Maonesho ya malumalu Italia yanavyogeuza nyumba kuwa kivutio

Italia. Kila mwaka jiji la Bologna nchini Italia hubadilika na kuwa kitovu cha ubunifu wakati wa maonyesho ya Cersaie Week ambayo hudumu kwa wiki moja katika kituo cha maonesho Bologna.

Maonesho haya ambayo huleta waonyeshaji kutoka pande tofauti za dunia hutoa fursa ya wao kuonesha bunifu zao katika ubunifu wa vigae sisi tunaweza kuita ‘malumalu’ kama tulivyozoea na mapambo ya nyumba.

Jiji hili ambalo mitaa yake yenye rangi ya udongo hujaa wageni kutoka duniani kote, wakiwa na shauku ya kugundua mitindo mipya ya malumalu zilizobuniwa na kampuni mbalimbali huku wakizigusa kwa mikono, kuziangalia kwa karibu ikiwa ni moja ya jambo linalotajwa kuweka urahisi kwao wanapotaka kufanya maamuzi ya kununua bidhaa yoyote.

Ndani ya kumbi kubwa za maonesho, malumalu huwekwa kwa mitindo mbalimbali ambazo zinaweza kuvuta wateja huku kampuni zikishindana kuonesha ubunifu kuanzia kwenye rangi zinazotumika katika utengenezaji na hata njia inayotumika katika kuonesha bidhaa husika.

Ndani ya eneo la kilomita za mraba 155,000 zilizotumiwa na kampuni hizo mwaka huu, unapopata nafasi ya kupita ni lazima utajiuliza swali kama mswahili baada ya maonesho hivi vyote vinaenda kuvunjwa?

Hiyo ni kwa sababu waoneshaji 620 wanaofanya kazi katika sekta hii ya malumalu wametumia mbinu, mbalimbali katika kumvuta mtazamaji na kumuonesha kwanini anapaswa kuchagua bidhaa zao.

Ni zaidi ya mabafu ya kuogea yalivyojengwa kwa ustadi ndani ya maonesho haya, ni zaidi ya vyumba vya kulala ni zaidi ya sehemu za kufanyia kazi au ofisi za nyumbani, ni zaidi ya varanda za nyumbani kwako.

Hii inamaanisha kuwa hawaoneshi tu bidhaa wanazozalisha wakiwa wameziweka katika maboksi bali wanakuonyesha namna ambavyo, bafu, ukuta wa nyumba yako, varanda, ofisi ya nyumbani kwako itakuwa baada ya kutumia bidhaa zao.

Baadhi ya mabanda unapoyatembelea unaweza kusahau kama uko kwenye maonesho na kudhani uko ndani ya nyumba ambayo watu wanaishi kwa namna ambavyo bidhaa zinaoneshwa.

Hali hiyo inafanya sehemu hii kuwa si tu ya maonesho bali kivutio kwa watembeleaji kutokana na aina ya maonesho yanayofanyika.

Katika hali ya kawaida mtu akisikia maonesho basi kitu kinachokuja akilini ni aina ya uwanja utakaotumika.


Hili ni tofauti kidogo kwani kituo hiki cha maonesho ambacho kila banda limepewa aina yake ya wawekezaji, kimewekewa mfumo wa kiyoyozi katika kila banda huku nje zikitandikwa kapeti nyekundu katika baadhi ya maeneo ya lami ambayo imesafishwa kwa kiwango cha juu hali inayofanya hata mtu akivaa raba nyeupe kuondoka kama alivyokuja.

Licha ya mpishano mkubwa wa watu lakini hali ya hewa unapokuwa ndani ya mabanda husika haikufanyi kuhisi joto hata kama umevaa suti ya kitambaa kizito na shati la mikono mirefu ndani yake.

Katika moja ya kitu ambacho kimevuta hisia za watu wengi ni maonesho haya kuibeba sekta nzima ya uzalishaji malumalu na bidhaa nyingine zinazofanana na hizo.

Hali hiyo imefanya kampuni nyingine zinazofanya kazi katika mnyororo huo wa thamani nazo kuchangamkia fursa, kuwaonesha wazalishaji namna shughuli wanazofanya zinavyoweza kuwasaidia katika kufikia masoko kwa urahisi na kuwafanya wazalishe kwa ubora unaotakiwa.

Moja ya wanaoshiriki maonesho hayo ni viwanda vinavyozalisha bidhaa, fremu mbalimbali zinazoweza kutumika kuonyesha malumalu kwa urahisi kwa wateja.

Ofisa msaidizi wa masoko kutoka kampuni ya VEP87, Michael Giovanard anasema wanaamini katika kuwapa mbinu rahisi ya kuonyesha bidhaa zao kwa wateja kama mbinu inayoweza kukuza masoko.

