WAHANDISI VIJANA WATAKIWA KUJIAJIRI, KUTATUA CHANGAMOTO ZA TAIFA

::::::::

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk. Charles Msonde, amewataka wahandisi vijana nchini kutumia taaluma yao si tu kwa ajili ya kujipatia kipato, bali pia kama nyenzo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na Taifa kwa ujumla.

Dk. Msonde alitoa wito huo jijini Dar es Salaam, Septemba 24, 2025, wakati akihitimisha kongamano la siku mbili la Wahandisi Vijana (Young Engineers Forum – YEF), lililoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Msonde alisema jukwaa hilo ni muhimu si kwa maendeleo ya mtu binafsi pekee bali pia kwa ustawi wa jamii nzima, na kwamba vijana wanapaswa kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya mabadiliko.

“Tunapohitimisha jukwaa hili, tukumbuke kwamba mbegu ili iote lazima ioze. Msikate tamaa mnaposhindwa kwa mara ya kwanza. Jaribuni tena na tena mpaka mpate suluhisho,” alisema Dk. Msonde.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa majukwaa kama hayo kufanyika mara kwa mara hasa kwa kuzingatia kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani, akisema yanaongeza fursa ya ubunifu na uvumbuzi.

“Dunia ya sasa inahitaji tukutane mara kwa mara, tubadilishane uzoefu na mawazo. Tumeshuhudia bunifu kama kifaa cha kugundua vitu vya kigeni kwenye viwanja vya ndege kikiwekwa, na hii imeongeza usalama. Hii ni mojawapo tu; zipo nyingi,” aliongeza.

Pia alihimiza vijana kutumia mifumo ya ndani ya kiufundi kuendeleza bunifu zao kwa kuwa inaleta manufaa kwao binafsi na kwa Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Eng. Menye Manga, alisema bodi itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri na kuwasaidia vijana wengine kupata ajira kupitia ubunifu.

“Bodi itaendeleza mafunzo haya ili wahandisi vijana waweze kuanzisha ajira kwao na kwa vijana wengine,” alisema Eng. Manga.

Naye, Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Mercy Jilalala, alisema jumla ya wahandisi vijana 145 walihudhuria kongamano hilo moja kwa moja ukumbini, huku wengine 84 wakishiriki kwa njia ya mtandao.

Alisema mafunzo hayo yamekuja baada ya bodi kubaini kuwa wahitimu wengi wa uhandisi wamekuwa wakisubiri ajira za moja kwa moja kutoka serikalini au sekta binafsi, hali inayochangia kuongezeka kwa vijana wasio na ajira licha ya kuwa na elimu.

“Kupitia kongamano hili, tumeamua kuwapa mafunzo yatakayowasaidia kujiajiri kwa kutumia taaluma walizonazo,” alisema Jilalala.

Kongamano hilo limekuwa sehemu ya juhudi za ERB kuhamasisha ubunifu, ujasiriamali na matumizi sahihi ya taaluma ya uhandisi miongoni mwa vijana nchini.