NCCR-Magezi yaahidi kutumbua mafisadi kikipewa ridhaa

Kibaha. Mgombea urais kupitia Chama cha NCCR-Magezi, Haji Khamis ameahidi kusimamia maadili ya uongozi na kuwawajibisha viongozi watakaobainika kutumia ofisi za umma kwa manufaa binafsi, endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Jumatano Septemba 24, 2025 mjini Kibaha, Khamis amesema moja ya changamoto kubwa nchini ni viongozi wa ngazi za utekelezaji wanaokwamisha maendeleo huku wananchi wakiendelea kuishi maisha magumu.

“Si kwamba Serikali haijafanya maendeleo, ila bado inahitaji kuongeza kasi. Tatizo kubwa ni baadhi ya watendaji wa chini wanaokwamisha utekelezaji. Historia inaonesha kwa miaka mingi   CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) amekuwa akitoa ripoti za upotevu wa fedha, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Hilo kwetu litakuwa historia. Tutatungia sheria ya kuwafunga mafisadi wote ili nchi ipige hatua,” amesema Khamis huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Aidha, amesisitiza kuwa maendeleo ya kisiasa na kiuchumi hayawezi kupatikana bila amani, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kulinda urithi huo wa Taifa.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa chama hicho, Dk Evaline Munisi amesema licha ya Mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi, wananchi wananufaika kidogo kutokana na kukosa ajira za kudumu na kulazimika kufanya kazi za vibarua vyenye malipo duni.

Matukio mbalimbali ya kwenye mkutano wa kampeni vipngozi wa chama cha NCCR magezi uliofanyika Septemba 24,2025 Kibaha Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri



“Tutaandaa sheria zitakazowalazimu wamiliki wa viwanda kuwapa kipaumbele cha ajira vijana wa maeneo husika. Vijana wameelimika, lakini wanapata taabu kwa kukosa nafasi za maana katika viwanda vinavyozunguka maeneo yao,” amesema Dk Munisi.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walieleza matumaini yao iwapo ahadi zilizotolewa zitatekelezwa kwa vitendo.

Musa Abedi, mkazi wa Maili Moja, amesema: Tumekuwa tukisikia ahadi nyingi kila uchaguzi, lakini hali ya maisha hubaki palepale. Tunataka viongozi watakaosimama kweli kwa ajili ya wananchi, si kwa masilahi yao binafsi.”

Naye Salma Shabani, mkazi wa Kibaha, amesema changamoto kubwa kwa wakazi wa Pwani ni ukosefu wa ajira licha ya uwepo wa viwanda vingi.

Kila siku vijana wanaenda viwandani kuomba kazi, wanapewa vibarua vya siku au wiki. Mwisho wa mwezi hakuna uhakika wa kipato. Tunataka mabadiliko yatakayotuonyesha manufaa ya viwanda hivi,amesema.