Dar es Salaam. Kwa sehemu kubwa, wengi wetu tunafahamu kuwa jukumu kuu la benki ni kuhifadhi fedha, kutoa mikopo, kusimamia malipo pamoja na kutoa ushauri wa kifedha.
Hata hivyo, jambo ambalo wengi hatulifahamu ni kwamba benki hizi sasa zimepewa wajibu mpana zaidi unaogusa moja kwa moja uhai na mustakabali wa kila mmoja wetu.
Katika zama hizi za changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ukame, ukataji misitu ovyo na uchafuzi wa vyanzo vya maji, taasisi za kifedha zimewekwa mstari wa mbele kama walinzi wa mazingira kupitia mfumo wa kimataifa unaojulikana kama ESG (Environmental, Social and Governance).
Mfumo huu unazitaka taasisi, hususan za kifedha, kuzingatia maadili ya kijamii, kulinda mazingira na kuhakikisha uongozi wenye uwazi katika kila hatua ya shughuli zao.
Juni 5, 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, alionya kuhusu kuendelea kwa tabia ya utiririshaji wa maji machafu na majitaka kutoka viwandani na migodini, akisema hali hiyo inahatarisha afya ya binadamu na usalama wa mazingira.
Majaliwa alibainisha kuwa uchafuzi wa mazingira umesababisha kupotea kwa baadhi ya viumbe hai, kuathiri vyanzo vya maji na kuongeza kasi ya ukame wa mara kwa mara.
“Nawasihi wananchi tutoe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili. Tuwe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe kwamba mpango kabambe wa usimamizi na hifadhi ya mazingira unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti za kila mwaka kwa kipindi cha utekelezaji wake wa miaka 10.
Kauli hii inaashiria dhahiri kuwa taasisi za kifedha, hususan benki, si watoa mikopo tu bali pia ni wadau wakuu wa uhifadhi.
Mwaka 2022, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa mwongozo maalumu unaozitaka benki kugusa moja kwa moja eneo la mazingira katika shughuli zao za kila siku.
Mwongozo huo ulisisitiza kuwa mikopo inayotolewa, hasa ile ya uwekezaji, lazima izingatie vigezo vya ESG. Hii ina maana kwamba benki sasa haziangalii tu uwezo wa mteja kurejesha mkopo, bali pia madhara ya uwekezaji husika kwa mazingira na jamii.
Mfano, iwapo mwekezaji ataomba mkopo kwa ajili ya kujenga kiwanda, benki ina jukumu la kuchunguza iwapo kiwanda hicho kitatiririsha majitaka kwenye mito, iwapo kitahifadhi taka kwa usahihi na iwapo kitatoa fursa za ajira bila ubaguzi.
Ikiwa athari ni hasi, benki inaweza kukataa kutoa fedha au kuweka masharti ya lazima yanayolenga kulinda mazingira.
Msimamizi wa Mradi wa Uwekezaji Endelevu kutoka WWF, Happiness Minja, anasema: “Benki zinafanya kazi hii lakini bado si kwa kiwango kikubwa kinachohitajika. Kwa sasa kuna mwamko mpya, hasa kwenye sekta ya uchumi wa buluu, ambapo mikopo yenye masharti makali ya uhifadhi wa mazingira inatolewa.”
Minja anabainisha kuwa wakati mwekezaji anapokaa mezani na benki, si suala la kurejea mikopo pekee, bali pia ni fursa ya kukubaliana namna uwekezaji utakavyokuwa rafiki kwa mazingira.
“Kuna fursa ya kipekee ya kugeuza mikutano ya kifedha kuwa mikutano ya hifadhi ya mazingira,” anasema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Utetezi TBA, Dan Tandasi anasema kuwa mwongozo huo unaweka wazi masharti kadhaa, kuanzia ukaguzi wa athari za kimazingira (environmental assessment), msaada wa kiufundi kwa wateja wanaoomba mikopo, hadi ulazima wa kuzingatia sheria za mazingira zilizopo.
“Kwa sasa benki nyingi zimeweka fomu maalumu za tathmini ya mazingira kabla ya kutoa mkopo.
“Hii inasaidia kuhakikisha tunakua kiuchumi bila kuharibu rasilimali za Taifa, lakini pia wananchi wanaozungukwa na uwekezaji huo wanakuwa salama,” anasema Tandasi.
Anasema kuwa hatua hiyo inalazimisha wateja wanaosaka mikopo benki kwa ajili ya kufanya uwekezaji, kuainisha mfumo mzima wa uwekezaji wao ili kuona ni kwa namna gani hauathiri mazingira na badala yake unalinda, huku akisisitiza kuwa benki inalazimika kutoa ushirikiano wa hatua kwa hatua kwa maana ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kwamba hakuna ukiukwaji wa makubaliano na kwamba mpango huo kwa sasa unakwenda vema.
Ushirikiano kati ya benki na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) Tanzania imekuwa mdau muhimu katika kuhamasisha ujumuishaji wa ESG kwenye sekta ya fedha.
Joan Itanisa, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa WWF, anasema taasisi hiyo inashirikiana na TBA ambayo inawakilisha zaidi ya benki 44 nchini.
“Fedha ndiyo ufunguo wa kufanikisha uhifadhi wa mazingira. Bila ushiriki wa benki, miradi ya misitu, mito na bahari haiwezi kusonga mbele. Ndiyo maana tunashirikiana nao kuhakikisha mikopo yote mikubwa inakubaliana na malengo ya uhifadhi,” anasema Joan.
Aidha, WWF imeweka malengo ya mwaka 2030 kuhakikisha kwamba Tanzania inajenga uchumi endelevu unaolinda rasilimali asilia.
“Kwa sasa tunatumia zaidi ya kile kinachoruhusiwa na rasilimali zetu. Tukiacha hali iendelee hivi, kufikia 2030 tutajikuta tumefika ukingoni. Hii ndiyo sababu benki ni kiungo muhimu cha mabadiliko,” anaongeza.
Changamoto za utekelezaji
Pamoja na jitihada hizi, bado kuna changamoto. Tandasi anaeleza kuwa, “Wakati mwingine wateja wanakubali masharti ya kutokuharibu mazingira lakini wakishapata fedha wanashindwa kuyatekeleza. Hapa ndipo changamoto ya usimamizi na ufuatiliaji inapoibuka.”
Aidha, si benki zote nchini ambazo zimefikia kiwango cha juu cha kuunganisha ESG kwenye shughuli zao. Baadhi bado zipo kwenye hatua za awali za kuweka mifumo ya tathmini na ripoti za uendelevu.
Hali hii inachangiwa pia na gharama kubwa za kuhamia mbinu endelevu, hasa kwa biashara ndogo na za kati. Bila msaada wa kifedha au kiufundi, taasisi ndogo zinaweza kuona masharti ya ESG kama mzigo badala ya fursa.
Vyombo vya habari kama kichocheo
Dk Ellen Otaru ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Mazingira Tanzania (JET) ambapo anasisitiza kuwa benki zinaweza kutoa fedha, lakini vyombo vya habari vina nafasi ya kutoa uelewa.
“Wanahabari wana wajibu wa kutafsiri dhana ngumu za ESG kuwa hadithi zinazoweza kueleweka na kuchochea mabadiliko ya tabia. Bila uelewa, juhudi za benki zitabaki kwenye karatasi,” anasema.