Nsajigwa asaka rekodi Transit Camp

KOCHA wa Transit Camp, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, amesema miongoni mwa malengo yake makubwa na timu hiyo ni kuhakikisha anaipandisha Ligi Kuu Bara, licha ya ushindani mkubwa na makocha wenzake wazoefu katika timu mbalimbali za Championship.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kuachana na Namungo, alikokuwa kocha msaidizi chini ya Juma Mgunda.

“Natambua kuna makocha wazoefu na Championship lakini hilo kwangu ni changamoto ambayo nimeamua kupambana nayo, najua malengo ya timu ni kupanda Ligi Kuu Bara, hivyo, nitapambana ingawa natambua wazi haitokuwa rahisi,” alisema Nsajigwa.

Nsajigwa alisema kwa mwezi mmoja aliokaa na timu hiyo hadi sasa, amefurahishwa na jinsi wachezaji wanavyojituma katika uwanja wa mazoezi, jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri pindi Ligi ya Championship itakapoanza Oktoba 10, 2025.

Nsajigwa amejiunga na kikosi hicho cha maafande akiwa ndiye kocha mkuu baada ya Emmanuel Mwijarubi aliyeifundisha msimu wa 2024-2025 kuondoka, huku uongozi ukionyesha matumaini makubwa kwake kutokana na uzoefu wake katika soka la Tanzania.

Kwa msimu wa 2024-2025, Transit ilimaliza nafasi ya 14 katika Ligi ya Championship na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19 kati ya 30 ilizocheza, ikifunga jumla ya mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50.  

Baada ya kumaliza nafasi ya 14, Transit ikacheza mechi mbili za ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kubakia Championship, ambapo ilianza kwa kuitoa Kiluvya United kwa jumla ya mabao 3-2, kisha kuiondosha pia Rhino Rangers ya Tabora kwa jumla ya 4-1.

Kikosi hicho kilipanda rasmi Ligi Kuu msimu wa 2004-2005, kikiwa chini ya Kocha, Stephen Matata, ambapo mwaka 2005, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tisa na pointi zake 30, ikishinda mechi saba, sare tisa na kupoteza 12, kati ya 28 iliyocheza.

Mwaka 2006, ikashuka daraja kwa kuburuza mkiani mwa timu 16 na pointi 20, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20, kati ya 30 iliyocheza, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 21 na kuruhusu 48.