Kilolo. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika miaka mitano ijayo, wanakwenda kuboresha huduma za afya kuwa bora na za kisasa kwa wananchi wa Kilolo, mkoani Iringa.
Wakati Dk Nchimbi akiahidi hayo, mgombea ubunge wa Kilolo, Ritha Kabati ameiomba Serikali kuliangalia kwa jicho la kipekee eneo la Mlima Kitonga kwa kuanzisha barabara ya mchepuko ili kuondoa adha wanayokutana nayo wananchi.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Septemba 25, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Isele, Jimbo la Kilolo ambapo Dk Nchimbi amemwombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, Kabati na madiwani.
Dk Nchimbi amesema Rais Samia tangu alipoingia madarakani amefanya kazi kubwa ya maendeleo na ndiyo sababu chama hicho kimempa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
“Rais Samia amedumisha umoja, mshikamano na usalama wa nchi yetu, ametekeleza ilani ya CCM kwa kasi kubwa. Ameboresha huduma za afya, elimu, miundombinu, viwanda kwa namna ambayo haijawahi kutokea,” amesema.

Amesema hata Kilolo yamefanyika mengi kwenye kila sekta na miaka mitano ijayo iwapo watapata ridhaa, wanakwenda kuboresha Hospitali ya Kilolo kwa kuiongezea majengo na vifaatiba.
“Tunataka kuwe na huduma za uhakiki na kisasa. Lakini pia tutajenga vituo vipya vitano, tutajenga zahanati kumi,” amesema.
Mgombea mwenza huyo ameahidi kuboresha zaidi miundombinu ya elimu ya Kilolo kwa kujenga shule mpya za msingi 12, za sekondari mpya nane na shule za zamani kutajengwa madarasa mapya 295.
“Majisafi na salama, tumedhamiria kujenga mfumo mzuri wa usambazaji maji na kukamilisha miradi mitatu inayoendelea na kuanzisha mipya mitatu,” amesema.
Wakulima na wafugaji hawapo nyuma kwani Dk Nchimbi amesema mbolea ya ruzuku itawafikia kwa wakati pamoja na mbegu ikiwemo maofisa ugani.
“Lazima watu wa Kilolo wanaojishughulisha na kilimo tuwatengenezee mazingira bora. Tumedhamiria kuanzisha mabwawa matano ili kusaidia mifugo yetu iwe salama, majosho na kujenga machinjio ya kisasa,” amesema.
Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin amesema heshima kwa wananchi wa mkoa huo kwa Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali.
“Kwa kazi kubwa iliyofanyika Iringa, tunataka mkoa wa Iringa iongoze na kurudi kwenye nafasi yake ya kuongoza kwa kura, tulifanya hivyo mwaka 2000 na 2005 na mwaka 2025 tunakwenda kurudi kwenye nafasi yetu,” amesema Yasin.
Alichokisema Kabati, Msigwa
Mgombea ubunge wa Kilolo, Ritha Kabati amesema umoja na upendo wa wananchi wa Kilolo watakwenda kupiga hatua ikiwemo kuwawezesha watoto wa kike kwenda na kuendelea na masomo kwani shule zipo.
Kabati amesema kulikuwa na tatizo la maji na miradi 14 imetekelezwa na kuwezesha kupunguza tatizo na vijiji 19 pekee kati ya 94 ndivyo havina maji na mikakati inaendelea.
Katika huduma ya umeme, Kabati amesema vijiji vyote 94 vina umeme na vitongoji 25 kati ya 320 havijaunganishwa. Barabara zinaendelea kukarabatiwa na kujengwa ili zipitike wakati wote.
“Tuna barabara ya Kitonga ni ya kibiashara, magari yamekuwa yanakwama, lakini Serikali imetoa Sh6 bilioni ili kuipanua na upanuzi umekwisha kuanza,” amesema Kabati.
Mgombea huyo amesema ili kuifungua zaidi barabara hiyo ijengwe barabara ya mchepuko.
Amefafanua kuwa kwenye maeneo yake, Dk Nchimbi amesema barabara mbalimbali za Kilolo na zinazounganisha wilaya hiyo na nyingine zitajengwa ili kurahisisha shughuli za usafirishaji na kufungua uchumi wa Kilolo.
Katika Mlima kitonga, imetanuliwa baadhi ya maeneo na kufungwa vioo vinavyowasaidia madereva kuangalia vyema kwenye kona za mlima huo wenye kuna nyingi.
“Kilolo yetu ya leo inahitaji kukimbia, Kilolo yetu inahitaji upendo na Kilolo yetu ya leo inahitaji mshikamano na anayeturudisha nyuma tumtenge ili tusonge mbele.
Nawaomba wana Kilolo kuweni na imani na mimi, nafahamu changamoto za Kilolo,” amesema Kabati aliyekuwa mbunge wa viti maalum ambaye sasa anawania jimbo kwa mara ya kwanza.
Aliyekuwa mbunge wa Kilolo, Justin
Nyamoga amesema anaungana na wana Kilolo kuzisaka kura za Rais Samia, mbunge (Kabati) pamoja na madiwani.
Naye Kada wa CCM aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema (2010-2020), Mchungaji Peter Msigwa amesema:”Rais Samia alichukua nchi ikiwa haiko vizuri, ikiwa katika kifungo cha kimataifa, aliichukua nchi ikiwa na miradi mikubwa, sisi wapinzani tukasema huyu mwanamke hataweza, lakini amepiga kazi kila mmoja anaiona.”
Mchungaji Msigwa amesema kwa kazi kubwa aliyoifanya Oktoba 29, 2025 wajitokeze kwa wingi ili kumpa tena nafasi ya kuendelea kuwatumikia: “Kwani ameonesha uwezo mkubwa usiokuwa na shaka hata kidogo, hivyo tumpe kura za kutosha.”
Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema Serikali chini ya Rais Samia imeboresha vilivyo huduma katika hospitali ikiwemo vifaa tiba na kuziboresha hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.
“Sasa hivi mama akiwa na ujauzito wa miezi miwili, anajua ndani mtoto amekaaje, yupo nje ya mfuko, kuna changamoto gani inajulikana yote haya ni kwa ajili ya Samia kuboresha huduma za wananchi anaowaongoza,” amesema Ally.