Salum Mwalimu atuma salamu za pole kwa familia ya Abbas Ali Mwinyi

Tunduma. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Fuoni na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kapteni Abbas Ali Mwinyi kilichotokea leo Septemba 25 katika Hospitali ya Lumumba, Unguja.

Akitoa salamu hizo leo Alhamisi, Septemba 25, 2025 akiwa Tunduma mkoani Songwe katika mwendelezo wa ziara ya mikutano yake ya kampeni amesema; “Nimepokea taarifa za kuondokewa na kiongozi na mbunge aliyemaliza muda wake wa Fuoni, Kapteni Abbas Ali Mwinyi, ambaye pia alikuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia CCM. Hili ni pigo si kwa familia ya mzee Mwinyi pekee, bali kwa familia nzima ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla.”

Mwalimu amesema Kapteni Abbas alikuwa mtaalamu mahiri aliyebobea katika masuala ya usafiri wa anga na baharini.

“Abbas alikuwa ni mmoja mwa watu wachache waliobobea kwenye masuala ya ndege na meli. Hakuwa na makelele, alikuwa mpole, msikivu, na mwenye weledi mkubwa. Mungu alimjalia vipaji viwili rubani na nahodha wa meli,” amesema na kuongeza;

“Nimejulishwa kuwa mazishi yanafanyika leo. Nitaangalia kama ratiba yangu itaniruhusu kufika, lakini kama itashindikana, familia ijue kwamba tuko nao pamoja katika kipindi hiki kigumu.”

Hata hivyo, taarifa zinasema mazishi yatafanyika kesho.

Katika salamu zake za pole, Mwalimu aliwafariji wanafamilia wote wa marehemu, akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, pamoja na uongozi mzima wa CCM kwa kuondokewa na kada na kiongozi wao muhimu.

 “Zaidi ya familia, nawapa pole wananchi wa Fuoni kwa kumpoteza aliyekuwa mwakilishi wao. Pamoja na tofauti zetu za kisiasa, Kapteni Abbas alikuwa kiongozi aliyeheshimika,” amesisitiza Mwalimu.

Mwalimu amesema Abbas atakumbukwa kwa mchango wake katika siasa na taaluma za anga na usafiri wa majini, akiwa miongoni mwa Watanzania wachache waliomudu majukumu ya urubani na unahodha kwa wakati mmoja.