NYOTA wa Namungo, Fabrice Ngoy amesema kucheza timu moja na mshambuliaji mwenzake raia wa DR Congo, Heritier Makambo kunampa motisha kuhakikisha anaendelea kupambana katika kikosi cha kwanza, kila anapopata nafasi uwanjani.
Kauli ya Ngoy inajiri baada ya kuongezewa washambuliaji wengine akiwemo Makambo aliyewahi kuichezea Yanga na msimu uliopita alicheza Tabora United (kwa sasa TRA United) na kuifungia mabao matano ya Ligi Kuu Bara.
“Makambo ni kaka yangu ambaye kila siku najifunza kutoka kwake, msimu huu ni mgumu kuanzia ushindani wa Ligi Kuu Bara na hata wachezaji wenyewe, kwangu inanipa motisha ya kupambana kila ninapopata nafasi uwanjani,” alisema Ngoy.
Nyota huyo aliyeifungia Namungo bao moja katika ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Tanzania Prisons, Septemba 21, 2025, alisema ataendelea kupambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake, ili kwa pamoja wafikie malengo.
Uongozi wa timu hiyo pia ulimwongeza aliyekuwa mshambuliaji wa TMA ya Arusha, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship akiwa na mabao 18.
Idadi hiyo ya mabao 18 aliyofunga Shahame anayefananishwa na mshambuliaji wa Klabu ya Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, ni sawa pia na ya nyota wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh na Andrew Simchimba aliyekuwa anacheza Geita Gold.
Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.
Mshambuliaji huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu uliopita wa 2024-2025, akiwa na kikosi hicho cha Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, alikifungia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara.