Afrika Kusini yataka Umoja wa Mataifa uongozwe na mwanamke

New York. Afrika Kusini imesema umefika wakati wa Umoja wa Mataifa kuongozwa na mwanamke na kwamba nchi hiyo inaunga mkono uchaguzi wa kiongozi mwanamke kushika wadhifa wa juu zaidi wa taasisi hiyo kubwa zaidi duniani.

Hayo yamesemwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wakati akihutubia katika siku ya kwanza ya mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.

Kwa dakika takriban 25, Rais Ramaphosa ameeleza masuala mbalimbali ambayo nchi yake inaunga mkono na yale inayopendekeza kufanyiwa mabadiliko na kuboreshwa.

Ramaphora amesema hayo wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na ikiwa mwaka, huu dunia inaadhimisha miaka 30 tangu kufanyika kwa mkutano mkubwa wa wanawake wa Beijing  nchini China.

Amesema Afrika Kusini inathibitisha dhamira yake isiyoyumba katika kuwawezesha wanawake na ushiriki wao kamili wa usawa na wa maana katika nyanja zote za maisha. “Ndiyo, na tunaunga mkono uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwanamke .”

“Mkutano wa Beijing umetukumbusha wajibu wetu wa pamoja wa kuendeleza haki za binadamu, utu na haki kwa wote. Sisi sote ni sawa, wanaume kwa wanawake na hakuna sababu kwamba tunaendelea kuwaweka wanawake wa ulimwengu nyuma.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945 Umoja wa Mataifa umekuwa ukiongozwa na makatibu wakuu wanaume pekee na Rais huyo wa Afrika Kusini amesema muda sasa umefika wa taasisi hiyo, kuongozwa na mwanamke.

Kwa mujibu wa Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 51/241 la mwaka 1997 lilieleza kwamba, katika uteuzi wa “mgombea bora,” kipaumbele kinapaswa kutolewa kwa mzunguko wa kikanda (bara) wa asili ya kitaifa ya mteuliwa na usawa wa kijinsia, ingawa hadi sasa hakuna mwanamke aliyewahi kuhudumu kwenye nafasi hiyo.

Hata hivyo, taasisi hiyo imewahi kuongozwa na naibu makatibu wakuu watatu wanawake, kwanza alikuwa Louise Fréchette kutoka Canada aliyeongoza kuanzia Machi 2, 1998 hadi Aprili Mosi 2006. Fréchette aliteuliwa katika nafasi hiyo na Katibu Mkuu, Kofi Annan.

Mwingine ni Dk Asha-Rose Migiro kutoka Tanzania aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu kuanzia Februari 5, 2007 hadi Julai Mosi 2012, aliteuliwa na Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon.

Naibu Katibu Mkuu wa tatu ambaye hadi sasa yupo ni Amina J. Mohammedkutoka Nigeria. Aliteuliwa Januari Mosi, 2017 na Katibu Mkuu, Antonio Guterres.

Mwaka 1995 ulifanyika Mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake wa Beijing uliokutanisha viongozi kutoka mataifa 189 na zaidi ya wanaharakati 30,000.

Walikutana kutengeneza na kupitisha mpango wenye dira ya kufanikisha haki sawa kwa wanawake na wasichana.

Mpango huo ulitambuliwa kama Azimio la Beijing na Jukwaa la Hatua za Utekelezaji, na imekuwa ni nyaraka iliyoidhinishwa zaidi duniani kuhusu ajenda ya haki za wanawake.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.