AMOUR akamuuliza: “Alikwambia ni jambo gani alilolifanya?”
Binti akajibu: “Aliniambia, lakini aliniambia iwe siri yangu.”
“Sasa ndio ninataka uitoe hiyo siri utuambie.”
“Aliniambia kuwa alipokwenda nyumbani kwa Sufiani alimvizia pale ukumbini kwao, akijua atatoka kwenda chooni kwa sababu alikuwa amelewa. Alipomuona anatoka chumbani saa tisa usiku akamnyatia kwa nyuma na kumpiga rungu la kichwa. Shefa akafa hapo hapo.
“Sasa alichokuwa anakitaka shoga yangu, mke wa Sufiani akamatwe kwa mauaji na alijua lazima atanyongwa. Akishanyongwa atakuwa amempata mume wake, na pia asiponyongwa atafungwa maisha hivyo ndoa yake na Sufiani itakuwa imevunjika.”
Msichana alipofika hapo akanyamaza kama vile alikuwa amemaliza kueleza kila kitu.
Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Kila mmoja wetu alikuwa akimtafuta huyo msichana akilini mwake. Bila shaka kwa upande wa Sufiani haikuwa hivyo, yeye alikuwa ameshamjua kwa sababu alikuwa ni hawara yake na ndiye aliyekwenda naye gesti siku ya tukio. Kumbe mwenzake alikuwa na ajenda yake ya siri.
Nilikuwa namhisi mtu huyo, lakini moyo wangu haukutaka kukubali kuwa ndiye aliyefanya hila za kiasi hicho.
“Jamani, mmemsikia shahidi wetu aliyeamua kutueleza ukweli kuhusu rafiki yake wa chenda na pete?” Amour akatuuliza na kuutanzua ule ukimya.
“Tumemsikia. Kama ni shahidi basi ushahidi wake unatosha kutufanya sote tuamini aliyezungumzwa hapo ndiye muuaji,” Sajin Meja Robert alimwambia.
Inspekta Amour alitoka mle ofisini. Baada ya muda kidogo aliingia tena akiwa amefuatana na msichana Raisa.
“Muuaji huyu hapa,” Inspekta huyo akatuambia.
Siwezi kusimulia mshituko nilioupata. Raisa alikuwa ametahayari vibaya sana. Aliinua macho yake mara moja akatutazama. Macho yake yalipokutana na yangu akayarudisha chini haraka.
“Raisa, ni wewe shoga yangu niliyekuamini na kukupenda, ndiye uliyenifanyia visa hivi?” nikamuuliza Raisa kwa kutaharuki.
Raisa alikuwa kimya. Alikuwa ameuinamisha uso wake kwenye sakafu ya chumba cha polisi kama vile alishikiwa bastola na kuambiwa ukiinua uso tu umekwisha.
“Raisa, shoga yangu umenizunguka. Kumbe vile unamtongozea Shefa halafu unatembea na mume wangu na ulikuwa na mipango ya kunimaliza umchukue mume wangu!” nikaendelea kumwambia.
Raisa alikuwa kimya akinisikiliza huku uso wake ukitazama chini kwa fadhaa na aibu.
Wale polisi nao hawakunizuia nisiyaseme niliyokuwa nayo moyoni kwani waliona yule msichana alifanya hila kubwa ya kutaka kuniangamiza. Kwa hiyo waliona waniache nimpashe.
Ile nafasi niliitumia vilivyo kumsema ili kupunguza dukuduku lililokuwa moyoni mwangu.
“Ulijiona ulikuwa mjanja sana kuja nyumbani kumuua Shefa. Kumbe vile nikihangaika ulikuwa unanichora tu. Mara unaniambia eti mke wa Shefa anakushuku wewe, mara unaniambia umeniona nikiutupa mwili wa Shefa makaburini. Kumbe ulikuwa unanifuatilia kuona nitautoa saa ngapi ule mwili na nitaupeleka wapi. Duh! Shoga wewe nakuvulia kofia! Wewe ni kiboko…!”
