MTAALAMU wa tiba ya mwili kwa njia ya mazoezi (physiotherapist) wa Yanga, Youssef Ammar amesema timu hiyo kwa sasa ina utofauti mkubwa wa ubora na utimamu wa wachezaji na timu nyingine na anaiona ikifanya vizuri msimu huu huku akimtaja Djigui Diarra.
Ammar alijiunga na Yanga Agosti 2021 chini ya Nasreddine Nabi pia amefanya kazi na Miguel Gamondi kwa muda wa msimu mmoja na baadae kuondoka kabla ya kurejea msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ammar alisema amefurahia kurudi Tanzania na hususani Yanga aliyofanya nao kazi kwa mafanikio na matarajio aliyonayo kwa msimu huu pia anaiona timu hiyo ikiwa bora kutokana na aina ya kikosi alichokikuta, huku akimtaja Diarra kuwa ndio mhimili mkuu.

“Yanga ni ile ile, ila kwa msimu huu natarajia kuona makubwa zaidi kutokana na aina ya wachezaji waliopo, Diarra ameendelea kuthibitisha kuwa ni mchezaji wa daraja kubwa zaidi, kila msimu anaibuka na mbinu bora za kuipambania timu na wengine tayari nilishafanya nao kazi bado wapo na wapo vizuri, matarajio ni makubwa,” alisema Ammar na kuongeza;
“Kuna benchi la ufundi ambalo lina kocha kijana ambaye anataka kuonyesha ubora kutokana na kupata nafasi ya kuongoza timu kubwa yenye uzoefu wa soka la ndani, naona akifanya mambo makubwa kwa kusaidiana na timu bora aliyonayo.”

Ammar alisema utofauti wa Yanga na timu nyingine ni namna timu hiyo inavyojengwa kuanzia ubora wa mchezaji mmoja mmoja na utimamu tofauti na wachezaji wa timu nyingine huku akisisitiza kuwa timu hiyo imefanya ujenzi wa timu imara ikichanganya damu changa.
“Yanga inaendana na malengo msimu hadi msimu. Kwa ubora wa kikosi walichonacho sasa naiona ikifanya vizuri katika Ligi Kuu na michunao ya kimataifa na kuhusu utimamu, tangu nimejiunga na timu hii naona mabadiliko siku hadi siku na upana wa kikosi unakuwa chachu ya ushindani wa ubora baina ya mchezaji na mchezaji.’’

Akizungumzia hali ya beki wa kulia wa timu hiyo, Yao Kouassi alisema anaendelea vizuri na matarajio yao ni kuona anarejea uwanjani miezi mitatu ijayo.
“Yao anaendelea vizuri yupo chini ya uangalizi wangu na naendelea naye kwa mazoezi, nafurahishwa na maendeleo yake siku hadi siku, nafikiri hadi kufikia Januari mambo yake yatakuwa sawa na ataweza kurudi uwanjani.”