Anasema kampuni yake imekuwa ikitengeneza fremu mbalimbali za chuma na katika ukubwa tofauti ili kuhakikisha wazalishaji wanapata urahisi wa kufikia wateja wao.


“Tunazo fremu za ukubwa mdogo mpaka kubwa zaidi kulingana na mahitaji ya mteja. Tunaweza kukutengenezea fremu kama kitabu uli uweze kuweka bidhaa zako nyingi na kuzionyesha kwa urahisi. Pia tunaweza kukuwekea vile unavyohitaji na hata ukitaka tutumie meza tunaweza,” anasema Giovanard.

Mbali na kuonesha ufikiaji masoko kwa njia rahisi na haraka pia ni jambo ambalo liliangaliwa kwa ukaribu na kampuni ya Visoft.

Kampuni hii yenyewe inaamini katika kutumia teknlojia kufikia wateja wate duniani, huku ikiwaunganisha wazalishaji na wateja wao kwa njia ya mtandao.

Si kuwaunganisha tu, kampuni hiyo imekuwa ikihakikisha wateja wanapata kile wanachokihitaji kwa kujaribu kutengeneza muundo wa sehemu wanayotaka kuweka malumalu, katika mfumo na kuona namna wanavyoweza kufanya mpangilio wa rangj na hata sehemu husika.

Hilo linawezekana kwa wateja kuweka vipimo sahihi vya eneo wanalotaka kufanyia kazi kama ni bafu, chooni au sebule ili aweze kupewa mapendekezo juu ya namna anavyoweza kubadili muonekano wa eneo lake.

“Tunampatia mteja kilicho bora, kwani anapata nafasi ya kujaribu si tu rangi za malumalu, sakafuni na ukutani pia tunamsaidia hata kuonesha rangi ya ukuta anayoweza kutumia baada ya kuweka sakafu yake,” anasema Michael Nissler ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Visoft.

Kupitia mfumo wake wazalishaji wa bidhaa kutoka pande tofauti za dunia, wamesajiliwa na kupewa uwezo wa kufanya biashara kwa urahisi pindi wateja wanaporidhika na mapendekezo wanayokuwa wamepewa.

“Mteja akiridhika anapewa namna ya kulipia bidhaa ili iweze kumfikia pale alipo, hii inamhakikishia kupata bidhaa anayohitaji kutoka kwa mzalishaji moja kwa moja,” anasema.

Mbali nao pia kulikuwa na viwanda vinavyozalisha mashine kwa ajili ya kukata malumalu, saruji kwa ajili ya kubandikia, gundi, vifaa mbalimbali vinavyotumika katika ujenzi ikiwemo vile vinavyohakikisha sakafu inanyooka.

Kampuni changa zapewa nafasi

Kama sehemu ya mkazo wake unaoendelea kuhusu ubunifu na kuhakikisha uendelevu wa sekta husika, maonesho haya ya Cersaie yametoa nafasi kwa kampuni changa (startups) sita zinazobobea katika suluhu za mapambo ya nyumba na usanifu wa ndani.

Kampuni hizo changa za Kiitaliano zinazofanya kazi katika nyanja mbalimbali ikiwemo mapambo ya bafu, ustawi, mazoezi ya mwili zinatarajia mchango muhimu katika maonesho hayo na uendelevu wa sekta husika.

Wakati uzalishaji malumalu ikiwa ni jambo ambalo linaangaliwa kwa ukaribu na kampuni zote, wengine walikuja na mbinu inayoweza kusaidia kulinda ubora wa bidhaa hizo zinapojengewa sehemu mbalimbali.

Kampuni ya Progress Profiles SPA wao wamekuja na mfumo wa kuweka ukavu katika sakafu yako ili kuhakikisha maji hayaathiri ubora wa malumalu baada ya kujenga.

Meneja wa kanda ya Pacific kutoka kampuni hiyo, Andrea Vaccari anasema umeme pia ni moja ya njia inayoweza kutumika kuleta ukavu katika malumalu hasa maenso ya bafuni ili kuepudha kubanduka.

Vaccari anasema njia hiyo hutumika kwa kutandaza waya maalumu katikati ya malumamalu moja nyingine wakati wa kujenga ambao utafanya kazi bila kusababisha athari kwa binadamu.

“Tumefanya utafiti wa hali ya juu sana na hakuna athari ambayo mtu anaweza kupata zaidi ya kuhakimisha uimara wa biddhaa yake kudumu kwa kuda mrefu tangu anapojenga,” anasema.

