WACHEZAJI takribani 137 wamejitosa kushiriki mashindano ya Lina PG Tour msimu wa nne yaliyoanza leo kwenye viwanja vya Gofu vya Gymkhana mkoani Morogoro.
Mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika 2024 yanaendelea tena mwaka huu yakiwa na lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani timu ya taifa ya wanawake marehemu Lina Nkya aliyekuwa na mapenzi makubwa na mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa mashindano hayo, Ayne Magombe amesema kati ya wachezaji hao waliojiandikisha kushiriki 65 ni wachezaji wa gofu wa kulipwa na chipukizi huku 72 wakiwa wachezaji wasindikizaji.
Amesema mashindano hayo yameanza leo Septemba 25 na yanatarajiwa kumalizika Septemba 28, 2025 na wanewaomba wachezaji kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michuano hiyo ambayo ina lengo la kukuza mchezo wa gofu nchini.
“Kama kawaida familia ya Said Nkya wameendelea kuyaandaa mashindano haya kwa lengo la kumuenzi mama Lina, kwa Morogoro yatafanyika kwa siku nne yakihusisha mashimo 72, hivyo niwaombe wapenzi wote wa mchezo wa gofu hasa waliopo Morogoro na sehemu mbalimbali kujitokeza kushiriki. Kwa pamoja tuongeze ujuzi zaidi, kukuza vipaji na vipato vya wachezaji wetu,” amesema na kusisitiza;
“Mashindano ya Lina Tour yatakuwa ni endelevu, kwa sasa tuna mashindano matano kwa mwaka, lakini tukipata sapoti kwa wadau wengine tunaweza kuwa na mashindano mengi zaidi ili kukuza huu mchezo.”
Mchezaji wa gofu chipukizi kutoka klabu ya Lugalo, Prosper Emmanuel amesema, amejipanga vema kuhakikisha anacheza vizuri na hatimaye kuibuka mshindi katika mashindano hayo.
“Watu kila shindano wanajipanga vizuri, nami nimeendelea na mazoezi na ninaimani kuwa kwa msaada wa Mungu nitafanya vizuri, niwaombe wachezaji kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki michuano hii,” amesema
Hata hivyo, ameipongeza familia ya Lina kwa namna wanavyoendesha mashindano hayo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa ya kuvutia na bora hapa nchini.
Kwa upande wa mchezaji wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya ameitaka jamii hasa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo ambayo yanalenga kuongeza ujuzi na kukuza vipaji.
Fadhili amesema kila mtu ana uwezo wa kucheza mchezo huo wa gofu na kwamba mishuano hiyo ya Lina inawasaidia wachezaji kufanya mazoezi ya kutosha ili kushiriki mashindano ya kimataifa nje ya nchi.