Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimesitisha mkutano wa hadhara na ratiba zingine za kampeni zilizopangwa kufanyika leo Alhamisi Septemba 25, 2025 ili kuomboleza msiba wa Abass Ali Mwinyi.
Abass ambaye ni kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amefariki dunia leo Septemba 25 katika hospitali ya Lumumba mjini Unguja na anatarajiwa kuzikwa kesho Septemba 26,2025 baada ya swala ya Ijumaa, Mangapwani Bumbwini.
Ratiba ya kampeni ya ACT-Wazalendo ilionyesha kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alitakiwa kufanya mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake katika Jimbo la Bumbwini.
Katika taarifa yake kwa umma, Katibu wa Idara ya Habari, Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Biman amesema kutokana na msiba wa Abass ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Fuoni wameamua kusitisha ratiba hiyo.
“Kwa kuzingatia utu, mshikamano na heshima ya kibinadamu, Chama cha ACT-Wazalendo kimeamua kusitisha shughuli za kisiasa katika eneo hilo ili kutoa nafasi kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wote kushiriki katika mazishi na kumzika kwa heshima stahiki mpendwa wao.”
“ACT-Wazalendo inaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Bumbwini katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” ameeleza Biman.
Biman amesema ACT-Wazalendo kitatoa tarehe mpya ya mkutano baada ya mashauriano na viongozi wa ngazi ya Taifa ya chama hicho.