MCT yasisitiza vyombo vya habari visiwe na upande wakati wa uchaguzi

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT), limesema katika kipindi cha uchaguzi, vyombo vya habari vina wajibu wa kuwa kiungo cha ukweli, badala ya propaganda na kuegemea upande mmoja.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Thomas Mihayo amesema  ni muhimu vyombo vya habari na wanahabari kubeba ujasiri huo kwani ndiyo ushahidi wa uhuru wao.

Jaji Mihayo ameyasema hayo leo, Alhamisi Septemba 25, 2025 alipowahutubia wanachama wa MCT katika mkutano mkuu wa baraza hilo, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema ni wajibu wa kila chombo cha habari kuwa kiungo cha ukweli, badala ya propaganda katika kipindi cha mitazamo tofauti hasa cha uchaguzi.


Jaji Mihayo amesema ni muhimu vyombo hivyo, kuzingatia na kuripoti uhalisia na ukweli wa yanayohubiriwa na vyama vyenye sera, itikadi tofauti na ilani za uchaguzi tofauti kuliko kuegemea upande mmoja.

 “Tujiulize kwa mfano, chombo gani cha habari kilicho huru leo kuweka katika mizania sawa kwa mitazamo tofauti kati ya wanaosimamia, Oktoba tunatiki? Au No reforms, No election? Au Oktoba Tunalinda kura?

“Wingi wa vyombo vya habari unaotajwa kuwa ndiyo uhuru wenyewe unatupa taswira gani ya mitazamo tofauti inayoweza kutolewa na chombo kimoja,” amehoji.

Katika hotuba hiyo, Jaji Mihayo amesema vyombo vya habari vilivyo huru vina nafasi ya kufichua maovu, kutetea haki za binadamu, kupaza sauti za wanyonge na kuwapa wadau taarifa sahihi ili wafanye uamuzi sahihi kuhusu maisha yao ya kila siku.

Amesema baraza hilo, lilipoanzishwa miongo mitatu iliyopita lilijenga misingi imara ya kujisimamia na kusimamia maadili na weledi wa taaluma ya habari na wanahabari.

Kuwepo kwa baraza hilo, amesema kumeokoa vyombo vingi vya habari dhidi ya mtego wa kufilisiwa au kufilisika kutokana na faini za mabilioni ya fedha iwapo kesi ingepita katika mkondo wa kimahakama.

“Mfumo wa kutumia usuluhishi ambao umekuwa ukifanywa na MCT umeifanya taaluma iwe salama zaidi kwa kuwa uamuzi mbalimbali wa usuluhishi umekuwa funzo kwa waandishi wa habari na wadau wa habari,” amesema.

Jaji Mihayo, amesema ushirikiano kati ya MCT na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), ni somo la kujifunza.

Ameeleza kila chombo cha habari kimeegemea upande wake na baadhi ya mitazamo inaminywa isisikike kabisa.


Jaji Mihayo ametaka vyombo vya habari visisahau wajibu wake wa kuwa darajа kati ya wananchi na viongozi wao, viwe na hoja na majibu ya maswali ya msingi kuhusu mustakabali wa Taifa.

Kuhusu uchumi kwa vyombo vya habari, amesema miaka 30 iliyopita hali ilikuwa nzuri, lakini hali hiyo imebadilika siyo Tanzania tu, bali duniani kote.

“Tuepuke vishawishi vya kutumia mambo binafsi na yasiyo binafsi tuliyoyabaini wakati wa kutenda kazi zetu kuwatisha watu ili watupatie fedha au upendeleo fulani,” amesema.

Ametaka wadau wa habari wakatae rushwa na kununuliwa hasa kipindi cha uchaguzi, akisisitiza “mtu akikununua anatarajia ubaki umenunuliwa, Hategemei kesho umwambie sasa wewe ni mtu huru, hutaki akutumie. Atafanya kila njia kukudhuru maana atakuona msaliti ama muasi.”

Jaji Mihayo amesema dunia kwa sasa ipo katika mabadiliko ya kiteknolojia na matumizi ya akili unde, jambo linalochochea habari nyingi za upotoshaji na zisizokuwa sahihi.

“Ninawaasa waandishi wa habari waendelee kuzingatia kanuni kubwa kabisa ya kazi yetu, ambayo ni kuwa wakweli. Tuepuke hiana, tuepuke kufanya kazi kwa chuki. Tusitumike na wanasiasa, wala wenye pesa na hata wamiliki wa vyombo vyenu,” amesema.

Jaji Mihayo, ameeleza umuhimu wa vyombo vya habari kutumika katika mazungumzo kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

“Hatuwezi kufanikisha dira hii bila ushiriki wa vyombo vya habari vinavyowajibika kwa wananchi. Kwa mantiki hiyo, ninatoa wito kwa wanachama wa MCT, kuwa mstari wa mbele kufichua changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura amesema kwa sasa baraza hilo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, limefanikiwa kupunguza utegemezi wa asilimia 90 hadi 60 kutoka wa wafadhili.


“Ikiwa tunataka baraza liendelee kuwahudumia, ni lazima kila mmoja wetu ajiulize anaweza kuchangia vipi kuifanya MCT ijitegemee. Zile enzi za kudhani MCT wana wafadhili watakaotoa fedha zimekwisha,” amesema.