Pemba. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameahirisha shughuli zake za kiserikali huko Pemba kutokana na taarifa za kifo cha kaka yake, Abbas Ali Mwinyi, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Lumumba huko Unguja.
Abbas ambaye alikuwa mbunge aliyemaliza muda wake na mgombea ubunge katika jimbo la Fuoni, amefariki dunia leo Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo, katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Baada ya kutokea taarifa za msiba huo, Dk Mwinyi ambaye alikuwa Pemba kwa shughuli za kampeni na kiserikali, amelazimika kuondoka kisiwani humo na kurejea Unguja mapema asubuhi.
Katika ratiba yake ya leo, Dk Mwinyi alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumkabidhi mkandarasi ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba na barabara ya Chake – Mkoani yenye urefu wa kilometa 43.5.
Baada ya Rais Mwinyi kuondoka, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amemwakilisha katika hafla hiyo.
Katika ratiba ya shughuli nyingine, Dk Mwinyi alikuwa awakabidhi wakulima wa karafuu hati za mashamba ili kuwamilikisha.
Abbas ambaye pia ni rubani, atazikwa kesho Ijumaa, Septemba 26, 2025, nyumbani kwao Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya swala ya Ijumaa.