Hukumu rufaa kesi ya Nyundo na wenzake kusomwa leo

‎Dodoma. Hukumu ya kesi ya rufaa waliyoikata Nyundo na wenzake watatu ya kupinga kifungo cha maisha gerezani inatarajiwa kutolewa kesho Septemba 25, 2025 kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

‎Nyundo na wenzake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwakuta na hatia kwenye mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile Binti Mkazi wa Yombo Dovya Dar es salaam aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la XY.

‎Wakata rufaa kwenye kesi hiyo ni aliyekuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) MT. 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, askari Magereza C. 1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson (Machuche) na Amin Lema (Kindamba).

‎Wakata warufani hao wanawakilishwa na mawakili watatu wa kujitegemea ambao ni Godfrey Wasonga, Roberth Owino na Meshack Ngamando huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali,  Lucy Uisso na wenzake wawili.

‎Katika rufaa hiyo wakili wa washtakiwa waliwasilisha hoja 33 walizoziweka kwenye mafungu tisa ikiwemo kukosewa kwa hati ya mashtaka, kutothibitisha kosa bila kuacha shaka, kushindwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili mpaka sasa na ushahidi wa kieletroniki.

‎Wakijibu hoja hizo upande wa Jamhuri walisema kuwa washtakiwa hao walikutwa na hatia baada ya kuthibitisha kutenda kosa bila kuacha shaka ikiwemo ushahidi wa video zilizotolewa mahakamani na ushahidi wa mwathirika mwenyewe.

‎Katika rufaa hiyo Mahakama ililazimika kumwita shahidi ambaye ni mtaalamu wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Jeshi la Polisi nchini, ili kucheza upya DVD zilizotolewa mahakamani kama ushahidi ili kujua ni muda gani mwathiriwa alikaa na washtakiwa uliomwezesha kuwatambua.

‎Ombi hilo la kumwita tena shahidi mahakamani lilipingwa vikali na mawakili wa wakata rufaa hali iliyopelekea Jaji Amir Mruma anayesikiliza kesi hiyo, kutoa uamuzi mdogo wa mahakama na kumruhusu shahidi huyo kucheza DVD hizo ili kujiridhisha kabla ya kutoa hukumu.

‎Nyundo na wenzake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na kutakiwa kumlipa binti Mkazi wa Yombo Dovya Dar es salaam kiasi cha Sh1 milioni kila mmoja baada ya Mahakama ya hakimu Mkazi Dodoma kuwakuta na hatia ya kosa la kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo, aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la XY Septemba 30, 2024.