Wawili Yanga waomba kumrithi Fadlu Simba

MIONGONI mwa makocha wanaotajwa kutuma maombi ya kazi pale Simba SC kurithi mikoba ya Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco siku chache zilizopita, ni pamoja na Patrick Aussems na Didier Gomes Da Rosa ambao waliwahi kukalia kiti hicho, sambamba na waliowahi kuifundisha Yanga, Luc Eymael na Miguel Gamondi..

Kwa sasa viongozi wa Simba wapo katika mchakato kabambe wa kusaka kocha mpya, mchakato ambao unaelezwa kwamba wamepanga ukamilike wiki hii, wakati ambao kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ akikaimu nafasi hiyo kwa muda huku akishirikiana na Seleman Matola.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaelezwa kuwa, kuna majina kadhaa makubwa yametuma maombi ya kushika nafasi ya Fadlu aliyeanza kazi Raja, klabu aliyokuwa nayo kabla ya kuja Msimbazi mwaka jana yakiwamo ya Aussems na Gomes yaliyoibuka kutokana na kumbukumbu na rekodi walizoacha walipokuwa Msimbazi.

Vyanzo hivyo vinadai tayari maombi yao yamepokewa mezani na uamuzi kwenye orodha ya makocha waliotuma maombi yao unaweza kufanyika muda wowote.

Aussems alijiunga na Simba mwaka 2018 baada ya klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18. Wakati huo Simba ilikuwa na ndoto ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na Mbelgiji huyo alionekana kuwa chaguo sahihi.

Katika msimu wake wa kwanza, Aussems aliifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata hivyo, safari yao ilisimama baada ya kutolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1. Aidha, aliiongoza timu hiyo kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2018/19.

Kutokana na mafanikio hayo, Aussems aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja kuendelea na kazi yake, lakini Novemba 2019, kibarua chake kiliota nyasi baada ya jahazi kwenda mrama, huku akiondoka akitoa maneno ya mazito kabla ya kurejea nchini msimu uliopita kuinoa Singida BS.

Kwa upande wa Gomes, aliteuliwa Januari 2021 baada ya kuvunja mkataba wake na Al-Merrikh ya Sudan. Malengo yalikuwa wazi: kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuendeleza ubabe kwenye Ligi Kuu.

Gomes alifanikiwa kuandika historia ya kipekee, akikusanya pointi 13 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, rekodi ambayo hakuna klabu ya Tanzania iliyowahi kuifikia. Zaidi, aliipa Simba ushindi wa kwanza wa ugenini katika hatua ya makundi ya CAF, baada ya kuifunga AS Vita ya DR Congo kwa bao 1-0 jijini Kinshasa.

Katika jumla ya michezo 37 aliyosimama kama kocha wa Simba, Gomes alishinda 27, akatoa sare tano na kupoteza mitano, huku akitwaa mataji mawili ya ndani. Hata hivyo, alijiuzulu Oktoba 26, 2021, baada ya Simba kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa kanuni ya bao la ugenini, licha ya kushinda 2-0 ugenini lakini kuruhusu kipigo cha 3-1 nyumbani.

Kwa sasa Gomes yupo huru tangu aachane na Al-Khor SC ya Qatar wiki chache zilizopita, jambo linalomfanya kuwa chaguo rahisi kwa Simba endapo watataka kocha mwenye uzoefu wa haraka barani Afrika.

“Ni kweli Gomes ametuma maombi rasmi. Viongozi wapo katika tathmini ya kina kwa sababu wanataka kocha atakayejua mazingira ya Tanzania na pia mwenye rekodi ya kushindana kimataifa. Ndiyo maana majina ya Aussems na Gomes yanapewa nafasi,” kilisema chanzo chetu cha ndani ya Simba.

Mashabiki wa Simba sasa matumaini yao yapo kwa Hemed Morocco na Matola wakati wakingoja uamuzi wa viongozi wao kuhusu mrithi wa Fadlu.

Mbali na Gomes na Aussems kocha mwingine ambaye anatajwa kutuma maombi ya kazi Simba ni pamoja na Luc Eymael aliyefanya kazi Yanga kwa kipindi kifupi kabla ya kuachana vibaya na timu hiyo.

Fadlu aliondoka Septemba 22 baada ya kuitumikia Simba kwa siku 444 akiwa na rekodi ya kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, akiiongoza katika jumla ya mechi 53, akishinda 38, sare saba na kupoteza nane, huku akifunga mabao 101 na kufungwa mabao 30.