chumu Juma wa Chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), akiashiria kuibuka kwa sauti mpya za wanawake kutoka vyama vidogo.

Kutoka Chama cha Demokrasia Makini, amesimama Azza Suleiman, akisisitiza dhamira ya chama chake kuonesha wanawake wanaweza kushiriki kwenye nafasi za juu.
Chausiku Mohamed kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), naye amejitokeza akiwakilisha kundi la wanawake vijana katika siasa za kitaifa kuwa makamu wa Rais, huku Amana Mzee wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) akijipambanua kama chaguo la kuunganisha historia ya chama chake na hoja za usawa wa kijinsia akigombea nfasi hiyo.
Kutoka chama kikongwe cha upinzani, NCCR-Mageuzi, jina la Dk Evaline Munisi limeibuka likiwakilisha kundi la wasomi na wataalamu wanaojitosa kwenye siasa akigombea nafasi ya mgombea mwenza wa urais.

Vilevile UMD imemsimamisha Mashavu Haji kuwa mgombea mwenza wa urais, jambo linalofanya chama hicho kuendelea na mwendelezo wa kusimamisha wanawake kwenye nafasi kubwa kwa kuwa tayari pia kimeweka mgombea urais mwanamke.
Kwa upande wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), jina la mwanaharakati maarufu na mwandishi wa habari, Devotha Minja, limesimama nyuma ya Salum Mwalimu kuwa mgombea mwenza kwenye chama hicho katika mbio za kusaka urais wa Tanzania.

Chama cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha Husna Abdalla na orodha hiyo inakamilishwa kwa jina la Satia Bebwa kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU).
Majina haya 12 ya wagombea wanawake, watatu wa urais na mengine ya makamu wa Rais, yameandika ukurasa mpya katika historia ya siasa ya Tanzania.
Kwa mara ya kwanza, wanawake wapo kwenye ramani ya siasa katika nafasi ya juu kabisa wakionesha dhamira ya kupaza sauti zao kwenye uongozi ngazi ya juu kabisa.
Hii imewasukuma wanaharakati wanaopambania masuala ya jinsia na uongozi kuona kwa Tanzania, huu ni mwaka wanawake kisiasa.
Kwa mujibu wa wanaharakati hao, hata kama si wote wana nafasi kubwa ya kushinda, hatua ya kujitokeza yenyewe ni ujumbe kwa jamii kuwa, wanawake wako tayari kugombea nafasi tofauti na chaguzi zilizopita.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk Onesmo Kyauke akizungumza na Mwananchi juu ya hilo, anasema katika uchaguzi wa mwaka 2025 idadi kubwa ya wanawake kujitokeza kugombea nafasi za juu za kitaifa ikiwamo watatu wa urais na tisa wa makamu wa Rais ni ishara ya mabadiliko ya kisiasa na kijamii nchini.

Anasema hali hiyo ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za kupigania usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia sera na mikakati ya kitaifa, kikanda na kimataifa kama Mkataba wa Maputo, maazimio ya Mkutano wa Beijing na ajenda za nchi za Afrika Mashariki sambamba na za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Pia, anasema huo ni mwendelezo wa mfano uliooneshwa na viongozi wanawake waliowahi kushika nafasi kubwa serikalini, hususan urais wa Samia, umefungua milango ya imani kwa wanawake wengine kwamba, nafasi hizo ni halisi na zinaweza kufikiwa.
Anasema mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, yameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa, wengi wao wakiwa na elimu ya juu, uzoefu wa kitaaluma na mitandao ya kisiasa inayowawezesha kugombea.

Wananchi wakimsikiliza sera za chama Cha AAFP katika mkutano wa kampeni kisiwani Pemba
Aidha, mtaalamu huyo anasema wananchi hasa vijana wanaanza kuthamini zaidi uwezo na sera badala ya jinsia pekee, hali inayowaweka wanawake katika nafasi ya kuonekana kama wagombea halali na si kama wasaidizi.
“Lakini licha ya hatua hii kubwa iliyofikiwa, changamoto bado zipo. Wanawake nchini nado wanakabiliana na mitazamo ya kijadi yenye mfumo dume inayowakatisha tamaa na kuzuia wengi kushiriki,” anasema Dk Kyauke.
Pia, inaelezwa kuwa, nguvu ya vyama vikubwa na mitazamo ya wapigakura vinaweza kuathiri nafasi za wanawake wenye nia ya dhati. Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, mchambuzi wa siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Consolata Sulley anasema mitazamo hasi ya kijamii bado ni tatizo linalowakwamisha wanawake.
Anasema wanawake mara nyingi hutazamwa kama wasioweza kufanya mambo makubwa kama wanaume, hata pale wanapojitokeza kutaka kuomba nafasi za uongozi wa kisiasa, mara nyingine hukatishwa tamaa hata na wanawake wenzao.
“Hali hii huathiri mwitikio wa jamii dhidi ya wagombea wanawake na kupunguza nafasi zao katika ushindani wa kisiasa. Safari ya wanawake katika siasa nchini imekuwa ndefu na yenye changamoto nyingi,” anasema Dk Sulley.
“Kuanzia enzi za uhuru, walionekana kwa idadi ndogo bungeni, hadi uteuzi wa viongozi wa ngazi za uwakilishi, hatua kwa hatua wameendelea kupenya kwenye nafasi kubwa na sasa kubwa zaidi, wanaonesha nia kwamba, sasa wanaweza na wako tayari kuwatumikia Watanzania.”
Katika historia ya urais, mara chache wanawake wamejitokeza, mfano mwaka 2015 alipojitokeza Anna Mghwira kupitia Chama cha ACT-Wazalendo na alishika nafasi ya tatu nyuma ya John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kilele kilikuwa mwaka 2021 baada ya nchi kukumbwa na msiba mkubwa wa kufiwa na Rais wake, na kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Makamu wa Rais ambaye alikuwa Samia, alipanda na kuapishwa kuwa Rais wa nchi.
Lakini mwaka huu, nchi inashuhudia ongezeko la wanawake wanaowania urais sambamba na wagombea wenza.
Hali hii ni ishara kwamba, historia ya siasa za Tanzania zinafunguka upya na sura ya mwanamke katika uongozi inaanza kupata nafasi yake.