Mbeya. Mahakama Kuu, masjala ndogo ya Mbeya mkoani Mbeya, imebariki kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh3.7 milioni, alichohukumiwa dereva wa lori, Philipo Mwashibanda aliyesababisha vifo vya abiria 26.
Hukumu hiyo imetolewa Septemba 22,2025 na Jaji Joachim Tiganga na kuwekwa katika tovuti ya mahakama leo Septemba 25,2025, ambapo Jaji ameitupa rufaa ya dereva huyo na kusisitiza adhabu aliyopewa ilimstahili.
Juni 7, 2025, katika eneo la Mlima Iwambi barabara kuu ya Mbeya-Tunduma, dereva huyo akiendesha lori aina ya Scania lenye tela alishindwa kulimudu gari hilo kutokana na uendeshaji wa hatari.
Lori hilo lilikwenda kugongana na basi dogo aina ya Mitsubishi Rosa ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva Baraka Samiel Mgalla na kusababisha vifo vya watu 26 waliokuwa katika basi hilo na majeruhi 10.
Alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi, Paul Rupia wa Mahakama ya wilaya ya Mbeya na kushitakiwa kwa makosa 37 ya uendeshaji wa hatari wa gari, na kusababisha ajali iliyosababisha vifo na majeruhi.
Kosa la kwanza hadi la 26 lilihusu uendeshaji wa hatari wa lori hilo na kusababisha vifo vya abiria 26 waliokuwa katika basi dogo, kosa la 27 hadi la 36 la kusababisha majeruhi na kosa la 37 la uendeshaji mbaya wa lori uliosababisha ajali hiyo.
Juni 24,2025 alitiwa hatiani baada ya kukiri makosa hayo ambapo kwa kosa la kwanza alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh100,000 kwa kila kosa kuanzia kosa la kwanza hadi la 36 katika shauri hilo.
Adhabu hiyo iliamriwa kutumikiwa kwa pamoja alitakiwa kutumikia kifungo cha miaka 108 na kulipa faini ya Sh3.6 milioni, lakini kwa kuwa vifungo viliamriwa kutumikiwa pamoja, atatumikia miaka 3 jela na kulipa faini ya jumla Sh3.6 milioni.
Katika kosa la 37, alihukumiwa kifungo cha miaka 3 na kulipa faini ya Sh100,000.
Baada ya kuhukumiwa, kupitia kwa wakili Philip Mwakilima, Mwashibanda hakuridhishwa na hukumu hiyo akaamua kukata rufaa akiegemea katika sababu kuu nne za rufaa kupinga kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa.
Alijenga hoja kuwa Hakimu aliyemhukumu alikosea kisheria na kimantiki pale aliposhindwa kuzingatia taratibu sahihi wakati wa kumtia hatiani na kumhukumu.
Pia kupitia kwa wakili huyo, dereva huyo alieleza kuwa Hakimu alikosea kisheria na kimantiki kwa kushindwa kumpa nafasi mrufani kubishania maelezo yaliyosomwa na upande wa Jamhuri au kupewa nafasi ya kuongeza katika maelezo hayo.
Halikadhalika alilalamika kuwa Hakimu alikosea kisheria na kimantiki pale aliposhindwa kuzingatia kuwa wakati wa maombolezo (mitigation), mtuhumiwa aliibua utetezi fulani ambapo hakimu alitakiwa abadili kukiri kwake kosa.
Mwisho, alidai Hakimu alikosea kisheria na kimantiki kwa kushindwa kufafanua visababishi vya makosa ambayo mrufani alikuwa akishtakiwa nayo, lakini pia alishindwa kurekodi kile ambacho mrufani alikieleza kuhusu makosa hayo.
Upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Salmin Zuberi, ulipinga sababu hizo za rufaa, akishikilia msimamo kuwa hakuna rufaa ambayo inaweza kukatwa kutokana na mshtakiwa mwenyewe kukiri makosa yake.
Wakili huyo alisema mashtaka dhidi ya mrufani yalisomwa kwa lugha ya Kiswahili anayoielewa vizuri na akajibu ni kweli alisababisha ajali na vifo na baadaye alikiri shtaka moja baada ya lingine kadri alivyosomewa na upande wa mashtaka.
Hukumu ya Jaji ilivyokuwa
Katika hukumu yake, Jaji Tiganga alisema baada ya kupitia kwa umakini kumbukumbu za usikilizwaji wa shauri hilo, sababu za rufaa na mawasilisho ya pande mbili, hoja ya kutolewa uamuzi inahusiana na mrufani kukiri kosa.
Jaji alisema hoja ni kama kukiri kwake huko kulichukuliwa kwa usahihi na Hakimu aliyesikiliza shauri hilo na kama ilitosheleza kumtia hatiani mrufani.
Alieleza kuwa katika shauri hilo, mwenendo wa kesi hiyo unaonyesha hati ya mashitaka ilisomwa kwa mrufani na kuelezewa kwa Kiswahili na mrufani akajibu (akinukuu alichojibu mahakamani) “Kweli na sahihi, nimesababisha ajali na vifo”.
“Baada ya kusomewa shtaka, upande wa Jamhuri ulielezea maelezo ya kosa kuwa aliendesha lori aina ya Scania na kugongana na Mitsubish Rosa na kusababisha vifo 26, majeruhi 10 na kuharibu magari na akakubali maelezo hayo,”alisema Jaji.
“Kwa mtazamo wa mahakama hii, utaratibu ulizingatia kikamilifu kifungu cha 245(2) cha CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai) na kukiri kwake kulirekodiwa kwa usahihi na hakuwezi kukosolewa,”alieleza Jaji Tiganga.
“Kwa kuongezea, makosa yote yalisomwa moja baada ya lingine ikifuatiwa na maelezo ya kina ya kila kosa kwa lugha ya Kiswahili ambayo mrufani kila alipoulizwa aliyathibitisha maelezo hayo kuwa ni sahihi,”alisisitiza Jaji.
Zaidi ya hayo, Jaji alisema uzito wa ushahidi wa Jamhuri uliongezewa na kuwasilishwa kwa vielelezo zikiwamo taarifa za uchunguzi wa vifo (postmortem reports), maelezo ya onyo ya mshtakiwa, PF 3 na ramani ya eneo la ajali.
“Kila kielelezo kilisomwa mahakamani na kilivyowekwa mbele yake (mrufani) alijibu na kukiri kuwa ni kweli maudhui ya nyaraka hizo ni sahihi,”alisema Jaji Tiganga katika hukumu yake hiyo akibariki hukumu ya mahakama ya wilaya.
Ni kwa msingi huo, Jaji alisema ameridhika kuwa kulikuwa hakuna dosari zozote za kisheria na kwamba kutiwa hatiani kwa mrufani huyo kulikuwa ni sahihi kisheria hivyo kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa ilikuwa sahihi kisheria.