Maonesho haya ya siku tano yalianza rasmi Septemba 22 na yanatarajiwa kukamilika Septemba 26 mwaka huu, huku mikataba mbalimbali ya wasambazajj na wazalishaji ikitarajiwa kusainiwa ili kupanua wigo wa masoko.

Zingatia haya kabla ya kufanya uamuzi wa kifedha                                                                                                                    

Kila siku tunafanya uamuzi wa kifedha ambao ni sehemu muhimu ya safari ya kila mtu katika kuendesha maisha na pia kuelekea ustawi wa kifedha.

Hata hivyo, watu wengi mara nyingi hupuuzia umuhimu wa kupanga, kufanya utafiti, na kulinganisha watoa huduma au bidhaa kabla ya kufanya uamuzi wa kifedha.

Tabia hii inaweza kusababisha matumizi yasiyo ya lazima, kupoteza rasilimali, na hata matatizo ya kifedha kwa muda mrefu.

Kwa hivyo, ni muhimu kuelewa kwa nini mipango na kufanya manunuzi ya kiutafiti ni hatua za msingi katika kufanikisha malengo ya kifedha.

Kwanza, mipango ni msingi wa uamuzi bora wa kifedha. Bila mpango, ni rahisi kupoteza mwelekeo na kutumia pesa kiholela. Mipango inahusisha kuweka malengo ya kifedha, kama vile kuokoa kwa ajili ya dharura, kununua mali, au hata kuwekeza kwa ajili ya siku zijazo.

Kwa mfano, mtu anayepanga kununua chombo cha usafiri anaweza kuanza kwa kuamua bajeti yake, aina ya usafiri anaoutaka, na gharama za ziada kama vile bima na matengenezo.

Bila mpango huu, mtu anaweza kujikuta akinunua chombo cha usafiri ambao hauendani na uwezo wake wa kifedha, jambo ambalo linaweza kusababisha madeni yasiyohitajika.

Pili, kufanya utafiti kabla ya kufanya maamuzi ya kifedha ni njia bora ya kuhakikisha unapata thamani bora kwa pesa zako hata kama ni ndogo. Utafiti unasaidia kuelewa chaguzi mbalimbali zinazopatikana sokoni na faida au hasara za kila chaguo.

Kwa mfano, unapofikiria kununua bidhaa kubwa kama vyombo vya kieletroniki kama fridge, televisheni au simu, ni jambo muhimu kufanya utafiti kuhusu wauzaji tofauti, bei na maoni ya wateja kunaweza kukusaidia kuchagua bidhaa bora zaidi kwa bei inayofaa.

Bila utafiti, unaweza kulipa zaidi kwa bidhaa ambayo ungeweza kupata kwa bei nafuu mahali pengine.

Zaidi ya hayo, kulinganisha watoa huduma au bidhaa ni mbinu muhimu ya kufanya maamuzi ya kifedha yenye busara. Watoa huduma tofauti mara nyingi hutoa bei na masharti tofauti kwa bidhaa au huduma zinazofanana.

Hii inakusaidia kuepuka kulipa zaidi kwa huduma ambayo ungeweza kupata kwa bei nafuu mahali pengine. Aidha, kulinganisha kunakupa nafasi ya kujadili masharti bora zaidi, jambo ambalo linaweza kuokoa pesa nyingi kwa muda mrefu.

Kwa watu wanaoamini kuwa hakuna haja ya kufanya utafiti au kulinganisha, ni muhimu kuelewa athari za maamuzi ya haraka. Bila utafiti, unaweza kununua bidhaa au huduma ambayo haikidhi mahitaji yako au hata kugundua baadaye kuwa ulilipa zaidi kuliko ilivyohitajika.


Kwa mfano, mtu anayenunua bidhaa bila kulinganisha bei anaweza kugundua kuwa duka jirani lilikuwa na ofa bora zaidi. Hali kama hizi zinaweza kusababisha majuto na kupoteza pesa ambazo zingeweza kutumika kwa mahitaji mengine muhimu.

Ni muhimu kuelewa kuwa mipango, utafiti na kufanya manunuzi ya kiutafiti ni hatua bora kabisa kwa mtu yeyote anayetaka kufanya maamuzi yenye thamani ya kifedha. Tabia hizi zinakusaidia kutumia pesa zako kwa busara, kuepuka matumizi yasiyo ya lazima, na kufanikisha malengo yako ya kifedha kwa ufanisi.

Kwa hivyo, usifanye manunuzi ya pupa bali, chukua muda wa kupanga, kufanya utafiti, na kulinganisha bei na huduma zako.

Hatua hizi rahisi zinaweza kuleta tofauti kubwa katika safari yako ya kifedha na kukusaidia kufikia ustawi wa kifedha kwa muda mrefu.