Mnigeria aongeza mzuka Mtibwa Sugar

BEKI wa kati wa Singida Black Stars, Mnigeria Victor Chukwuemeka Collins amejiunga na Mtibwa Sugar kwa mkopo wa mwaka mmoja, huku kocha wa kikosi hicho, Awadh Juma ‘Maniche’, akieleza ataongeza ushindani na nyota wengine waliopo kikosini.

Collins aliyezaliwa Novemba 2, 2024, katika mji mkuu wa jimbo la Enugu, Nigeria, amejiunga na Singida dirisha kubwa la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea, Nasarawa United, ingawa ametolewa kwa mkopo kwenda Mtibwa Sugar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maniche alisema kuna baadhi ya wachezaji waliokosa mechi ya kwanza ya msimu huu ambao kikosi hicho kilichapwa kwa bao 1-0, ugenini dhidi ya Mashujaa, Septemba 21, 2025, japo kwa sasa kila kitu kinaendelea vizuri.

“Kuna wachezaji wengine ambao hawakuonekana katika mechi yetu iliyopita tunaoamini huko mbeleni tutaanza kuwaona, ni kweli hatujaanza vizuri ila hata ukiangalia hatujacheza vibaya, isipokuwa ni makosa madogo madogo,” alisema Maniche.

Collins aliyecheza Nasarawa United na Remo Stars zote za kwao Nigeria, amewahi kuichezea pia Amanat Baghdad SC ya Iraq, ikielezwa alisajiliwa Singida kwa lengo la kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mghana Frank Assinki aliyejiunga na Yanga.

Licha ya kusajiliwa ila inaelezwa uongozi umemtoa kwa mkopo kwenda Mtibwa ili apate nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza zaidi, akiungana na beki wa kushoto Mghana Ibrahim Imoro na kiungo mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Serge Pokou.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara na pointi zake 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja msimu wa 2022-2023.