Katika kuendeleza dhamira yake ya kuchochea maendeleo ya kilimo nchini, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendesha semina maalum kwa wakulima wa Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Bukoba.
Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa ELCT, ikiwa ni jukwaa la maarifa lililowakutanisha wakulima takribani 100 kwa lengo la kupata uelewa kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa na Benki.
Kupitia mafunzo haya, wakulima walipata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu upatikanaji wa mikopo ya kilimo, huduma za uwezeshaji wa uzalishaji, na mbinu bora za kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Semina hii ni ushuhuda wa azma ya TADB ya kuendeleza kilimo chenye tija, jumuishi na endelevu kilimo kinachojenga maisha, jamii na uchumi wa Taifa.
Sambamba na semina hiyo, TADB inatarajia kufungua ofisi ndogo mkoani Kagera, hatua muhimu inayolenga kusogeza huduma karibu zaidi na wakulima, wafugaji, na wadau wa sekta ya kilimo.