“Halafu yeye ndiye aliyetufahamisha kuwa wewe ulilala kwake kutukimbia polisi na ulipanda basi asubuhi kwenda Dar, ndipo tulipokufuatilia na kukukamata Muheza,” Inspekta Amour akasema na kuongeza:
“Tulipopata habari kuwa yeye ndiye anayehusika na mauaji tulimfuata nyumbani kwake na tukamkuta akiwa na rafiki yake huyu hapa. Baada ya kuwabana alitueleza mengi kama ambavyo mmemsikia sasa hivi. Alikuwa akijua siri nyingi za Raisa.”
Inspekta aliendelea kueleza:
“Katika simu yake tulikuta meseji nyingi za mapenzi walizokuwa wakiandikiana na Sufiani, na kulikuwa na meseji za nyuma kabisa ambazo alikuwa akiandikiana na Shefa. Zilionyesha kuwa alikuwa akimwambia Shefa kuwa wewe ndiye uliyemtaka kimapenzi na alikuwa akimshawishi akubali. Unaona jinsi alivyowazunguka!”
“Sasa kuna kitu ninakigundua,” yule kijana wa bodaboda akasema. “Kila siku usiku alikuwa akiniambia nimpeleke jirani na nyumba ya huyo aliyeniambia ni mdogo wake, halafu tunakaa pale nje kwa muda mrefu kabla ya kuniambia tuondoke. Sasa siku hiyo wakati tumekaa tukamuona huyo mdogo wake ambaye ndiye huyu hapa anatoa gari.”
Yule kijana alinionesha mimi kisha akaendelea:
“Baada ya huyu msichana kutoa gari, Raisa akaniambia nilifuate lile gari nyuma nyuma. Tukalifuata hadi makaburini. Akaniambia nisimamishe pikipiki, yeye akashuka na kuingia makaburini. Kumbe alitaka kumuona huyu dada akiitupa ile maiti…”
Hapo hapo nikakumbuka jinsi Raisa alivyonidanganya kwa kuniambia kuwa usiku ule aliponiona alikuwa akitoka kwenye muziki, kumbe alikuwa akinifuatilia.
“Wewe si uliniambia usiku ule ulikuwa unatoka kwenye muziki, ndio ukaliona gari langu?” nikampasha hapo hapo.
Nilipomuona amenyamaza, nikaendelea kumwambia:
“Kwa hiyo ulikuwa unanichora tu, lakini kila kitu ulikuwa unakijua…ah… we’ mwanamke una roho mbaya sana!”
Mke wa Shefa alikuwa akilia kimya kimya baada ya kusikia jinsi mume wake alivyouawa. Kadiri tulivyokuwa tunazungumza, sauti yake ya kulia ilizidi kusikika.
Kulikuwa na muda nilinyamaza, kukawa kimya kwa sekunde kama tano hivi. Mke wa Shefa akainua uso wake na kumtazama Raisa. Macho yake yalikuwa mekundu na makali kama kaa la moto.
“Nililia vya kutosha baada ya mume wangu kuuawa, lakini sasa nitalia tena baada ya kugundua kuwa wewe Raisa ndiye uliyemuua!” Mjane wa Shefa alimwambia Raisa kwa sauti ya hasira kisha akaongeza:
“Wewe Raisa ni muuaji kisha ni ndumilakuwili. Baada ya kumuua mume wangu, kila siku ulikuwa unakuja kwangu kujidai kunifariji na kuniambia unamshuku mke wa Sufiani. Ukaniambia usiku wa siku ile uliyomuua Shefa, Shefa alikwenda nyumbani kwa Sufiani wakati Sufiani mwenyewe akiwa safarini. Kumbe wewe ni muongo na mnafiki…?”
“Nisameheni jamani… nisameheni jamani, nilipitiwa na shetani tu…” Raisa alijitia kuomba msamaha huku akilia lakini hakuthubutu kuinua uso wake.
“Tukusamehe nini wakati umeshamuua mume wangu? Yaani unatoa roho ya mume wangu hivi hivi kwa sababu ya mume wa mtu! Wewe ni binadamu kweli?” Mjane wa Shefa akafoka.
“Wewe si mtu wa kusamehewa. Wewe ni muuaji unayestahili kupata adhabu kali ili iwe fundisho kwako na kwa wengine. Umenizunguka mimi, umemzunguka mjane wa marehemu, umewazunguka polisi… sasa ujanja wako umeishia wapi? Ulikuwa hujui kuwa mbio za sakafuni huishia ukingoni…?” Nikamwambia Raisa kwa hasira na kuongeza:
“Kama si ukweli huu kubainika, mimi ningenyongwa kwa kuonekana nimemuua marehemu Shefa, kumbe ni wewe!”
Raisa akanyamaza kimya. Hakuthubutu kuomba msamaha tena kwa sababu alijua kuwa kosa lake halikuwa likisameheka hata kidogo.
Inspekta Amour akamuamuru yule polisi mwanamke ampeleke Raisa mahabusu.
Raisa alipoondolewa, Amour alituambia:
“Huu ndio ulimwengu tunaoishi, watu kuzidiana mbinu. Raisa alitaka kuwazidi wenzake, alitaka kutuzidi hadi sisi polisi, lakini mimi nilikuwa makini naye sana. Tangu mapema wakati namhoji mtuhumiwa wa kwanza niligundua kuwa palikuwa na jambo ambalo lilijificha. Vinginevyo tungeishia kumpeleka mahakamani mtu asiye na hatia na kumuacha mwenye hatia.”
“Ni kweli,” Sajin Meja Robert akamwambia.
Inspekta Amour akamtazama Sufiani:
“Ndugu yangu Sufiani, umeponea tundu la sindano. Tamaa yako ya kimapenzi ingekugharimu. Ulifanya kosa kubwa kudanganywa na rafiki wa mke wako mpaka ukathubutu kuwa naye kimapenzi bila hata kuifikiria dhamiri yake! Sasa sijui hicho cha mno alichokuwa anakipata kwako ni kitu gani!”
“Labda aliniona mimi nafaidi,” nikasema.
“Unafaidi nini wakati watu ndio sisi sisi! Ni ujinga tu! Tena si ujinga wa Raisa tu bali pia ni ujinga wa Sufiani. Mara nyingine ndugu yangu jifundishe kuangalia alama za nyakati.”
“Nashukuru kwa kunipa wasia huo. Hivi sasa nitakuwa makini sana na wasichana. Kwa kweli nimepata fundisho,” Sufiani akasema, lakini alikuwa bado ameshikwa na fadhaa kwa kubainika kuwa alikuwa akitembea na Raisa.
“Halafu bado wewe dada yangu,” sasa ikawa zamu yangu.
Inspekta akaniambia:
“Ulimuamini sana shoga yako. Nadhani mlikuwa mkiambizana hata mambo ya chumbani, ndiyo maana akamtaka mume wako ili na yeye apate hiyo ladha. Hilo ni kosa la kwanza. Kosa la pili ni kushawishika kumsaliti mume wako kwa rafiki yake kama yeye alivyokusaliti wewe kwa rafiki yako. Kosa lile lile alilolitenda mume wako na wewe umelitenda. Sasa hapo mchezo umekwenda sare. Sijui ni nani atamlaumu mwenzake! Nyote mmedanganywa na shetani mmoja.”
Amour aliposema hivyo alitoa kicheko.
“Sajin Meja, sicheki kwa furaha bali ni kwa huzuni. Hili tukio limetuchanganya sana!”
“Ni kweli. Yule msichana anaonekana kuwa mjanja sana,” Sajin Meja Robert akamwambia.
“Lakini ujanja wake umekutana na wataalamu, wameufichua. Sasa amekivuna kile alichokipanda. Siku zote nasema uhalifu haulipi na hautalipa.”
Inspekta Amour akaitazama saa yake kisha akatuambia:
“Naona muda umekwenda sana, nawaruhusu mwende zenu, lakini kesho saa mbili asubuhi mfike hapa kituoni muandikishe maelezo yenu. Sawa?”
Sote tukamjibu: “Sawa.”
Bado Watatu – 39 | Mwanaspoti
